Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana na mimi kwa kunipa nafasi kuchangia kwenye hotuba iliyoko mbele yetu na mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara, kwa hiyo, ningependa kushauri Serikali baadhi ya mambo ili tuweze kuona namna ya kuyatatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na jambo la kwanza kabisa, Mheshimiwa Mpakate hapa amechangia vizuri sana kwenye suala la stakabadhi za ghala, lakini yale yote aliyoyasema ili waweze kupata pesa ya kutosha kuna haja ya Sheria ya Stakabadhi za Maghala kuletwa ndani ya Bunge hili ili tuweze kuipitia waongezewe wigo mpana wa kufanya kazi, kwamba maghala yote yasimamiwe na Sheria ya Stakabadhi za Maghala kutoka kwenye bodi ya leseni za maghala. Kwa hiyo, ije sheria, tumuombe Mheshimiwa Waziri hapa ashirikiane na Waziri wa Kilimo na Waziri wa Viwanda na Biashara waone namna ya kuleta sheria sasa maghala yote Tanzania yasimamiwe na Bodi ya Stakabadhi za Ghala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine liko kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwenye ukurasa wa 18; nilikuwa napitia hapa, Mheshimiwa Waziri ameanza vizuri sana anasema; mwenendo wa kupanda bei usipoendana na uhalisia wa soko ni kati ya changamoto zinazokabili sekta yetu ya biashara. Chini ametoa mfano wa bidhaa za kilimo, lakini pia ametoa mfano wa bidhaa za ujenzi; kwa upande wa vifaa vya ujenzi wastani wa bei ya nondo moja ya milimita 12 imepanda kutoka shilingi 20,393 kipindi cha mwezi Machi, 2021 na kufikia shilingi 26,875 mwezi Machi, 2022 maana yake kipindi cha mwaka mmoja kuna ongezeko zaidi ya shilingi 5,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, hiki ndio kinachoongelewa na Wabunge wengi humu ndani na hii ndio maana halisi ya mfumo wa bei na sisi tuko hapa kama Wabunge kuishauri Serikali yetu sikivu ya Chama cha Mapinduzi, lakini pia kutaka kuwasaidia wananchi wote kwamba, tusiambiane hapa kwamba hakuna mfumuko wa bei, mfumuko wa bei upo tena mkubwa na ni real. Lazima sasa sisi kama Wabunge tutafute solution tunatokaje hapa kwenda kudhibiti mfumuko wa bei.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hatua zinazochukuliwa na Serikali, lakini lazima zifanyike hatua za dharura. Kama Waziri anakiri kuna mfumuko wa bei basi tuweze kujadili hili kwa kina na tutoke hapa na maazimio kwamba, ili kupunguza mfumuko wa bei, kwa sababu kuna upandishaji wa bei kiholela holela kwa wafanyabiashara huko chini pasipo kufuata uhalisia wa soko ama kwenye importation documents zao na hivi vitu vinafanyika makusudi kwa wafanyabiashara wenye tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini utetezi wao mkubwa na Mheshimiwa Waziri hapa anasema kutokana na hili jambo ambalo linaendelea sasahivi, kuna hii vita ya huko Ukraine na maeneo mengine, lakini mambo haya ya kubadilisha- badilisha bei hayajaanza karibuni kwenye nchi yetu. Sasa mimi nataka nishauri kwenye mambo mawili matatu, niishauri Serikali na ione.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa leo kama mara ya nne au ya tano ninaongelea suala la ETS kwa sababu tumesema tunatafuta namna ya kuondoa mfumuko wa bei. Ndugu zangu nataka nitoe mfano, ETS ni stamps za kielektroniki zinazotumika na kampuni nyingi, hasa hizi zinazozalisha vinywaji, lakini nimesikia kwamba inawezekana wakaingia mpaka kwenye sukari.

