Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Eric James Shigongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kwa kutoa pongezi nyingi sana kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyofanya kazi kubwa sana katika elimu ya Taifa hili. Mheshimiwa Rais alifanya jambo moja kubwa ambalo limemtengenezea heshima kubwa mno. Alichukuwa mkopo kwa ajili ya UVIKO (COVID 19) lakini akatumia fedha mkopo ule wa COVID 19 kujenga madarasa elfu 15 nchi nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, that was the smart decision, katika Afrika hakuna kiongozi yeyote aliyechukuwa uamuzi wa namna ile. Alikuwa na uwezo wa kuamua anunue barakoa au anunue sanitizer lakini akaona jambo la maana sana kwa watu wake ni kujenga madarasa. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Buchosa namshukuru sana Mheshimiwa Rais na tumejenga madarasa 128, hivi ninavyozungumza watoto wanakaa kwenye madarasa mazuri yaliyotengenezwa vizuri. Ahsante sana Mheshimiwa Rais na Waheshimiwa Wabunge naomba tumuunge Rais wetu mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashangaa kwa nini hampigi makofi ya kutosha kwa Mheshimiwa Rais. Nianze na kitu kinachoita form four certificate dilemma, dilemma ya cheti cha form four. Kabla sijakugusa cheti cha form four nisiache kumshukuru kwanza Profesa Mkenda kwa kazi kubwa ambayo ameanza nayo kwenye Wizara ya Elimu, Profesa namwamini sana, nilikuwa na mpango wa kushika shilingi lakini kwa mambo anayoyafanya sitashika shilingi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Naibu Waziri, ndugu yangu Mheshimiwa Kipanga, anazunguka Tanzania nzima kama pier kwenda kila wilaya kuangalia maendeleo ya elimu. Nampongeza sana Naibu Waziri kwa kazi nzuri. Nachukua nafasi hii pia kumpongeza sana Katibu Mkuu wa Wizara hii Profesa Eliamani Sedoyeka. Kwa kweli namfahamu Katibu Mkuu huyu tangu akiwa Chuo Cha Uhasibu Arusha kwa mambo aliyoyafanya pale Arusha. Aliingia Chuo Cha Uhasibu Arusha kikiwa kwenye hati ya kufungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, chuo hiki kilikuwa na wanafunzi kama sikosei 2,000, amekaa pale si zaidi ya miaka miwili, ameacha kina wanafunzi elfu 10 na kitu na tayari kina majengo ya ghorofa. Kwa hiyo naamini ujio wake kwenye Wizara ya Elimu, hatakubali hata siku moja kuharibu rekodi yake. Kwa hiyo rekodi yake iliyomsababisha akapewa Ukatibu Mkuu aendelee nayo na Watanzania wanufaike kwa kiasi kikubwa sana na umahiri wake. Niwashukuru Manaibu Makatibu Wakuu na pia niwashukuru watumishi wote wa Wizara ya Elimu, tuna kazi kubwa sana kwa ajili ya elimu ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nizungumzie dilemma cheti cha form four. Wengi mnafahamu mimi sikupata nafasi ya kusoma elimu ya sekondari, lakini kwa neema ya Mwenyezi Mungu na kwa kipaji ambacho Mungu alinipa cha uandishi nilitathiminiwa na TCU nikakubaliwa kusoma Chuo Kikuu kwa mfumo uliokuwa unaitwa RPL Recognition of Prior Learning na nikamaliza Chuo Kikuu vizuri kabisa. Nilipotaka kufanya masters Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nikakataliwa nikaambiwa huna cheti cha form four na hayo ndio imekuwa vita yangu profesa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshazungumza sana na Mheshimiwa Profesa na dada yangu Mheshimiwa Ndalichako anakumbuka vizuri sana kwa mapambano yangu mimi na yeye humu Bungeni, kwamba haiwezekani mtu nina shahada ya kwanza TCU wamenikubalia, halafu Chuo Kikuu wanakataa nisifanye masters kwa sababu sina cheti cha form four. Hii haiwezekani, wanawanyima watu haki ya elimu, kuna watu wengi nchi hii wamebuni vitu vingi, watu wametengeneza umeme bila elimu ya sekondari, wanajenga nyumba bila elimu ya sekondari, wanataka kusoma Chuo Kikuu wanakataliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Profesa Mkenda, aichukue kazi hii na kazi yangu hii aweze kulikamilisha jambo hili. Namwamini mno Mheshimiwa Profesa na tumeshazungumza mara nyingi sana kuhusu suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Profesa Ndekidemi anafahamu, kuna mtu mmoja kwenye Taifa hili lazima nimtolee mfano, alikuwa gardener kwenye chuo kimoja cha kilimo, akawa anatengeneza garden nzuri sana na kwa sababu hiyo Wazungu wakaona anafaa kusoma diploma, akapelekwa kusoma diploma, akamaliza best student kwa diploma kutunza gardener.

