Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hoja ya Dharura (Changamoto ya Kupanda kwa bei za Mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa)

Hon. January Yusuf Makamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bumbuli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hoja ya Dharura (Changamoto ya Kupanda kwa bei za Mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa)

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa hii ya kuchangia hoja hii na moja kwa moja nianze kusema kwamba naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Kigua. Ni hoja iliyokuja kwa wakati sahihi kwa jambo sahihi na kwa namna sahihi. Pia nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia na kutoa maoni katika hoja hii. Maoni, ushauri,
mapendekezo mazuri kabisa, nasi kama Serikali tunayachukua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mambo kadhaa katika jambo hili. Ni dhahiri kwamba, wote tunajua bei zimepanda duniani. Nasi kama nchi sio wazalishaji wa mafuta, tunanunua mafuta kutoka nje na sehemu kubwa ya bei ya mafuta inayopangwa hapa Tanzania inatokana na vitu viwili. Kwanza, gharama ya mafuta yenyewe kwenye Soko la Dunia; pili, gharama ya kuyaleta mafuta hapa Tanzania; tatu, kodi na tozo mbalimbali za hapa nchini; na mwisho kabisa, gharama za kufanya biashara yenyewe hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, sasa kuna mambo katika hayo hatuna mkono nayo. La kwanza ni bei ya mafuta duniani; la pili, ni gharama za kuyaleta mafuta duniani na la tatu ni gharama ya ufanyaji wa biashara yenyewe ya mafuta. Sasa tunaweza kusema maana vita ya Ukraine imekuwa ndiyo sababu ya rahisi zaidi. Siku hizi wanasema, mtu hata ukichelewa kurudi nyumbani unasema vita ya Ukraine. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii vita imesababishaje? Kwa sababu ni lazima kulieleza. Ukilieleza hivi juu juu tu, hata wananchi wanasema kila kitu sasa mnasema vita. Asilimia 12 ya mafuta yote duniani yalikuwa yanazalishwa na nchi ya Urusi. Ni nchi ya pili kwa uzalishaji wa mafuta; ya kwanza ni Marekani; ya pili ni Urusi na Saudi Arabia wanakaribiana. Asilimia 12 ya mafuta yaliyokuwa yanazalishwa Urusi yalikuwa yanauzwa pale eneo la Ulaya. Baada ya vita sasa, kwanza uzalishaji ukapungua; pili, mauzo ya mafuta Ulaya na yenyewe yakasimama, kwa sababu zile nchi zilipunguza kununua mafuta na sasa hivi zinataka kugomea kabisa.

Mheshimiwa Spika, mfumo wa usafirishaji wa mafuta yale katika nchi za eneo lile ulikuwa ni karibu. Sasa hivi ambapo yale mafuta yanatafuta soko alternative, mfumo mzima wa usafirishaji wa mafuta duniani maana yake ni kwamba meli hizi zinaenda umbali zaidi, insurance inakuwa kubwa zaidi nagharama inakuwa kubwa zaidi. Kwa hiyo, siyo suala la bei tu, hata suala la usafirishaji wa mafuta limekuwa kubwa sana na ndiyo maana premiums, maana gharama ya kuleta mafuta imepanda sana kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Spika, ukitazama hizi bei za mwezi wa Tano ambazo zimepanda kwa kiasi kikubwa ambazo ndiyo zimesababisha hoja hii, maana yake ni kwamba zimetokana na bei iliyokuwepo ya mafuta duniani miezi miwili iliyopita. Mfumo wetu sisi ni kwamba bei ya mafuta tunayoingiza ambayo yamesafishwa ya kwenye pump hapa nchini, bei zake zinashabihiana na bei za dunia za miezi miwili iliyopita.

Mheshimiwa Spika, mtu akiangalia kwenye internet leo akaona bei zimeshuka, akasema ninyi hamshushi, inakuwa ni makosa, lazima utazame bei za miezi miwili iliyopita ndiyo ujue bei ya pump leo. Ukitazama historia ya bei ya mafuta duniani kwa miaka 15 iliyopita, bei ya juu iliyowahi kufikiwa miaka 14 iliyopita ilikuwa ni Shilingi 137/= kwa pipa. Sasa hivi bei ya mwezi Machi ilikuwa ni kubwa kuliko bei ya miaka 14 iliyopita. Ndiyo maana bei za mwezi wa Tano zimepanda kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kuna mengi ya kueleza kuhusu kupanda kwa bei. Sasa nini tunafanya, kwa sababu muda ni mfupi?

