Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Prof. Kitila Alexander Mkumbo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ubungo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na Mwenyekiti wangu wa Kamati Mheshimiwa Nyongo kwa kupongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake yote akiwepo Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi kubwa wanayoifanya. Niwapongeze sana kwa maboresho ambayo yanaendelea kuboresha sera pamoja na mitaala yetu, tunawatakia kila la kheri na sisi tutawapa ushirikiano wote kama Kamati.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatekeleza dira ya maendeleo na Mpango wetu wa Tatu wa Maendeleo, nyenzo kubwa ya kutekeleza hayo ni uwekezaji katika rasilimali watu. Nyenzo kubwa ya kujenga rasilimali ni elimu na nyenzo kubwa ya kutoa elimu ni Walimu. Mchango wangu leo ni kuhusu Walimu na hasa kwenye kuchangia kwenye maboresho ambayo yanaendelea katika taaluma ya ualimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Profesa Issa Shivji aliwahi kusema, mmoja wa maprofesa maarufu hapa Profesa wa kisomo, ukitaka Taifa bora boresha elimu, ukitaka kuboresha elimu boresha Walimu, ukitaka Taifa la watu wanaojiheshimu heshimu Walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwalimu Nyerere aliwahi kusema na namnukuu pia, alisema kwa Kiingereza: “No education policy however good can succeed, without well trained professional carder.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo maboresho ambayo tunayafanya haya ya kisera na kimitaala, yatafanikiwa sana kama yakienda sambamba na uwekezaji katika taalum ya ualimu na Walimu wenyewe. Kada ya ualimu Tanzania ina changamoto nyingi lakini naomba nizitaje tatu tu na nitoe mapendekezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tumeshasema na Mheshimiwa Mwenyekiti wangu amesema tuna changamoto ya uhaba wa Walimu tulishalisema hapa, tuna upungufu sasa hivi 175,000 takriban 40% lakini changamoto kubwa zaidi ni kwa upande wa Walimu wa sayansi. Kwa sasa kwa mfano tunahitaji Walimu wa sayansi na hesabu 70,327, waliopo ni 23,647, unazungumzia upungufu wa 66%, takriban theluthi mbili, huwezi kujenga uchumi wa viwanda bila sayansi, hesabu na teknolojia. Kwa hiyo, ni lazima tuwekeze katika ku-train Walimu wa hesabu, sayansi na teknolojia.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2026 tutakapomaliza kutekeleza mpango wetu wa maendeleo ambao tunao, inakadiriwa kwamba tutakuwa na wanafunzi wa elimu ya awali msingi na sekondari 23,600,000. Hawa tutahitaji Walimu 724,000, maana yake changamoto ni kubwa. Kwa hivyo tunazungumzia ili tuweze ku-cover hizi changamoto tufikie hayo malengo ambayo tumejiwekea, tunahitaji kuajiri Walimu kila mwaka takriban Walimu 100,000. Sasa hivi tunaajiri Walimu 10,000 hiyo itachukua miaka zaidi ya 18 kuweza kuziba pengo. Sasa hiyo ni changamoto ambayo lazima tuione.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya pili kwa upande wa Walimu ni kwamba, Mwalimu ana mabosi wengi mno. Moja Mwalimu anaajiriwa na Mkurugenzi wa Halmashauri, anapandishwa cheo na Tume ya Utumishi ya Walimu, Mwalimu akiwa na shida ya mshahara wake inabidi aende kwa Katibu Mkuu Utumishi, Mwalimu akiwa na changamoto na mitaala inabidi aende Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Juzi mwaka 2018 tukaunda Bodi ya Walimu inaitwa Tanzania Teachers Professional Board ambayo ipo upande wa Wizara ya Elimu maana yake na yenyewe inakwenda kumbebesha Mwalimu mzigo.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya tatu kwa leo ni ukweli kwamba ambayo wote tunajua ni maslahi duni kwa Walimu wetu na kukosekana kwa motisha. Nataka nitumie muda uliobaki nitoe mapendekezo saba kwa ajili ya kuboresha na kutatua hizi changamoto ninazozizungumza. Mapendekezo saba ambayo yataingia Mheshimiwa Waziri akiyapenda aingize katika mchakato wake wa maboresho. Changamoto ya kwanza kuhusu kupunguza upungufu wa Walimu napenda kutoa mapendekezo manne ambayo yatatusaidia kupata Walimu 44,000 kwa kila mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, hakuna shaka kwamba Serikali pekee yake kwa ukubwa wa changamoto ya Walimu kwa maana ya idadi haitaweza kuijibu hii changamoto, kwa sababu tunazungumzia kuajiri Walimu 100,000 kila mwaka, maana yake Serikali iache shughuli zingine zote ishughulike Walimu tu, hicho hakitawezekana. Napendekeza Serikali tuweke mazingira mazuri ya kuvutia sekta binafsi kuwekeza katika elimu kwa sasa kwa mfano katika elimu ya msingi tupo chini ya 10% ya shule ambazo zinamilikiwa na private sector, kwa nini? Kwa sababu nyingi lakini mojawapo ni kwamba tuna kodi 13 katika shule. Ukianzisha shule hapa, utalipa kodi 13 haya mazingira yanafanya ada ziwe kubwa, mazingira yanafanya watu washindwe kufungua shule.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wetu wa halmashauri waelekezwe kwamba wewe kufungua shule hapa City Council Dodoma, mtu akifungua shule yake wanafunzi wanaokwenda pale, inamsaidia Mkurugenzi wa Halmashauri kwa sababu wale wanafunzi, vinginevyo angewabeba yeye, lakini Wakurugenzi wetu wanakimbilia sana ile service levy, kwa hiyo tuweke mazingira hayo. Tukifanya hivyo tunakadiria kwamba tuna uwezo wa kuongeza Walimu mpaka tukapata Walimu 5,000 kutoka private sector.