Mheshimiwa Naibu Spika, alipomaliza hiyo kozi ya gardener, wakasema aaa, umemaliza na distinction, basi distinction yako tunakupeleka kusoma Uingereza, akapelekwa Uingereza kusoma, from a gardener akaenda kufanya degree ya kwanza ya mambo ya kilimo na degree ile akarudi Tanzania baada ya miaka mitatu akarudi na masters, ndani ya miaka mitatu. Alipofika Tanzania, Tanzania yangu, nchi yangu, inayothamini cheti cha form four, alipotaka kufanya masters akaambiwa huwezi kufanya masters huna cheti cha form four.

Mheshimiwa Naibu Spika, huyu mtu yupo ukitaka nikuletee nakuletea na Profesa Ndekidemi yupo pale ni shahidi wangu. Yule mtu ikabidi aache kufundisha aende akasome QT Tanzania, Profesa Mkenda, akaenda kusoma QT miaka miwili, alipopata cheti cha form four ndiyo akafanya PhD na leo ni Profesa, the best professor in the country. Mimi binafsi siko tayari na nimesema sitashika shilingi, namwomba sana Waziri Profesa Mkenda hili jambo ni la kisheria, alete sheria Bungeni tubadilishe ili Watanzania wapate nafasi ya kusoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kengele ya kwanza kulia, sasa nitoe mchango wangu, nina mambo mawili tu. La kwanza medium of instruction, lugha ya kufundishia. Kwa muda mrefu sana nchi yangu imevutana tufundishe kwa Kiswahili, tufundishe kwa Kiingereza, mvutano huu mpaka lini?

Sasa ni wakati wa kufanya maamuzi, mwanangu anasoma darasa la kwanza kwa Kiswahili mpaka darasa la saba kwa Kiswahili. Akianza form one anaanza kwa Kiingereza. Ile transition ya kutoka Kiswahili kwenda kwenye Kiingereza tunapoteza watoto wengi wenye akili form one atakuwa anajifunza Kiingereza. Form two anajifunza Kiingereza form three kaanza kuelewa Kiingereza kidogo, mtihani wa form four umefika anapata division zero.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri na nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge kwa umoja wetu tuamueni tunataka tufundishe Kiingereza au Kiswahili.

WABUNGE FULANI: Kiingereza.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Kiingereza.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hili nisiliseme nimwombe Mheshimiwa Waziri, afanye utafiti aje na majibu ya watu wanataka tufundishe kwa lugha ipi, tuwe na lugha ya kufundishia ili tuwasaidie watoto wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni suala zima la mitaala ya elimu, limezungumzwa. Dunia inakwenda kwenye fourth industrial revolution, mapinduzi ya nne ya viwanda, lazima mitaala yetu ili-reflect kule tunakoelekea hatuwezi kuendelea kuwafundisha watoto wetu kwa mambo ya second industrial revolution kwa mambo ya third industrial revolution, hatuwezi kufanikiwa. Tutakapofika mapinduzi ya nne ya viwanda ambayo kutokana na mambo ya intelijensia ya bandia niseme hivyo, mambo ya five technology, cloud computing, lazima tuwaandae watoto wetu tuanze kuwafundisha kuanzia primary schools, kuna shida gani kumfundisha mwanangu coding akiwa primary school, kuna shida gani? Hatutaki kufanya maamuzi, matokeo yake shule za binafsi watoto wanaandaliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachotokea, huko mbele tunaandaa matabaka ya watu wawili; watoto wenu hapa watakuwa na nafasi kuliko watoto walioko vijijini, hatutaki Tanzania ya aina hiyo. Tunataka Tanzania yenye usawa, kwa hiyo naomba waache maandalizi mtaala huu, tufikirie sana kuwapa watoto wetu elimu ya computer toka Shule ya Msingi. Walimu tunao, hatuna sababu yeyote ile ya kutofanya jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ni suala la maslahi ya Walimu. Ukitaka kufanikiwa kwenye elimu mfurahishe Mwalimu, basi. Walimu lazima wawe na furaha katika nchi yetu, najua wananisikiliza, Walimu wanaouza visheti…

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Shigongo.