Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Juma Othman Hija

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tumbatu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami nichukue fursa hii kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ili nitoe mchango wangu katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, lakini pili nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake Waziri kwa namna walivyowasilisha hotuba hii kwa umakini mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara hii ni Wizara muhimu sana inayolinda amani yetu katika nchi yetu. Katika kuchangia hotuba hii mimi nitachangia masuala mawili tu ambayo yamo katika jimbo langu. Jambo la kwanza ni kuhusu ujenzi wa Kituo cha Polisi katika Kisiwa kidogo cha Tumbatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimekuwa kila ninapopata nafasi ya kusimama kuchangia katika Bunge lako Tukufu nimekuwa nikilizungumza suala hili la kujenga Kituo cha Polisi katika Kisiwa cha Tumbatu. Mara ya mwisho nilipokuwa nalizungumzia suala hili kupitia swali langu namba 36, Mheshimiwa Waziri alinijibu kwamba, Serikali itachukua hatua ya kufanya tathmini ya kitaalamu ili kuona namna ya kujenga Kituo cha Polisi katika Kisiwa cha Tumbatu. Mpaka leo sijajua nini kinaendelea? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini lingine ni kwamba, alinitaka nioneshe initiative ya kujenga Kituo cha Polisi pale kwetu Tumbatu. Mimi nili-provide kiwanja kwa ajili ya kisiwa kile lakini mpaka leo hii kiwanja kile kipo, hakuna kinachoendelea. Kwa hivyo, namuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kusimama hapa atueleze nini kinaendelea kuhusiana na ujenzi wa Kituo cha Polisi katika Kisiwa cha Tumbatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo langu la pili ni kuhusu Kituo cha Polisi cha Mkokotoni. Mara ya mwisho nilivyokuwa nazungumza kuhusu jengo la Mkokotoni nilieleza masikitiko yangu makubwa kuhusu hali ilivyo pale Mkokotoni. Askari wa pale walikuwa wanaishi katika mazingira magumu, mabovu, walikuwa wanafanya kazi inaponyesha mvua wana-shift kutoka walipo wanafanya kazi katika chumba kidogo cha mahabusu.

Mheshimiwa Spika, lakini leo nasimama hapa kutoa shukrani zangu za dhati kwa Serikali yetu kwa kutujengea kituo chetu kikuu kile. Tunashukuru sana kwa kutujengea kituo kile. Tumeshapata kituo kizuri cha kisasa kabisa. Ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri na kwa Wizara ni kukiboresha kituo kile, kukiboresha kwa maana ya kwamba, kukijengea thamani na kukijengea uzio. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, juzi nilipokwenda kukiangalia kile Kituo cha Polisi cha Mkokotoni waliniambia kwamba, wameshaanza kujenga uzio lakini wamesita kutokana na upungufu wa fedha. Kwa hiyo, naomba Wizara itupatie fedha, iwapatie fedha ili wamalize ule ukuta pale Mkokotoni. Aidha, makazi ya maaskari ya pale Mkokotoni ni mabovu sana. Kuna nyumba pale zimejengwa kabla ya uhuru, yaani kabla ya mapinduzi; nyumba ni chakavu, hazistahiki kabisa kuishi maaskari wetu. Kwa hivyo, naomba Wizara ichukue juhudi za makusudi kuwajengea makazi askari wa pale Mkokotoni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hayo yangu mawili ambayo yanahusu jimbo langu naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)