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais, alitoa maelekezo na Mheshimiwa Waziri Mkuu jana tumekaa kikao kirefu kutazama hatua za haraka kama ambavyo Wabunge wanataka tufanye, kama ambavyo wanawasilisha sauti za wananchi wanaowawakilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna hatua ambayo imezungumzwa kwa kirefu nayo ni ya kikodi na tozo. Sasa hizo hatua zinataka mashauriano, zinataka uzingatiaji wa sheria na kanuni zinazoongoza uwekaji na uondoaji wa hizo kodi na tozo. Sasa bahati nzuri mamlaka yapo kwenye Serikali, lakini pia mamlaka yanayohusu masuala ya kifedha pia yapo hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sisi kama Serikali na kama alivyogusia Mheshimiwa Simbachawene, tunasema kwamba suala hili tumelichukua. Tunafahamu udharura na uharaka wake, na vilevile tunataka uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu za nchi zinazohusiana na masuala ya kodi. Hivi karibuni tumekubaliana kwamba tutakuja na majawabu kuhusu suala hili, hasa kwenye masuala haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kama alivyozungumza Mheshimiwa Waziri Mkuu jana, suala lingine ni kutafuta namna mbadala ya kupata watu watakaotuletea mafuta kwa bei nafuu. Suala hilo limetokana na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge hapa Bungeni, nasi tukatoa kauli kukaribisha watu. Tumepokea maombi mengi, tumeyachakata na tuna imani kabisa kwamba katika wale ambao watapita vigezo ambavyo vitazingatia kanuni na taratibu na sheria za Serikali, tutaingia nao kwenye mazungumzo kwa namna ya uwazi, ili tuone kama tunaweza kupata nafuu katika uagizaji huo wa mafuta.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema wakati ule, sisi hatung’ang’anii mfumo hata kama hautupi bei nzuri. Kama Serikali tupo tayari kwa njia yoyote kwa namna yoyote kutumia mfumo wowote ambao utatuhakikishia bei nafuu na hilo ndilo ambalo tumelifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na malalamiko kuhusu mfumo uliokuwepo. Malalamiko haya yamekuwepo muda mrefu, lakini pia biashara ya mafuta ni biashara ambayo ina vita ya wenyewe kwa wenyewe. Kuna madaraja matatu; kuna wenye vituo, kuna wa katikati wale MCS na kuna wale suppliers. Huu mfumo umekuwa ni sehemu ya ugomvi; na wakati mwingine udhaifu wa mfumo pamoja na kwamba upo wakati mwingine unakuzwa ili mfumo huu aidha uchanganywe na vitu vingine au uondolewe kabisa ili turudi kule katika mfumo ambao ulikuwa hautuhakikishii supply. Falsafa yetu ni kwamba chochote kinachotuhakikishia bei nafuu kuleta mafuta tutakifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa pamoja na kwamba tunachukua hizi hatua za kikodi haraka zaidi lakini kuna hatua za muda wa kati ambazo pia tumeanza kuzichukua. Mojawapo ni kuanzisha hifadhi ya kimkakati ya Taifa ya mafuta (Strategic Petroleum Reserve). Iliahidiwa muda mrefu na mimi nimeelekeza na ndani ya wiki mbili tutasaini kanuni mpya kwa sababu lazima ianzishwe kwa kanuni inayotokana na Sheria ya Mafuta ya Petrol ndani ya wiki mbili tutaanzisha kanuni mpya za kuanzisha hifadhi ya kimkakati ya mafuta hapa nchini, na tutaelezea kwa kirefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini hatua nyingine ni kuanzisha mfuko wa kuhimili bei za mafuta kama alivyozungumza Mheshimiwa Shangazi, inaitwa Fuel Price Stabilization Fund. Wizara ipo katika hatua za mwisho za kuandika andiko la Baraza la Mawaziri na tutapeleka katika kikao kijacho cha Baraza la Mawaziri ili mfuko huo uanze na uweze kutumika katika nyakati kama hizi kwa siku zijazo; na utaratibu wake tutauelezea kwamba mfuko huu unapataje pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nyingine ni ile ndoto yetu ya muda mrefu ya kuanzisha kituo kikubwa cha biashara ya mafuta hapa nchini. Pia tuko katika hatua za mwisho, kwa sababu hii ina ushirikiano na sekta binafsi, wa kuigeuza TIPPER kuipanua, kuikarabati, kui-modernize na kuijengea uwezo wa kuhifadhi mafuta mengi zaidi na ili pale sasa pawe kituo kikubwa cha biashara ya mafuta katika ukanda huu.

