Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai kuweza kusimama hapa mbele na kuwasilisha bejeti hii; lakini kwa namna ya pekee nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini na kuendelea kufanya kazi kama Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara kumsaidia Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nipende kushukuru sana michango ya Waheshimiwa Wabunge kwa kuchangia kwa mtazamo chanya kwenye bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara ili kuendeleza kutimiza adhma ya ujenzi wa uchumi wa Viwanda nami nasimama hapa ili niweze kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji kwa kazi kubwa na umakini ambao anaoufanya katika kuendelea Sekta hii ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Mheshimwia Mwenyekiti, bajeti iliyowasilishwa imebeba dhamira kuu ya kuendeleza kasi ya uwekezaji na ujenzi shirikishi na unganishi wa Uchumi wa Viwanda kwa kutambua nafasi ya Sekta Binafsi; kama ambayo Waheshimiwa Wabunge wameeleza kama injini ya ujenzi wa Uchumi wa Viwanda na shughuli za ubia kwa Sekta Binafsi ya Umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kuwa mfumo huu wa maboresho na mengine yanayoendelea nchini likiwemo kutekeleza mpango wa kuboresha mazingira ya biashara kwa maana Blue Print unalenga kuboresha mazingira ya biashara na kushushia ari ya ujenzi wa uchumi wa viwanda na kuleta maendeleo endelevu katika nchi na wananchi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo haya ya awali na mimi niweze kuchangia kidogo kwanza kwenye hoja zilizotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira katika kuchangia bajeti hii. Kulikuwa na hoja kuhusu Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara ya TanTrade ambayo imechangiwa pia na Wabunge wengi sana, kuhusu kuona namna gani tunaweza kuisaidia ili kuhakikisha inatimiza wajibu wake kwa kufanya kazi ya kutafuta masoko ya bidhaa hasa mazao ya kilimo na bidhaa nyingine. Serikali inafanyakazi kubwa kuhakikisha tunawezesha taasisi zote ikiwemo hii ya TanTrade.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na katika bajeti hii tunayoendelea nayo sasa tulikuwa tumewapa fedha kidogo lakini mwaka huu tumeongezea kufikia bilioni 1.8 hii maana yake ni kuiwepo kwa dhamira njema ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha masoko ya bidhaa na hasa mazao ya kilimo yanapata masoko ya uhakika kwa kuhakikisha TanTrade inafanyakazi yake vizuri. Lakini Serikali itaendelea kuweka fedha zaidi kuhakikisha TanTrade inafanya kazi yake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kulikuwa na hoja kuhusu uandaaji wa kanzidata ya viwanda. Ni kweli Kanzidata ya viwanda ni moja ya matokeo ya utafiti na utambuzi wa viwanda ambayo huwa ni fursa kwa uwekezaji na wa rasilimali inayopata hapa nchini.

Kwa hiyo, kanzidata ni kweli itakuwa na taarifa sahihi za viwanda ikiwemo maeneo viwanda vilipo, ukubwa na uwezo wa viwanda hivyo na ajira ambazo zinatokana na viwanda hivyo. Lakini zaidi itaweza kutusaidia kujua malighafi zinazotakiwa kwa ajili ya kuzalisha bidhaa katika viwanda hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa taarifa hizo zitatusaidia pia kuona namna gani tunajua wapi kwa kuwekeza kwenye maeneo yapi, pia ambapo tunaamini yataleta tija. Sasa Wizara kupitia TIRDO tumeshaanza kazi hiyo kwa kushirikiana na taasisi zingine kama vile Ofisi ya Rais, TAMISEMI, NBS, BRELA na SIDO wanaendelea na uhakiki wa kukusanya takwimu za taarifa mbalimbali ambazo zitajumuishwa kwenye kanzidata ya viwanda katika Mikoa mbalimbali hapa nchini na sasa wameanza katika Mikoa ya Kanda ya Mashariki ikiwemo Morogoro na Mikoa mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja pia kwenye Kamati kuhusu uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji hapa nchini, ambao pia imechangiwa pia na