Mheshimiwa Naibu Spika, pendekezo la pili, Serikali iweke malengo ya kuajiri Walimu 20,000 mpaka 30,000. Tukiwaajiri Walimu 20,000 inaweza ikasaidia kuliko kuajiri walimu 10,000. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pendekezo la tatu, muda wa mafunzo ya ualimu katika Vyuo Vikuu uongezwe, uwe miaka minne na ule mwaka wa nne wote utumike kwenye mafunzo mashuleni. Kwa hiyo tutapata Walimu kati Walimu 15,000 mpaka Walimu 20,000 kila mwaka kutoka katika vyuo vikuu na hawa hatuwalipi wanaendelea kulipwa na Bodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pendekezo la mwisho hapa, tupunguze nafasi ya utawala katika elimu, tufute kada ya Maafisa Elimu Kata, tuimarishe menejimenti ya shule ili watu hawa waende kufundisha. Tunazungumzia kupata Walimu 3,956, hakuna sababu ya kuwa na Maafisa Elimu wa Kata, hakuna sababu kama tuna uongozi imara wa shule, kwa nini tuwe na Afisa Elimu wa Kata, kwa hiyo tuondoe hiyo watu wakafundishe.

Mheshimiwa Naibu Spika, pendekezo la mwisho kwenye upande wa motisha, sasa niingie kwenye motisha kwa sababu ya muda ni suala la motisha kwa Walimu. Naomba kwa heshima na taadhima turudishe posho ya kufundisha kwa Walimu (teaching allowance). Tunazungumzia kitu kidogo, tunazungumzia Sh.4000 kwa siku kwa Mwalimu, maana yake kwa siku tano Sh.20,000 kwa mwezi Sh.100,000. Hii itahamasisha Walimu, ilikuwa ni vitu muhimu sana, walimu wameshaomba mara nyingi, Waziri wa Fedha yupo hapa, hatuwezi kushindwa kuweka Sh.100,000 kwa Mwalimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, tunaomba Teachers Service Commission…

NAIBU SPIKA: Waziri wa Fedha nimesikia taarifa au siyo wewe? Siyo wewe au basi endelea.

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Naomba Teachers Service Commission ipewe nafasi ya kufanya kazi kikamilifu. Kwa kufanya hivyo, hatuna sababu ya kuwa na Teachers Professional Board kwa sababu majukumu yake mengi yapo ndani ya Teachers Service Commission.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie mchango wangu kwa shukran za pekee kwa hili ambalo limefanyika hapa watu wengi wanalichukulia ni mafuta tu, lakini kitendo cha Mheshimiwa Rais cha kusikiliza maoni ya Bunge, akaheshimu badala ya kutangaza mwenyewe jana akaamua kuleta hapa, ni kiwango cha juu cha kuheshimu utawala bora. Ameliheshimisha Bunge na sisi Wabunge tuna wajibu wa kumheshimiwa Mheshimiwa Rais. Tunampongeza kwa hatua hii, tutaendelea kumuheshimisha, tutaendelea kutoa maoni ya kujenga ili Serikali yetu iende vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)