Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, ahsante nami naomba kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Magereza ya mwaka 2002, Kifungu cha 58 kinaonesha bayana kwamba Magereza yanatakiwa kuwa na miundombinu wezeshi kwa maana ya mifumo ya maji safi, majitaka, malazi na kwingineko. Ripoti ya CAG ambayo imetoka imeainisha mapungufu makubwa sana ya kiufanisi kwenye mlundikano wa mahabusu na wafungwa uhaba wa nyumba za Magereza, uhaba wa Magereza yenyewe lakini pia uhaba wa usafiri na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda nitaenda kwa haraka sana kwa kuanza na mlundikano wa wafungwa na mahabusu. Mwenzangu aliyepita ameainisha hapa, hata ripoti ya CAG imeainisha na hata nikitolea mfano kutoka kule kwetu Tarime, Gereza limejengwa enzi za mkoloni 1942 lenye uwezo wa kubeba watu 209 tu lakini sasa hivi ukienda unakuta saa nyingine wafungwa na mahabusu kati ya 460 mpaka 670 na hii ni hatari zaidi mara tatu zaidi ya uwezo uliopo. Kwa hiyo, ilikuwa dhahiri kabisa Serikali kutambua kwamba population ya sasa hivi ofcourse imeongezeka na population ikiongezeka hata rate of crimes zinaongezeka na watambue tu ni upeo wa kawaida, kwa hiyo hata haya majengo yaliyojengwa kipindi hicho yanatakiwa aidha yaboreshwe na yaongezwe yawe expanded kuweza ku-accommodate kiwango cha watu kilichopo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ripoti inaainisha kabisa kwamba Jeshi la Magereza lilikuwa na mpango mkakati ambao uliainisha kujenga Magereza kumi kwa miaka mitano, lakini haikuweza kufanya hicho badala yake ikajenga Magereza mawili ambayo hata hawakufanya needs assessment, hawakufanya uhakiki wa mahitaji wakaenda kujenga Ruangwa na Chato ambapo kiwango cha uhalifu kipo chini sana, wakaacha huku kwingine na wameainisha kabisa huo kwamba ni ubadhirifu na walikuwa hata hawana mpango katika bajeti yao ya mwaka kipindi wanajenga hayo Magereza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia huku kwingine mlundikano ni mkubwa sana wameainisha Keko na kwingineko ambapo tukiacha hivi tunasababisha magonjwa na kadhalika. Sasa mimi ningeshauri tu tuwe tunafanya needs assessment, uhakiki wa wahitaji wa haya Magereza unaenda kujenga wapi. Kwa mfano, Gereza la Tarime limejengwa zamani nimesema linavuja lingeweza kukarabatiwa na kuweza kujengwa kisasa zaidi kuweza kuwapokea hawa watu.

Mheshimiwa Spika, pia ukiangalia unakuta Rorya wanajenga Mahakama watu wa Rorya wanakuja kuhifadhiwa pale Gereza la Tarime, haya Magereza hayana usafiri kama nilivyosema mwanzo sasa mkishamaliza kujenga ile Mahakama Wilaya ya Rorya hawa watu watakuwa wanatoka vipi Tarime kwenda Rorya wakati hamna usafiri wa magari kwenye Magereza! Tangia walivyotoa mwaka 2008 walipewa misaada tena ni Arusha, Dodoma, Dar es Salaam sijui na Pwani magari mawili tu. Serikali mpaka leo hamjawahi kununua magari ya Magereza kuweza kupeleka mahabusu Mahakamani, hii inapelekea mlundikano wa wafungwa na mahabusu kuendelea kuwepo. Mahabusu wasipoenda gerezani ina maana kesi inazidi kupelekwa mbele mlundikano unaendelea kuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama tunaweza tukanunua magari ya fire magari ya washawasha, ambayo ni zaidi ya Milioni 500, Milioni 600 huko, ina maana gari moja tu lingeweza kutumika kununua hata zaidi ya magari matano mpaka sita kwenye Magereza. Kama tunaweza kununua haya magari ambayo yanatumika mara moja baada ya miaka mitano hayana faida yoyote wala tija wakati wa uchaguzi tu ndiyo yanatumika kuzuia ghasia, kwa nini tusiweze kununua magari ya magereza kuweza kusafirisha hawa watanzania ambao wanasubiriwa kusikilizwa kesi zao waweze kwenda mahakamani na kuepusha mlundikano wa mahabusu kwenye magereza yetu. Kama tumeshindwa tuangalie possibility zingine haya magari yamekaa tu, mwaka ule Bunge lililopita Mheshimiwa Masauni akiwa Naibu Waziri anasema wanaangalia kuyafanya yawe magari ya zimamoto. Sasa baada ya kuzima moto yapigeni tu mnada kama inawezekana mnunue magari mengine ya Jeshi la Magereza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu uhaba wa nyumba za wafanyakazi. CAG ameainisha kabisa kwamba kwenye mpango mkakati wenu mnaonyesha kwamba mtajenga nyumba takriban 14,000 na kukarabati nyumba 2,000 lakini hamkuweza kufanya hivyo na uhitaji huo wa nyumba za wafanyakazi ni zaidi ya 14,747, hii ni kinyume na Prisons Standing Order ya mwaka 2003 na wameainisha Gereza la Segerea mathalani zaidi ya wafanyakazi asilimia 65 wanakaa nje ya Magereza kinyume kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Gereza la Wazo wamesema zaidi ya asilimia 72 wanakaa nje ya Magereza, sasa mipango yetu ni ipi? Tunapanga, tunaainisha lakini hatutekelezi! Yaani mpango mkakati wenyewe unakuwa kama uko tu yaani hautekelezeki, kama picha tu inakuja kwenye daftari ukipekua kitabu unafurahia lakini hamna utekelezaji wowote ule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine imeainishwa pia uhaba wa usafiri na hii naendelea ku-sement tukishindwa kuwa na usafiri kupeleka watu kwenye Mahakama basi tujenge hata mifumo ya kisasa kesi ziweze kusikilizwa kutoka kule wakiwa magerezani maana yake mahakamani tumeona wenyewe wanakuja na mifumo ya kisasa na kuna nchi zingine kama Zambia mahabusu wanasikilizwa kesi zao wakiwa kule, kama tumeshindwa kununua magari kwa gharama za magari, kama tumeshindwa kujenga magereza, kupunguza mlundikano wa mahabusu, tuweke mifumo ya kisasa iweze kutumika.

Mheshimiwa Spika, kingine ni uhaba wa miundombinu na mifumo ya kiusalama. Ripoti imeainisha kabisa kwamba katika Magereza yote yaliyotembelewa 15 ni Magereza mawili tu yalikuwa na CCTV camera. Gereza hazina scanner, hazina metal ditactor, hazina hata satellite.

Mheshimiwa Spika, nilishaisema hata mwaka jana nikapiga kelele, wengine sisi ni wahanga tumeshaenda huko, ukifika unavuliwa nguo zote unabaki kama ulivyozaliwa na Mama yako unaambiwa uruke kichura chura ili waone kama una object kwenye mwili wako ni udhalilishaji na unatweza utu wa binadamu! Kwanini msilichukue hili mlifanyie kazi muweze kuhakikisha kwamba mnaweka hivi vitu? (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana.