Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 6 Mei, 2022 niliwasilisha katika Bunge lako Tukufu hotuba ya bajeti ya Wizara yangu ikiainisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka, 2022/2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukushukuru, Mheshimiwa Spika pamoja na Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ambavyo mmeongoza na kusimamia vyema majadiliano ya bajeti ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara. Nawashukuru pia Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao waliyotoa kwa njia ya kuzungumza na maadhishi pia, maoni na ushauri wenu tumeuchukua kwa ajili ya kuufanyia kazi ili tuweze kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kuwa ninatambua na kuthamini dhamira na nia njema iliyotawala mjadala huu ambao kimsingi ulilenga kuboresha mikakati na mbinu za kisekta, zitakazotekelezwa katika mwaka 2022/2023 na hata kuelekea mbele zaidi na hivyo kutoa mchango unaotakiwa kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishukuru sana Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile Mbunge wa Mufindi Kusini na Makamu Mwenyekiti wetu Eric James Shigongo Mbunge wa Buchosa, pamoja na Waheshimiwa Wajumbe wote wa Kamati kwa maoni na ushauri mzuri waliotupatia kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi ndani ya Wizara yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Martha Nehemia Gwau Mjumbe wa Kamati, kwa kuwasilisha vema Taarifa ya Kamati kwa niaba ya Mwenyekiti, hongera sana. Aidha, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia kuanzia mwanzo mpaka mwisho na kipekee kabisa, naomba pia nimshukuru Kaka yangu Mheshimiwa Mohamed Hussein Bashe Waziri wa Kilimo kwa kuchangia hoja hii na kutoa ufafanuzi wa hoja ambazo zimeibuliwa na Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa napenda kumshukuru Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mheshimiwa Exaud Silaoneka Kigahe Mbunge wa Mufindi Kaskazini, kwa kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninawashukuru Watendaji wote ndani ya Wizara yetu wakiongozwa na Katibu Mkuu kwa kuweza kufanya kazi usiku na mchana, hadi leo tunaelekea kuhitimisha mjadala huu wa hotuba ya Bajeti ya Wizara yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea pongezi nyingi za utendaji wa Wizara na Taasisi zake kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge nasi tunaahidi kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kwa ari zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, tumepokea michango mingi ambayo ni chachu katika kuleta maendeleo ya uchumi wa nchi yetu, hususani kupitia sekta yetu ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara. Napenda kuwahakikisha Waheshimiwa Wabunge kuwa maoni na ushauri wenu na maelekezo ya Bunge hili katika kujadili bajeti ya sekta hii tutayazingatia kuyafanyia kazi ikiwemo kutoa mrejesho wa utekelezaji. Aidha, kutokana na muda mfupi tulionao hadi kuhitimisha hotuba hii, maelezo na majibu ya kina ya michango mbalimbali yameandaliwa na tutayawasilisha kwa maandishi kwa Ofisi ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwatambua Waheshimiwa Wabunge waliochangia hotuba ya bajeti ya Wizara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya Waheshimiwa Wabunge waliochangia ni Wabunge 29 na kati ya hawa Waheshimiwa Wabunge 23 wamechangia kwa kuzungumza hapa Bungeni na Waheshimiwa Wabunge Sita wamechangia kwa maandishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo ya utangulizi naomba sasa nitoe ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge katika kujadili hoja hii niliyowasilisha kama ifuatavyo: - (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ridhaa yako niruhusu nijikite katika hoja moja au mbili ambazo ni msingi mkubwa wa mjadala huu wa siku hizi mbili za kujadili hotuba ya bajeti yetu. Hoja yenyewe inaweza kuwa imebeba michango yote ya Waheshimiwa Wabunge nayo ni hoja iliyosemwa