Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi; na napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa maandalizi ya Bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sitazungumza mambo mengi, mimi najielekeza kwenye jambo moja tu, ambalo linagusa viwanda pamoja na biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema Mheshimiwa Neema na mimi kwa miaka kadhaa sasa nimekuwa nikishauri kuhusiana na suala la sukari; na wakati wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu nilisema kuhusiana na mafuta ya kula; na juzi Mheshimiwa Injinia Ezra amesema, Mheshimiwa Kingu na Wabunge wengine wamesema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama taifa lazima tufike mahali kuna mambo tuyakatae, na kama Bunge lazima mahali tufike kuna mambo tuyakatae. Sasa tunayakataa mambo gani? Na tunayakataaje? Kati ya mambo ambayo tunatakiwa tuyakatae moja wapo ni hili la kuagiza bidhaa kutoka nje ambazo tunaweza kama taifa kuzalisha hapa hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani tukawa tunaagiza mafuta ya kula, tunaagiza ngano, tunaagiza sukari. Mjumbe mmoja alisema hapa. Kwa mfano tunategemea mafuta ya kula kutoka Malaysia kwa asilimia kubwa, what if siku ikitokezea soko kubwa liko Marekani wakaelekeza mafuta yao yote kwenda Marekani, na sisi tutafanya nini kama taifa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, yako mambo lazima kama taifa tuyakatae, kwa sababu haiwezekani kama Taifa sisi ni kuagiza tu, ni kuagiza tu, ni kuagiza tu vitu ambavyo tunaweza kuzalisha hapa nchini. Hii mifumuko ya bei, ugumu wa maisha tunaosema ni kwa sababu pia takriban kila kitu tunaagiza. Yaani ukiangalia sisi kama taifa kitu ambacho ambacho hatuagizi ni hewa tu ya Mwenyezi Mungu ambayo ametugaia lakini a lot of things sisi ni kuagiza! ni kuagiza! ni kuagiza!. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninashauri jambo hili tulikatae kama taifa. Tutakataaje? Mwaka 2019 tarehe 15 mimi baada ya kuchangia, pamoja na mchango wangu wa maandishi niliandika barua kwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Waziri wa Kilimo, Waziri wa TAMISEMI na Waziri wa Fedha. Niliandika barua kuwaambia namna ambavyo kama taifa tunaweza tukaondokana na shida ya kuagiza sukari kila mwaka. sasa kwa nini niliandika barua hiyo kwa Mawaziri hawa? Ni kwa sababu sukari ni biashara lakini ni viwanda; lakini kabla hujapata sukari lazima mtu wa kilimo awe amehusika katika kulima miwa.

Pia ili aweze kulima miwa lazima Waziri wa Fedha kwa namna moja ahusike katika masaula mazima ya financing. Yuko Waziri mmoja sitamtaja alinijibu na haikuwa lazima ile barua wanijibu, hapana, ulikuwa ni ushauri tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama taifa, wenzetu Brazili na India wamefanikiwaje katika sukari? Wametumia small scale industries. Kwamba unakuwa na maeneo ambayo yako suitable kulima miwa, lakini pia gharama zake si kubwa katika kuwekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nashauri tuwekeze kwenye small and medium scale sugar plantations? Kwanza kiwanda hakihitaji eneo kubwa, kina hitaji kama heka tano tu, na pia unahitaji kama heka 3,000 za kuzalisha miwa. Lakini pia ukishazalisha miwa hiyo heka 3,000 ambayo niliwaandikia watu wa Kilimo na TAMISEMI; unaweza kushirikiana na Halmashauri za maeneo husika zenyewe zikatoa ardhi, Wizara ya Fedha wana-finance kupitia hata Benki ya Kilimo na uwekezaji wake hauzidi dola kati ya milioni 3.5 hadi milioni 5. Maana yake hapo unazungumzia bilioni nane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia hata ukiwa na wale wakulima wa nje (out growers) inakuwa ni rahisi kuwapa extension services. Lakini pia ukijenga viwanda hivi vidogo vidogo hata gharama za usafirishaji wa miwa kutoka shamba kwenda kwenye hiyo factory hauwi mkubwa kama ilivyo sasa. Tunazungumza mradi wa Mkulazi, huu nadhani ni mwaka wa sita. Mradi wa Dola milioni 150 lakini sisi hapa tukiwa na Dola milioni 100 kwa miaka miwili hatutaagiza sukari nje na tutauza sukari nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yapo. Kuna Manyara, Mfilisi, Kibelege Ifakara, Luembe, Wami, Kasulu na Lufiji. Kwa sababu nchi yetu imejaliwa hali tofauti tofauti. Kwa hiyo, mimi nashauri sana Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ikae kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona Mheshimiwa Rais ameunda kikosi kazi chini ya Profesa Mkandala kwa ajili ya kuzungumza na kujadili namna gani mustakabali wa kuendesha siasa zetu katika hali iliyo njema na bora. Mheshimiwa Waziri…

