Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Esther Edwin Maleko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua nafasi hii kuipongeza sana Wizara hususan Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Naibu wake pamoja na Watendaji wote kwa kazi nzuri wanayoifanya. Moja kwa moja niende kwenye hoja yangu kutokana na muda huu mchache.

Mheshimiwa Spika, napongeza sana Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri wanayoifanya, lakini pamoja na kupongeza jeshi hili kwa kazi nzuri wanayofanya tunajua kazi kubwa ya Jeshi la Polisi ni kulinda rai na mali zake. Sasa, cha kushangaza hawahawa Polisi ambao tunategemea ndio watakaotulinda sisi na mali zetu sisi hatujui wao wanaishije. Nyumba zao ni mbaya na hazifanani na kazi kubwa wanayoifanya, lakini pia mishahara yao na posho zao haziendani na kazi wanazozifanya nah uku tukitaka wafanye kazi hii kwa weledi mkubwa. (Makofi)

MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Esther Malleko, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jerry Slaa.

T A A R I F A

MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya watoto wa line tulioko humu ndani napenda kumpa taarifa mzungumzaji kuwa hali ya makazi ya Polisi kusema kweli ni mbaya. Tangu zile za pale Ukonga, zile Police Hunger Officers Line, ile namba tano niliyozaliwa mimi, zile za File and Rank na zile za FFU hali ni mbaya. Naomba kumpa taarifa mzungumzaji. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Esther Malleko, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa hiyo kwa sababu ni kweli kwamba askari wetu wanafanya kazi kubwa sana lakini mazingira wanayoishi hayakidhi mahitaji wala viwango vya kuishi mwanadamu. Ukiangalia nyumba wanazoishi kuna nyingine ni za bati, haifai wala haipendezi; huku tukiwataka hawa askari tunataka wakatulinde. Wanaendaje kutulinda sisi ilhali wao wameacha familia zao zikiwa katika mazingira duni? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaomba sana Wizara hii katika bajeti hii iangalie namna ya kuboresha nyumba za askari wetu, kuboresha maslahi yao pamoja na kuboresha zaidi vitendea. Askari hawa wanaenda kufanya kazi ya kulinda kwenye doria usiku, lakini magari yote ni mabovu. Sasa, wataendaje kufanya kazi hii kubwa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini si hivyo tu, tumesikia hata wenzangu hapa wakichangia, hata mafuta wanaenda kuomba kwa wadau. Haipendezi, tunatakiwa tuangalie ni namna gani ya kuwezesha jeshi hili la Polisi ili liweze kufanya kazi yake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna changamoto nyingine kubwa sana. Jeshi la Polisi linafanya kazi nzuri, lakini leo kumeibuka wimbi kubwa la matapeli wanaojifanya ni maafisa wa Serikali. Ninaomba sana Jeshi la Polisi liweze kusaidiwa; kama ni sheria haijakaa vizuri iletwe hapa tuirekebishe, lakini kama kuna namna yoyote ile sisi kama Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao tuliwahi kupitisha hiyo sheria na sasa imepitwa na wakati tuifanyie kazi tena. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna jambo lingine pia ambalo linawatesa sana wananchi. Jambo hili ni kuhusu matapeli wa mitandaoni. Leo tumeambiwa kwa kupitia vitambulisho vya NIDA watasajili namba za simu na tatizo hili litakwisha, lakini kila kunapokucha tatizo hili linazidi kuongezeka, kila kuchapo tunatumiwa ujumbe kuna babu, kuna bibi anatoa dawa ya mapenzi, sijui ya nini, kila siku. Sasa, mimi ninauliza, hivi TCRA, Jeshi la Polisi pamoja na kampuni za simu ambazo zinawapa wakala wao kwenda kusajili hizi line za simu wanashindwa kudhibiti jambo hili? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)