na Waheshimiwa Wabunge wengi kuhusu hali ya sekta ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, lakini ikiunganishwa na hali inayoendelea duniani hali ya mfumuko wa bei katika bidhaa mbalimbali na mwishoni ikionekana kama Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi inaendeshwa bila maono wala dira naomba niseme yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna nchi duniani iliyofikia hatua ya juu ya maendeleo bila kuwa na mageuzi ya uchumi wa viwanda. Hata hivyo, nadharia ya maendeleo ya kiuchumi (Theory of Economic Development) inabainisha kwamba ipo misingi muhimu misingi mikuu ambayo nchi ama Taifa hutakiwa kuwanayo ili kufikia hatua yoyote ile ya maendeleo. Misingi hiyo ni uwepo wa miundombinu wezeshi kwa ajili ya shughuli endelevu za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukirejea kwenye nadharia ya uchumi wa miundombinu (The Economics of Infrastructure) inatueleza miundombinu hii wezeshi uwekezaji wake ni mkubwa na hakuna Taasisi ama Sekta binafsi yoyote yoyote ambayo ipo tayari kuwekeza kwenye miundombinu, lazima miundombinu hii wezeshi iwekezwe na Serikali yenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu hii wezeshi ni pamoja na miundombinu ya barabara ni pamoja na miundombinu ya usafirishaji wa reli, usafirishaji wa anga, miundombinu ya afya, miundombinu ya elimu yote hii lazima iwepo kama tunataka kuona matokeo makubwa ya uchumi wa viwanda ndani ya Taifa lolote duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nchi yetu Tanzania ilikuwa ni muhimu sana tulipopata uhuru mwaka 1961 kuwa na mipango ya muda mrefu na mipango ya muda mfupi. Nichukue fursa hii, kuwapongeza sana Viongozi wetu wa Serikali ambao wote wametokea Chama cha Mapinduzi kuanzia Serikali ya Awamu ya Kwanza Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere nampongeza kwa dhati ya nafsi yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mzee wetu Alhaji Ali Hassan Mwinyi nampongeza kwa dhati ya nafsi yangu alifanya makubwa kuhakikisha, nadharia hizi za uchumi zinafikiwa na Taifa letu linanufaika na mapinduzi ya viwanda. Nampongeza sana Mzee wetu Hayati Mkapa alifanya makubwa. Nampongeza sana Rais wetu mstaafu wa Awamu ya Nne Jakaya Mrisho Kikwete alifanya makubwa kuhakikisha Taifa letu linanufaika na uchumi wa viwanda.

Nampongeza sana Hayati Dkt. John Pombe Magufuli amefanya makubwa na sasa nampongeza sana Mama mlezi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anafanyakazi kubwa kuhakikisha yale yote yaliyofanywa na watangulizi wake yanazaa matunda yanayotakiwa. Pongezi nyingi na niliombe Bunge lako Tukufu tusimkatishe tamaa Rais wetu anafanyakazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ipi ilikuwa dira yetu baada tu ya kupata uhuru. Baada ya kupata uhuru dira yetu ilikuwa ni kuwa na Taifa huru katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Hivyo, ili tuweze kufika huko kama Taifa ilitulazimu tuanze hatua moja kwenda hatua nyingine na ndipo aliposema Mheshimiwa Waziri wa Kilimo viwanda vilijengwa katika Serikali ya Kwanza ni sahihi kabisa, lakini kuna kiwanda kilichojengwa eneo moja la nchi unazalisha bidhaa ambazo hakuna miundombinu ya kupeleka sokoni unakwenda kuzalisha tunachokiita botanic inflation. Kwa hiyo, kifo kile kilikuwa ni kifo cha kiuchumi na wala hatutakiwi kujilaumu na kwa sababu tuna Serikali makini, ndio maana tukarudi kwenye nadharia zote za kiuchumi na sasa tuko sehemu sahihi ya kunufaika na mapinduzi ya nne ya viwanda ambayo dunia nzima ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yalisemwa sisi watanzania kweli tulalamike kuhusu mafuta kutoka Ukraine, mafuta kutoka Malaysia ambayo yameshindwa kufika nchini ni sahihi. Kwa sababu, tulianza na utekelezaji wa mipango mingine huko nyuma, naomba nianzie na Mpango wa kwanza wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano tulioanza kuutekeleza mwaka 2011/2012 hadi mwaka 2015/2016. Mpango huu ulilenga