Waheshimiwa Wabunge wengi. Wizara kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC) inakamilisha mfumo wa kielektroniki wa kutoa huduma ya mahali pamoja kwa wawekezaji (Tanzania Investment Electronic Single Window), ambayo itasaidia kuhakikisha tunaondoa baadhi ya changamoto na kupunguza urasimu usio wa lazima ambao umesababisha ucheleweshwaji kwa upatikanaji wa vibali kwa wawekezaji ikiwemo kujaza fomu nyingi na kujirudiarudia kwa sababu ya taasisi nyingi ambazo zinafanya kazi zinazofanana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo ni hoja chache kutoka kwenye Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nichangie kidogo kwa baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia katika bajeti hii hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja ya Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate ambayo aliongelea kuhusu umuhimu wa kuwezesha Bodi ya Maghala ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa uhakika na kwa ufanisi zaidi. Ni kweli nasi Wizara na Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha tunawezesha Bodi hii iweze kufanya kazi yake. Kwa sasa hivi inasimamia baadhi ya shughuli lakini pia tutaleta nadhani maboresho ya Sheria kuona sasa inasimamia maghala yote nchini ili yaweze kufanya kazi zake vizuri, lakini tumeendelea kuwawezesha kwa kuwapa fedha zaidi kila mwaka ili waweze kukamilisha majukumu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia alisema hoja ya Bodi hii ihakikishe inaweza kujenga maghala kwenye vijiji na maeneo mengi. Nia ya Serikali ni kuona sasa tutashirikisha sekta binafsi ili nao waweze kufanya kazi zao vizuri lakini pia na sisi kama Serikali tutaendelea kuwezesha ujenzi wa maghala hayo maeneo tofauti tofauti na hasa vijijini ambako ndiko kuna haja kubwa ya kuwa na maghala haya ili wananchi waweze kuhifadhi mazao yao yawe katika ubora unaotakiwa lakini pia kuweza kudhibiti kupata bei bora ya mazao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa na hoja ya Mheshimiwa Subira Mgalu kuhusu SIDO kuwezeshwa mitaji ya fedha lakini pia kuwezeshwa na vitendea kazi. Ni kweli SIDO ambayo ndio inahudumia viwanda vidogo vidogo na biashara ndogo ndogo kama Waheshimiwa Wabunge wengi walivyosema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali ni kuona sasa tunaimarisha sekta hii ya viwanda vidogo vidogo ili viweze kusaidia wananchi wengi zaidi kwenye ngazi ya chini ambako ndiko wananchi wengi wanashiriki katika kukuza uchumi wa nchi hii. Kwa hiyo, tutaendelea kuwawezesha SIDO na kuhakikisha teknolojia muhimu katika maeneo tofauti mikoani mpaka kwenye Halmashauri ili angalau zisaidie maendeleo ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa na hoja ya kuhakikisha kufanya tathmini ya vile viwanda mia moja vya kila Halmashauri ambavyo tulikuwa tunaendelea navyo. Ni kweli tutaendelea kufanya zoezi hilo la utambuzi wa viwanda vile na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vingine ili kuhakikisha kila Mkoa unapata fursa ya kuongeza thamani hasa kwenye eneo hili la mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja nyingine pia ya kuona namna gani tunaendeleza kuhakikisha tunahamasisha ujasiriamali. Kama nilivyosema SIDO ndiyo wanasaidia sana katika eneo hili lakini pia na vyuo vingine kama VETA na Taasisi zingine TCCIA na CTI ambao wapo kwenye sekta binafsi kuhakikisha tunawawezesha wajasiriamali katika elimu kwa maana ya ujuzi lakini pia teknolojia lakini na mitaji kuhakikisha nao wanashiriki vizuri katika kuendeleza sekta ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo naomba kusema tena naunga mkono hoja na ninawaomba Waheshimiwa Wabunge wote, tuunge mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri ili kuhakikisha Wizara inaweza kutimiza majukumu yake katika Mwaka, 2022/2023. Ninakushukuru sana. (Makofi)