Mheshimiwa Naibu Spika, stamp moja uchapishaji ambayo ni kampuni moja tu pekee sasahivi inaitwa SISPA, anachapisha stamp moja kwa shilingi nane mpaka shilingi kumi; na wale watu wenye viwanda vyao wanapokwenda kulipia zile stamps maana yake watalipa stamps kutokana na bidhaa walizozalisha. Na siku moja nilitoa mfano hata ndani ya Bunge, hata kwenye Kamati kwamba Serikali wanapata kiasi gani kutokana na hizi stamps zinazochapishwa na SISPA?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kushangaza kabisa kwamba Serikali haijataka kujifunza zaidi kwenye hili jambo. Sijaona hatua za waziwazi zilizochukuliwa ili kuweza kuwapunguzia wananchi mzigo wa uzalishaji kwa sababu gharama zote za uzalishaji zinazofanywa na kampuni, kwa mfano kampuni za vinywaji katika kila chupa moja inaweza ikaongezeka kati ya shilingi 10 mpaka shilingi 15 tuseme, lakini mwisho wa siku gharama hizi zinakwenda kwa mlaji wa chini kabisa. Hiyo ni moja ya vitu vinavyoongeza inflation kwenye uzalishaji. (Makofi)

Kwa hiyo, niiombe sana Serikali kabisa na ninafahamu kwamba mkataba mpya wameingia kati ya SISPA na TRA, mkataba ambao haukuwa wazi kwa wawekezaji wengine ambao wangeweza kuzalisha stamps hizi kwa gharama nafuu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaficha nini kwenye jambo hili? Kwa nini hatutaki kuwaondolea wananchi mzigo huu wa kulipia stamps za kielektroniki, jambo ambalo linaweza likafanywa kwa bei rahisi? Kuna wazalishaji wako tayari kuzalisha stamps hizi kwa shilingi mbili, sisi kama Serikali, sisi kama nchi tunang’ang’ania stamp za shilingi kumi kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na katika shilingi kumi hii Serikali inapata 18% tu pesa nyingine yote inayobakia inakwenda kwa yule mtu anayezalisha stamps na kuwauzia watu wenye viwanda. Tuliangalie hili kwa makini na niwaombe sana Wabunge wenzangu tulijadili hili jambo kwa umakini kwa sababu linawaumiza wananchi na sisi tuko hapa tunatafuta namna bora ya kupunguza inflation kwenye bidhaa mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, gharama za uzalishaji wa stamps ni kubwa, wenye viwanda wanalalamika, kila siku wanakuja Bungeni mpaka sasa, mwisho wanatuona sisi Wabunge hatuwezi kuwasaidia kwa sababu, hatujatafuta solution, hatujakaa nao, hatujawasikiliza nab ado tunalazimisha mikataba hii izalishwe na wale watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna jambo lingine lipo kwenye vinasaba vya mafuta. TBS sasahivi wanalipa karibu shilingi 16 kwa lita moja, wanalipa kwa SISPA haohao ambao wanazalisha na hizi stamps za kielektroniki. Tunasema tunataka kupunguza gharama, kwa nini tusiangalie tukatafuta vinasaba vya gharama nafuu zaidi vinavyofanya kazi sawasawa na hivi vinavyoletwa na hizi kampuni, ili kupunguza gharama za uingizaji wa mafuta?(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na malengo ya vinasaba ilikuwa ni kupunguza uchakachuaji. Sasa kama tunataka kupunguza uchakachuaji, tumefanikiwa kwa kiasi gani kwa wakati wote ulipita? Utafiti uko wapi unaoonesha kwamba, kuweka vinasaba kwenye mafuta kumepunguza huu uchakachuaji unaosemwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatujawahi kuletewa hapa Bungeni sisi tukafanya review. Sana sana tumewaongezea mzigo sasahivi TBS, TBS wanalazimika kulipa kwa SISPA, EWURA nao wamalazimika kulipa kwa SISPA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kwenye suala la Mtwara Corridor, Bandari ya Mtwara pamoja na Mchuchuma na Liganga. Hivi ni lini Serikali itaamua kwa dhati kabisa kufanya uzalishaji wa makaa ya mawe, lakini pia kufanya uzalishaji wa chuma? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunahangaika hapa kwenye suala la bei ya mafuta. Kwa mfano gesi yetu, sasa hivi ni zaidi ya miaka 20 au miaka 30 tuseme tunaongea kuhusu Mchuchuma, tunaongea kuhusu Liganga, tunaongea kuhusu gesi ya Mtwara. Kama tungekuwa tumeanza kutumia gesi tusingehangaika leo na suala la bei ya mafuta, wako wapi watu wenye kufanya maamuzi? Kwa nini gesi ile ambayo tunajua kabisa iko pale na inatakiwa itumike na wananchi haitumiki? (Makofi)