kufungulia fursa fiche za ukuaji wa uchumi baada ya kuwa tumesoma tumerudi kwenye Structural Adjustment tumeona haifanyikazi, wachumi wa Taifa hili wakafanya kazi yao na sasa tukaanza mwelekeo sawasawa wa kwenda kunufaika na mapinduzi ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu ulitaka kuhakikisha kuwa Taifa letu linakuwa na miundombinu sahihi kwa ajili ya kuwezesha shughuli zingine za maendeleo kuelekea kwenye uchumi wa kati na wa juu. Ni katika kipindi hiki ndipo tulipoona kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliona ukarabati wa reli ya kati yenye urefu wa kilomita 2,707 ambapo huko nyuma tuliona matatizo makubwa ya miundombinu hii lakini tulikarabati na mwendo ukaendelea. Tukahakikisha kuna jengo la kukarabati kilomita 2,775 za barabara za lami kwa mara ya kwanza ndani ya Taifa letu tukielekea kuufungua uchumi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukaona maboresho makubwa katika Bandari ya Dar es Salaam ambako uwezo wa kuhudumia shehena ya mizigo uliongezeka kwa kiwango kikubwa. Tukaona kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme kutoka megawati 900 mwaka 2010 hadi megawati 1,246 mwaka 2015.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukazalisha chakula cha kutosha hadi asilimia 125 ya chakula kikazalishwa. Tukaona miundombinu ya elimu shule za kata zikajengwa kwenye kila Kata ndani ya Taifa letu. Tukaimarisha miundombinu ya afya na lishe katika ngazi zote kwa wakazi wote wa Mijini na Vijijini. Huwezi kuwa na Tanzania ya viwanda kama huna jamii ambayo iko imara kiafya na ambayo imeelimika. Hii ilikuwa ni mpango wa kwanza wa maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa Pili wa Maendeleo ambao ulisemwa hapa Serikali ya Awamu ya Tano ilikuwa ya viwanda; viko wapi viwanda? Viwanda tunavyo na nimetaja kwenye hotuba ya bajeti yangu. Mpango wa Pili wa Maendeleo ulikuwa na dhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya uchumi na maendeleo ya watu. Lengo kuu la pili lilikuwa ni kurekebisha mapungufu yote ya mpango wa kwanza ili tuweze kuendelea kutembea mguu sawa kuelekea mapinduzi ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwenye mpango huu ndipo tulipoona Serikali ya Awamu ya Tano ya Chama cha Mapinduzi ikiongozwa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na msaidizi wake Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, tukianza ujenzi wa reli ya kisasa ili kuhakikisha sasa viwanda vyote vilivyojengwa vikizalisha bidhaa ichukue muda mfupi bidhaa hizo kufika bandarini na kusafirishwa nje ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona mradi mkubwa wa kuzalisha umeme. Huwezi kuwa na viwanda kama huna umeme wa kujitosheleza. Tunao mradi mkubwa wa umeme unaokwenda kuzalisha megawati 2,115 ambao hatuna muda mrefu mradi huu unakamilika. Ni maandalizi ya uchumi wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi kwenye ziara ya Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan, moja ya hati za makubaliano tulizosaini ni mkataba wa kibiashara kati ya Jiji ya Dallas na nchi yetu ya Tanzania. Jiji la Dallas liwe kama lango la biashara ya bidhaa zinazozalishwa Tanzania kwenda kuuzwa katika Bara la Amerika yote Kaskazini na Kusini, lakini Tanzania kiwe kama kituo kikuu cha biashara kwa Afrika ya Mashariki, kwa Afrika ya Kusini na Nchi za Afrika ya Kati. Biashara zote zinazotoka duniani zipite Bandari ya Dar-es-Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ndiyo tunayoyafanya kuelekea uchumi wa viwanda na kupitia utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo tukaona mradi wa kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) inafanya kazi ndani ya nchi na nje ya nchi. Huwezi kuingia mikataba ya biashara na wenzako, wenzako wakaleta ndege zao wewe usifanye hivyo, hapana. Moja ya kipengele kwenye mkataba huu ni kuwa na mkataba mwingine mdogo (Open Skies Agreement), niishukuru Wizara ya Uchukuzi inahitimisha