Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Madini

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Madini

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na ninaomba pia kutumia nafasi hii kusema ninaunga mkono hoja, lakini kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na Watendaji wake wote kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya.

Mheshimiwa Spika, mimi labda nianze kusema tunafanya vizuri sana na CSR kwetu hasa Jimbo langu la Geita Mjini, lakini pia tunafanya vizuri sana na local content kwa hiyo ni vizuri kule ambako bado wanapata shida wakaja kujifunza namna ambavyo tunafanya na hasa kwenye local content namna ambavyo wakulima wameshirikishwa katika maeneo mbalimbali ya Saraguro na Mgusu kwenye kushiriki kuhudumia mgodi, Mheshimiwa Waziri nakupongeza sana kwenye eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Mheshimiwa Waziri ulifanya ziara Geita na kwenye ziara hiyo tulikuwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa, ulipokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi wa Geita na Mheshimiwa Waziri naomba ni-quote sehemu ya hotuba ya Ndugu Paul Young alipokuwa kwenye World of Engineers huko Australia alisema ‘‘Mining sustainably within a community should provide relief from poverty, hunger and safety hood for local communities, this is not considered to be charity, it is about being a part of a community good health and educational aspiration’’ na akamalizia kusema ‘’however extraction of metals and mining of industrial minerals must be done sustainably, this means giving consideration to people, the environment and the economy, human aspect including heath, social and cultural element’’.

Mheshimiwa Spika, ipo shida nimelazimika ku-quote haya maneno ili Mheshimiwa Waziri aweze kunielewa. Ilikuja ziara ya Mawaziri wanane Geita, wananchi wakazungumzia mgogoro wa miaka 20 karibu na tatu kwa wananchi ambao wanaishi kwenye vigingi na mipasuko, Mheshimiwa Rais wa sasa akiwa Makamu wa Rais alishatoa maelekezo suala hili lishughulikiwe, Mheshimiwa Rais Hayati Magufuli alitoa maelekezo, Mawaziri wote tangu Profesa Muhongo na Mawaziri wengine na Mheshimiwa Biteko alitoa maelekezo ishughulikiwe.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa mitaa karibu saba wanaishi kwenye mgogoro wa mgodi wa vigingi kwa miaka 23 na matokeo yake wananchi hawa wanaishi kwa umaskini mkubwa kwa sababu Serikali imeshindwa kufanya maamuzi.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, mitaa ninayozungumzia haina barabara, haina maji, haina shule, haina zahanati hawaruhusiwi kupima viwanja kwa sababu tu eneo wanaloishi ni ndani ya leseni ya mgodi. Maelekezo yametolewa na Serikali, Kamati imetoa maelekezo kwamba hawa wananchi wapimiwe mgodi unakataa. Vimefanyika vikao vya kila namna imeshindikana.

Mheshimiwa Spika, nataka kusema jambo moja hapa, Mheshimiwa Waziri alizungumza na wafanyakazi wa GGM akasifia Serikali kwamba sasa 95 percent ya watumishi wa GGM wa menejimenti, niseme wameondoa 95 percent ni Watanzania, lakini wafanyakazi walimwambia kuwepo kwa sehemu kubwa ya waswahili kwenye menejimenti kumeongoza matatizo makubwa na urasimu kuliko ilivyokuwa Wazungu. Tatizo hili linakuja kwa sababu Waswahili hawafanyi maamuzi ya kum-favor mtanzania hata kama anaona sheria inaruhusu. Nazungumza hivi kwa sababu malalamiko ya watumishi wa GGM ni makubwa mno na uonevu ni mkubwa kuliko ilivyokuwa zamani wakati Wazungu ni wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa wananchi wanayo haki ya maeneo yao, lakini wamekataa wanasema sisi hatufanyi. Tumeshughulika na jambo hili kila mkutano, kila hotuba halifanyiwi maamuzi, namwomba Mheshimiwa Waziri…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Muda wake umeshaisha anamalizia sekunde thelathini.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Namwomba Mheshimiwa Waziri wapo watumishi pale wa mahusiano ambao wanazuia maelekezo ya Serikali achukue hatua, bila kuchukua hatua hatutafikia suluhu ya wananchi hawa ambao wanailamu Serikali bila sababu ya msingi na sheria zipo wazi.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)