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Napenda kumpa mchangiaji kaka yangu Mheshimiwa Cosato Chumi kwamba mikakati ya kuwekeza katika viwanda vya TCD ndogo vyenye uwezo wa kuzalisha kuanzia tani 100 na kuendelea aliyekuwa Mkurugenzi wa NSSF wakati huo ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara hii ya Uwekezaji na Viwanda alishakuja na mipango mikakati kwa ajili ya kujenga viwanda vidogo lakini mipango hiyo masikini ya Mungu sijui imepotelea wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kwa taarifa hii anachokisema Mheshimiwa Cosato Chumi tunauwezo wa kujenga viwanda vya TCD ndogo ndogo tukaeupukana na uagizaji wa sukari na kuliokoa Taifa letu katika kutumia fedha za kigeni kwa ajili ya uagizaji wa sukari. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Cosato Chumi, unaipokea hiyo taarifa?

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa na Mheshimiwa Kingu ninaamini ni miongoni mwa walionielewa ninacho kimaanisha. Naamini ataungana na mimi ninaposema kama taifa kuna mambo tukatae. Kwa muundo huo wa kuwa na viwanda vidogo vidogo ambavyo tunaweza kushirikisha, kama nilivyosema, Halmashauri zikatoa ardhi, Benki ya Kilimo ikatoa mitaji, Wizara ya Kilimo ikasaidia katika namna ya kuhakikisha kwamba tunakuza hiyo miwa. Mimi ndugu zangu nimekaa Kilombero, miwa ukipanda ni miezi 12 unaanza kuvuna na baada ya hapo kila baada ya miezi sita utavuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaposema tukatae ndiyo mambo kama haya kwamba anasema hapa Mheshimiwa Kingu. Bahati nzuri Profesa mko nae huko sasa aliyekuwa NSSF ndiye Katibu Mkuu; na ndiyo maana nasema Mheshimiwa Waziri pamoja na ile timu yako unaweza ukawa na kitu kinaitwa kitchen cabinet...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia muda wangu kidogo. Kitchen cabinet ni nini?

MWENYEKITI: Malizia kidogo.

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na timu yako unaweza ukawa na timu ya wataalam kutoka SUA. Kama tumeunda kikosi kazi kwa ajili ya mambo ya siasa, kwa nini tusiunde kikosi kazi kwa ajili ya mambo ya uchumi? Ili tukatae mambo ya kuagiza, ukachukua wataalam kutoka SUA, ukachukua wataalam kutoka UDSM pale, kutoka Mzumbe, kutoka hapa Chuo cha Mipango wakasaidia nao kama kitchen cabinet. Simaanishi kwamba wataalam ulionao hawana uwezo, hapana, ili wakushauri ipasavyo ili kusudi dhana ya kwamba tukatae, tukatae, tukatae baadhi ya mambo iweze kuthibitika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nakushukuru. Nilisema siku moja, katika baadhi ya maeneo along the high way naomba Serikai itusaidie. Watu kama wa Mafinga, Mikumi, Makambako, Mombo – Korogwe na kwingineko turuhusiwe kufanya biashara masaa 24. Tujiongezee kipato na Halmshauri zipate kipato, kwa sababu sheria as it is now mwisho kufanya biashara ni saa nne. Lakini hata dunia zingine watu wanafanya shughuli saa 24.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono na Mungu atubariki. Mungu abairiki taifa letu. (Makofi)