mkataba huo ili sasa na sisi ndege zetu ziweze kuruka kuelekea duniani kupitia Dallas. Haya yote yamewezekana kwa sababu tumetekeleza mpango wa pili wa maendeleo tukifungua zile fursa fiche, miundombinu wezeshi kwa ajili ya uchumi wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya msingi, Mpango huu wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano pia ulijikita katika kujenga viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini, hususan katika sekta za kilimo, madini na gesi asilia na uzuri takwimu huwa zinaongea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya viwanda utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo tulifikia asilimia 105 ya malengo tuliyokuwa tumejiwekea. Kwa mara ya kwanza tukaona mchango wa sekta ya viwanda kwenye pato la Taifa ukifikia asilimia 25.1, ni mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kasi ya ukuaji wa shughuli za uzalishaji iliongezeka kutoka asilimia 5.2 hadi asilimia 8.5, huku tukiona mchango wa sekta ya madini ukikua kwenda kufikia asilimia 12.6 kutoka asilimia 6.9. Hii ni kwa sababu miundombinu wezeshi yote ilishafanya kazi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunatekeleza Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano tulioanza kuutekeleza mwaka 2021/2022 na tunakwenda kuhitimisha mwaka 2025/2026, ambao ni muendelezo wa Mpango wa Kwanza na wa Pili na lengo lake kuu sasa ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge mmesema vizuri sana, lazima viwanda hivi vitambue watu wetu nini walichonacho. Ndio maana sasa baada ya kuona miundombinu wezeshi yote imekamilika nchi yetu imefunguka kwa miundombinu. Bidhaa itakayozalishwa kwenye kona yoyote ya Taifa letu ina uwezo wa kusafiri kwenda eneo lingine lolote ndani ya Taifa letu kwa muda mfupi. Ndani ya mpango huu ndio tunamwona kiongozi wetu makini, jasiri, Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wetu, anaelekeza bajeti kwenda kwenye sekta za uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Bashe, amesema vyema. Hotuba ya bajeti yake inakwenda kuongezeka kwa kiwango kikubwa. Hiyo yote ni kuwezesha viwanda vyetu vipate malighafi tayari kwa uzalishaji ili tuweze kusafiri salama kwenye safari ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu imefunguka kama nilivyosema kwa miundombinu yote ya msingi kuelekea uchumi shindani na wa viwanda. Pongezi nyingi kwa Serikali yetu ya Awamu ya Sita na Serikali nyingine zote ambazo zimeongozwa na wazalendo wa Taifa letu waliojua vipaumbele vya Taifa letu kuelekea kwenye nchi ya maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa. Ndio maana tunaona sasa jitihada kubwa anayoifanya Mheshimiwa Rais wetu ni kuueleza ulimwengu Taifa letu liko tayari sasa kwa safari ya kimaendeleo. Tuko tayari na wawekezaji tumefungua milango ili waje kuwekeza kwenye maeneo yote ya kiuchumi ndani ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona mikataba ambayo tumesaini, hati zote za makubaliano 44 zote zinawaelekeza wawekezaji kuja kuwekeza katika sekta za uzalishaji, katika sekta za viwanda. Ndio maana mpaka kufika mwaka 2025 tutakuwa hatuna tena upungufu wa sukari nchini Tanzania, tutazalisha kutoka Tanzania, kutoka kwenye viwanda vidogovidogo na viwanda vikubwa na jitihada hiyo ni pamoja na uwekezaji kwenye eneo la Mkulazi ambalo Waheshimiwa Wabunge wamesema na tayari mwekezaji yuko site anafanya kazi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunakwenda kutumia teknolojia zote, teknolojia za kati, teknolojia za juu, ili kuhakikisha viwanda vidogovidogo, vya kati na vikubwa vinawekezwa. Ndio maana tuna kongani za viwanda kule Kitaraka, Manyoni, lakini tuna kongani za viwanda pale Kwala, Kibaha na tuna kongani za viwanda hapa Nala, Dodoma. Tunachotaka kufanya ni kuihudumia dunia kutoka Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge ambao wametusemea kwamba, tuongezewe fedha, lakini wamekiri sisi ni Wizara inayoratibu