Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Eric James Shigongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wa rafiki yangu Mheshimiwa Condester umenichukua kidogo, nikawa nimepoteza kidogo direction.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuishukuru sana Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Makamu, Katibu Mkuu na ninawashukuru pia Wajumbe wenzangu wa Kamati ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu Tanzania miaka miwili iliyopita tulisherekea tukashangilia kwa pamoja kupanda mpaka uchumi wa kati. GDP ya Taifa ilikua, per capital income ikaongezeka, na hivyo tukasherekea kwamba nchi yetu inakwenda vizuri, lakini ninavyozungumza na wewe hivi sasa, nchi yetu imerudi ilipokuwa. Pato la Taifa (per capital income) la Mtanzania imeshuka mpaka 976. Ina maana tumeporomoka chini kwa sababu yoyote ile; iwe ni sababu ya COVID au ya kitu chochote, lakini ukweli ni kwamba tumeporomoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi yetu kama Wabunge, kama Watanzania ni kuhakikisha tunafanya kazi kwa nguvu tena kurudi tulipokuwa na kwenda mbele zaidi. Hili litawezekana kwa jambo moja kubwa, Agriculture. Kilimo peke yake; kilimo cha nchi yetu ndiyo kitatupeleka tena tulipokuwa na hata kuwa na per capital income ya dola 4,000 au 5,000 tuweze kukua zaidi. Kilimo peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia Kamati ya Viwanda na Biashara leo, sizungumzii Wizara ya Kilimo. Sasa hoja yangu iko wapi? Watanzania wanalima sana, lakini kinachowasumbua ni soko la mazao yao. Watanzania siyo masikini, ila wanakosa soko la mazao yao. Hili lazima nilizungumze kwa utaratibu na nieleweke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha nchi hii kinachangia asilimia 27 ya pato la Taifa. Maana yake ni kwamba kama tukiamua kulima kwa nguvu kubwa zaidi, tutaweza kuchangia hata asimilia 50 ya pato la Taifa. Ardhi tunayo, ardhi yetu ni square kilometer 940 arable land. Inayoweza kulimika ni square kilometer 345,000 hivi, lakini nchi kama Malawi inatuzidi kwenye pato la Taifa katika kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka kuzungumza kitu kimoja, Wizara ya Viwanda na Biashara ina Kitengo kinachoshughulika na masoko, na Kitengo hiki ni TANTRADE, wapo hapa wananisikia. Nimeshawahi kukutana nao mpaka ofisini kwangu nimeongea nao, nimewaleza what to do? Tufanye nini kama Taifa ili tuweze kusaidia kilimo chetu? Mheshimiwa Bashe analima sana, lakini hauzi mazao. Kazi ya Bashe ni kulima, na kazi ya kuuza mazao ni ya dada yangu Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji. (Makofi)

Mheshimiwa Menyekiti, sasa TANTRADE hawa ninaowaongelea, nitumie neno hili; linaweza kuwa siyo zuri lakini naomba wanivumilie, wako ICU. TANTRADE wako ICU, hawana pesa za kutafuta masoko, wanawezaje kushindana na Kenya? Wanawezaje kushindana na Malawi? Hawana fedha halafu tunategemea Mheshimiwa Bashe alime, halafu atafute masoko. Watatafutaje masoko hawa? Hawana uwezo, hawana technology.

Mheshimiwa Mweneyekiti, ninachokizungumza na nieleweke, kama tumedhamiria kurudi tulipokuwa kiuchumi, pato la Taifa liongezeke, per capita income iongezeke, ni lazima kuanzia sasa tuamue kuwekeza. Hatuwezi kupeleka wanajeshi wetu vitani bila silaha. Tuna tabia ya kupeleka wapiganaji halafu hatuwapi silaha. Unategemeaje wewe Mheshimiwa Bashe unalima, halafu kesho unataka uongeze pato la Taifa, halafu hutafuti masoko?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtafuta masoko hana fedha anahangaika, kazi yake imebadilika kuwa kuandaa sabasaba kila mwaka; kazi ya TanTrade siyo kuandaa sabasaba, kazi ya TanTrade ni kutafuta masoko yenye mazao ya nchi yetu. (Makofi)

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge Eric Shigongo kwamba amesema tuliingia uchumi wa kati lakini tena tumerudi tulipokuwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumtaarifu ni kwamba, kilichotuingiza uchumi wa kati tumekiacha ndiyo maana tumerudi tulipokuwa; hii ni kwa sababu ya kukosa dira ya taifa na maono ya taifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Shigongo taarifa hiyo unaipokea?

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu, naweka sawa hiyo.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee au nikae kwanza?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri ulikuwa unasemaje.

KUHUSU UTARATIBU

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti nataka niweke kumbukumbu sawa; kwamba hatujarudi tulipokuwa; hii naomba isikike vizuri sana. Tulitoka uchumi wa chini, tukaenda uchumi wa kati wa chini, hatujawahi kurudi uchumi wa chini. Nchi yetu bado iko middle income. Tunachokiongelea ni ukuaji peke yake. Yaani hizi terminology za kiuchumi ni vizuri sana kuzisogelea kwa utaratibu. Kuta tofauti sana kati ya level of income ya nchi na growth rate.

