Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hoja ya Dharura (Changamoto ya Kupanda kwa bei za Mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa)

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hoja ya Dharura (Changamoto ya Kupanda kwa bei za Mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa)

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nianze kwanza kwa kuunga hoja mkono. Hoja hii ni hoja mahususi na nadhani matumaini kubwa ya Watanzania yalikuwa ni jinsi gani Bunge litajadili hili jambo na kwa kweli nimefurahishwa kwamba tumepewa nafasi ya kulijadili jambo hili mahususi kwa ajili ya Taifa letu na ni la dharura.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli hali ya wananchi huko nje ni mbaya sana. Leo ninavyozungumza wananchi wangu wa Makete wananunua mafuta kwa bei ya Sh.3,400 mpaka Sh.3,500 na kwenye vidumu wanakaribia karibu Sh.4,600 na kuendelea. Hali ya wananchi wetu ni mbaya na bahati mbaya sana suala la mafuta lina athari nyingi za kimnyororo kwenye maisha ya wananchi. Suala la mafuta sio kama jambo dogo, ni jambo kubwa ambalo linaathiri kuanzia maisha ya mtu wa chini kabisa hadi mtu wa mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali, hata kama tuko kwenye mazungumzo, kwenye vikao tunavyoendelea navyo, hili jambo ni la dharura lazima tulichukue katika udharura wake. Kwenye hizi kodi na tozo ambazo tunazizungumza, bei ya mafuta duniani hadi yanafika Dar es Salaam ni Sh.1,162 kwa lita, lakini msalaba na mnyororo wa kodi zilizoko na tozo zilizoko kwenye mafuta ni zaidi ya shilingi 1,300, yaani bei ya mafuta duniani ni ndogo kuliko mnyororo wa kodi tulizonazo nadhani za nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi niombe Serikali ione umuhimu wa kuzipunguza hizi tozo ambazo hazina umuhimu kwenye maisha ya Watanzania. Kwa sababu hata tukifanya vipi tukasema bei ya mafuta shilingi 1,000 kwa lita lakini kama huu mnyororo hapa wa hizi tozo TBS, TASAC, EWURA... (Makofi)

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Sanga kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Nollo.

T A A R I F A

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, nataka tu nimpe taarifa mzungumzaji badala ya kutumia mifano ya mbali sana kwa nchi zingine, tofauti tuna Zanzibar hapo Zanzibar lita ni Sh.2,600 na huku iko hivyo. Kwa hiyo, tutumie tu ka-treatment ka Zanzibar hapo ili tuweze ku-rescue situation ambayo ni nchi moja. Ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Festo Sanga unaipokea taarifa hiyo?

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, naipokea na hili ndio maana nalisisitiza, hizi tozo ambazo zipo kwenye mafuta zingepunguzwa. Nataka tujenge msingi kwa mfano EWURA, wako kwenye maji, wako kwenye umeme, wako na maeneo mengine; EWURA wangeondolewa mle kwa sababu kwa kipindi hiki, kwa udharura huu, hawana haja TASAC wangepunguziwa lakini hizi excise duty kwenye kodi karibu shilingi 400 zingepunguzwa hizi zote ili tuweze ku-rescue hali ya nchi kwenye Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine nazungumzia tupate mkopo popote pale kwa ajili ya kuweka ruzuku kwenye mafuta ili yaweze kupungua. Kwa sababu tukiendelea kuacha hali hii na kwa jinsi tunavyofanya projection inawezekana mbele mafuta yakazidi kupanda bei, tutasema nini kwa Watanzania. Ni vyema tukaanza ku-rescue kwa uharaka zaidi hali hii kwa kutafuta fedha mahali pengine tukaweka kwenye mafuta, Watanzania wakarudi kwenye hali ya kawaida, nauli zitashuka, bodaboda sasa hivi huko nje ukiangalia hata bei zimepanda, yaani hali sio nzuri kwa wananchi huko nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuiombe Serikali, hatua zinachukuliwa ikiwemo ya kusaidia kuongeza watu wanaoagiza mafuta nje, lakini kwa wakati huu na Mheshimiwa Rais anaupiga mwingi na tunaamini hili atalipiga mwingi kuhakikisha kwamba tunapata fedha ya kuweka ruzuku kwenye mafuta ili bei ishuke.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa na hayo tu kwamba Serikali ichukue hatua hiyo kuhakikisha kwamba tunashusha bei kwenye mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)