uwekezaji na viwanda. Uwekezaji na viwanda hivi upo kwenye sekta nyingine za kiuchumi na tunafanya kazi kwa karibu zaidi na sekta zote; sekta ya madini, sekta ya kilimo, sekta ya fedha tunafanya kazi kwa karibu kuhakikisha haya yote yanafanikiwa. Tuko kwenye majadiliano na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuona viwanda vilivyopo kwenye mifugo na uvuvi tunavipaje kipaumbele ili vinufaike na mafanikio makubwa haya. Kwa hiyo, niwatoe hofu tunafanya kazi hii kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo niseme tu Taifa letu lina dira ya muda mrefu na lina dira ya muda mfupi. Mipango yote hiyo inapitishwa na Bunge lako Tukufu kwa ajili ya utekelezaji. Kikubwa niwaombe Waheshimiwa watuunge mkono ili tuweze kuyatimiza haya yote mazuri tunayoyapanga kwenye sekta hii ya uwekezaji, viwanda na biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema nianze na jambo hili na moja dogo la pili ambalo napenda kulisemea kabla muda wangu haujaisha ni mradi wa kimkakati wa Liganga na Mchuchuma. Tumesikia Bunge lako limesema na limekiri ni mradi wa muda mrefu. Tunafanya kazi kwa karibu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuona tunapohitimisha mjadala na mwekezaji wetu Taifa letu linaendelea kuwa salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze timu yetu ya kitaifa ya majadiliano imefanya kazi yake nzuri na sasa jambo hili liko mikononi mwa Waziri wa Uwekezaji na Mwanasheria Mkuu wa Serikalim. Tunaliahidi Bunge lako Tukufu tunakwenda kulihitimisha. Nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Ludewa, ndugu yangu Mheshimiwa Kamonga, alitahadharisha kuhusu mgongano wa sheria mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inafanya kazi kuona hakuna mgongano wa sheria hizi mbili, Sheria ya Ardhi pamoja na Sheria ya Uthamini ili tuweze kufika hatua njema kwa ajili ya wananchi wetu na wananchi wetu waweze kufanikiwa. Jambo ambalo naweza kuahidi ni kwamba, Wizara yangu pamoja na Mthamini Mkuu wa Serikali tutafanya ziara na kuongea na wananchi wa vijiji hivyo viwili ili tuweze kuhitimisha jambo hili kwa mafanikio makubwa kati ya Serikali, wananchi wetu, pamoja na mwekezaji wetu. Hivyo, nimtoe shaka Mbunge, tuko tayari na muda mfupi mradi huu utaanza utekelezaji wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno haya, kabla ya kuhitimisha hoja yangu, napenda tena kuwashukuru kwa dhati Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja hii. Niwaombe tu tuendelee kushirikiana katika kuwatumikia Watanzania katika kuwaletea maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jitihada zinazofanywa na Serikali yetu kupitia Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan, zinatuhusu sisi sote. Tumemsikia jana Mheshimiwa Rais akisema ametusemea vizuri Watanzania; sisi ni wakarimu, wawekezaji wamemsikia wanakuja kwa wingi. Naomba tuwapokee na tushirikiane nao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wakati sasa, kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge mmoja, wa kutengeneza mabilionea kutoka ndani ya Watanzania waongezeke zaidi na wanaanza na sisi Waheshimiwa wawakilishi wa wananchi. Sisi Wabunge tushiriki, Taifa letu limefunguka na tunasema Tanzania is ready to take off, lazima na sisi tuwe ndani ya safari hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwahakikishie pia kuwa, Wizara yangu itaendelea kuilea na kuisimamia sekta binafsi ya Tanzania. Hakuna Taifa lililofanikiwa bila sekta binafsi. Ndio maana viwanda vingi kwa asilimia 90 vinashikiliwa na sekta binafsi.

Mimi nasafiri na sekta binafsi kama Waziri mwenye dhamana. Mheshimiwa Rais wetu kwenye safari zake zote anasafiri na sekta binafsi ili sekta yetu binafsi ishindane ndani na nje ya Taifa letu. Hivyo, tusafiri kwa pamoja kwenye safari hii ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno haya, naomba kutoa hoja. Ahsante sana. (Makofi)

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.