Kwa hiyo sasa hivi ambacho kimeathiriwa na COVID pamoja na vitu vingine vyote ni growth rate tu; na yenyewe ni trend zinazobadilika kama mfumuko unavyobadilika. Kwa hiyo kilichobadilika tulishafika asilimia 7 tukashuka mpaka asilimia nne ya ukuaji wa uchumi ile ya annual growth rate.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na sasa hivi tumeshapanda kutoka hiyo asilimia nne tumeshakwenda asilimia 4.9; na takwimu hizi zinapokamilika za 2021 likely ukichukua quoters ambazo zimekwishajumlishwa, ukijumlisha wastani unakwenda kwenye 5; na 2022 wastani unaotarajiwa ni 5.2…

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Utaratibu.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: …kwa maana hiyo; hata wenzetu wa Benki ya Dunia juzi walisema huenda tukaenda 5.5. Na kwa sasa hivi ambavyo tunategemea kuwekeza pakubwa kwenye bajeti inayokuja kwenye sekta za uzalishaji tunategemea tutakwenda kwenye hiyo saba. Kwa hiyo, hatuongelei level of income tunaongelea growth rate.

MWENYEKITI: Umeeleweka ahsante Mheshimiwa Waziri; Mheshimiwa Shigongo karibu umalizie.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee; na kama siendelei naomba muda wangu uhifadhi kwenye friji.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Shigongo naomba usubiri kuhusu utaratibu. Msiwe mnahata nafasi mimi naangalia sauti yako huku kumbe upo huku. Mheshimiwa kuhusu utaratibu?

KUHUSU UTARATIBU

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu ulikuwa unakwenda kwa Mheshimiwa Mwigulu Nchemba. Ulikuwa unatafakari sauti kabla hujaniona; lakini nimesimama kuhusu utaratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa ni kawaida ambayo inakwenda kinyume na Kanuni zetu. Kwanza tunatakiwa tunapotoa taarifa isizidi dakika mbili; lakini Mheshimiwa Mwigulu Nchemba akisimama anahutubia zaidi ya dakika mbili, kinyume kabisa na taratibu; na hii imeshawahi kutolewa angalizo na Mheshimiwa Spika hapa baada ya kuombewa mwongozo. Tunaomba tu-observe Kanuni zetu, kama Waziri umeshindwa kuvumilia uje kujibu mwishoni basi ukisimama ujihakikishe unaji-confine ndani ya dakika mbili unatoa ule taarifa yako watu wanaendelea siyo unaanza kuhutubia kabla ya muda wenyewe husika.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Easter tumepokea kuhusu huo utaratibu na naamini wenyewe wamesikia na kwa vile imeshatolewa mwongozo basi tunaomba wajirekebishe. Mheshimiwa Shigongo naomba uridhie.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu mimi kama mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi, mwaminifu, Mbunge wa Chama cha Mapinduzi siyo vizuri sana kupisha na Waziri wangu wa Fedha. Lakini document hapa inanionesha hivi; qualification of a country to become middle income is per capital income of USD133,000 to USD 445,000; yaani qualification ya nchi yoyote kuwa uchumi wa kati ni pato lake la mtu mmoja per capital kufikia dola 1036 sisi tulifikia Dola 1080; tuka-qualify kuwa uchumi wa Kati. Lakini hivi sasa record zilizopo hapa zinaonesha uchumi wetu sisi sasa hivi pato la mtu mmoja per capital imefikia 976. Ndiyo maana nasema tumerudi kwa sababu per capital income imeshuka.

Mheshimia Mwenyekiti, nchi hii imepiga hatua kubwa sana, kazi kubwa sana imefanyika; tulikotoka na hapa tulipo ni pazuri sana; lakini hoja yangu ilikuwa ni kwamba kurudi nyuma kwetu hapa sisi siyo sababu, kazi yetu ni kuwaomba Wabunge na watanzania tufanye kazi kwa juhudi kubwa turudi tulipokuwa. Sasa itawezekanaje hili; hili linawezekana kwa kilimo; na kilimo tuanzie sokoni, kwanza tutafute soko ndipo tuje tuwaambie wakulima walime nini, na hiyo kazi ni Tantrade. Kwahiyo Tamtrade TanTrade wawezeshwe, wapate fedha, watafute masoko halafu wakulima waambiwe walime nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wangu wa Buchosa wwaliambiwa walime maparachichi, lakini hivi sasa yanawaozea. Sasa watu wanalima miwa inawaozea, TanTrade wapewe fedha, TanTrade wapo ICU, tuwatoe ICU kwa kuwapa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuhakikishia, na kumbukumbu zikae sawasawa; kama tukiwa-impower watafuta masoko wetu; na wananchi wetu wakalima uchumi wanchi hii utakua, pato la taifa litaongezeka na watanzania watakuwa na fedha. Kwa hayo, ninayosema nakuona unagusa kengele bila shaka unataka kunisimamisha; ahsante naomba kuunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)