Mheshimiwa Spika, ndani ya mwezi huu wa tano kabla haujaisha tutasaini makubaliano na sekta binafsi ya kuanzisha kituo hicho kitakachotuwezesha kuhifadhi mafuta yatakayotosheleza mahitaji ya hapa nchini kwa kipindi kirefu.

Mheshimiwa Spika, lingine ni kwamba, rasmi kama Waziri mwenye dhamana nimeongea na Mawaziri wenzangu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki pamoja pia na nchi za Zambia na Malawi kuomba tuitishe mkutano wa dharura ndani ya mwezi huu wa tano kule Arusha ili kwa pamoja tujadiliane kama tunaweza kuunganisha nguvu na kujenga soko moja la ukanda huu ili tuwe na mkono mkubwa zaidi wa kuweza kuamua namna ambavyo tunaweza tuka-dictate bei vilevile. Tumeshakubaliana kikao hicho kitafanyika Arusha. Bado tunazungumza kuhusu tarehe kwa sababu yapo ya kubadilishana uzoefu.

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile ni ile point aliyoongea Mheshimiwa Manyanya kwamba mafuta hapa duniani yapo ya kutosha chini ya ardhi yanayoweza kutolewa kwa ratiba stahiki na bei ikashuka, lakini kuna mambo ya kijiopolitiki, mambo ya kisiasa duniani ambayo yanasababisha baadhi ya mafuta yawe locked out kwenye soko la dunia. Lakini mkiunganisha nguvu kama nchi kama za kwetu mnaweza mka-lobby na mkafanya jitihada ili mafuta ya namna ile yaingie kwenye soko la dunia na bei iweze kushuka. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Haya Mheshimiwa Waziri malizia dakika moja.

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, la mwisho tumekuwa tunafanya jitihada; nimeongea na Waziri wa Algeria, Waziri wa Nishati wa Zabeijan, Waziri wa Nishati wa Oman kuona kama tunaweza kwa nchi kupata unafuu. Na katika mazungumzo yote jambo moja limekuja kwamba Mheshimiwa Waziri tunaweza tukawapa petrol diesel hatuna. Kwa sababu hapa imezungumziwa habari ya diesel, tofauti ya diesel. ukitazama mwenendo wa bei katika mwaka mzima uliopita landed cost ya mafuta bei iliyofika pale Dar es Salaam, ukiangalia jirani zetu Wakenya mwezi Machi tofauti kati ya gharama za diesel ilipofika Kenya na petrol ilipofika Kenya kuna tofauti ya shilingi karibu 600 kwa Kenya.

Mheshimiwa Spika, hapa kwetu landed cost ya diesel na petrol ilikuwa ni 1,960 kwa petrol, 2,150 kwa diesel. Kwa mara ya kwanza unaona divergence (kupanuka) kwa tofauti kati ya diesel na petrol. Leo hii kituo kikubwa (price point) ya diesel duniani ni Bandari ya New York. Kwa mara ya kwanza diesel iko chini kwa record ya miaka 32 iliyopita na nchi yetu hii siyo mara ya kwanza ambapo diesel iko juu kuliko petrol. Yote inahusiana na mfumo wa usafirishaji wa diesel na petrol na refining capacity na demand ya diesel na petrol.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kusitokee maneno hapa kwamba petrol iko hivi kwa hiyo kuna kitu, hili ni jambo la kawaida katika biashara hiyo. Napenda nihakikishie Bunge lako kwamba Serikali ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inawajali wananchi, inajua kilio chao inaungana na Wabunge katika kuhakikisha kwamba kilio hicho cha kupunguza gharama tunakichukua na tunakifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimalize kwa kuunga mkono hoja tena. (Makofi)