Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Madini

Hon. Masache Njelu Kasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Madini

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami kupata nafasi niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Madini.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na watendaji wake, kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaifanya kuhakikisha kwamba sekta hii ya madini inazidi kukua siku hadi siku. Pia niipongeze Wizara kwa kazi nzuri ambayo inaendelea kuifanya katika kuwawezesha wachimbaji wadogo ili waendelee kushiriki kwenye uchumi wa madini ambao unawawezesha kushiriki kwenye uchumi huu na katika kujitafutia riziki na kuweza kulipa kodi.

Mheshimiwa Spika, lakini wachimbaji wadogo hawa wameweza kuendelea na kuwezeshwa katika kupata maeneo ya kufanyia kazi, kupata ama kupewa leseni kwa maeneo ambayo yanaonekana yana madini. Lakini pia tuwapongeze Wizara kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wameendelea kuifanya katika kutoa semina mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo tumeona kwamba kazi nzuri inaonekana kufanyika, na kazi hii inayofanyika na Wizara inasababisha hata maduhuli ya Serikali kuongezeka. Tukiangalia mwaka wa fedha uliopita kiasi cha fedha ambazo kiliingizwa na mwaka huu wa fedha zaidi ya asilimia nne zimeongezeka. Hii ni kazi kubwa sana na kwa hiyo Wizara maana imechangia kwenye Pato kubwa la Taifa.

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na kazi kubwa hii nzuri inayoendelea kufanyika tunawapongeza pia Wizara kwa kuhakikisha kwamba wanaendelea kuzishirikisha taasisi za kifedha ambazo zimeonana na wachimbaji wadogo ili kuhakikisha kwamba wanapata mikopo midogo midogo itakayowawezesha kupata vifaa na vifaa hivi vinawawezesha wao kuweza kurahisishia uchimbaji wao.

Mheshimiwa Spika, pamoja na taasisi za kifedha kuwapatia wachimbaji wadogo lakini bado masharti ya taasisi hizi yamekuwa magumu kuwawezesha wachimbaji wadogo hawa kuweza kunufaika. Tuiombe Wizara, pamoja na kwamba wameendelea kufanya kazi kubwa katika hili lakini pia waendelee kuongea na taasisi za kifedha hizi ili benki na taasisi nyingine walegeze haya masharti waliyonayo ili kuwawezesha wachimbaji wengi wadogo hasa wale wa chini kabisa waweze kunufaika.

Mheshimiwa Spika, leo hii wachimbaji wadogo ambao wananufaika ni wale ambao wanaweza wakapata mascaveta, mabuldoza pamoja na ma-tipper, yale makubwa.

Mheshimiwa Spika, leo hii wachimbaji wadogo ambao wananufaika ni wale ambao wanaweza wakapata ma-excavator, bulldozer pamoja na tipper kubwa, lakini tunataka tushuke chini zaidi kwa wale wachimbaji wadogo ambao wanaweza wakapata fedha ya kuwanunulia makarasha, wakapata fedha ya kujenga plant na vitu vingine kama hivyo ili mzunguko huu wa fedha uweze kwenda kwa wachimbaji wengi zaidi na wao pia waweze kujiwezesha kiuchumi waweze kulipa kodi zitakazoisaidia nchi yetu hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo pamoja na kuwezeshwa huko wachimbaji lakini taasisi ya GST iendelee kufanyakazi yake kuhakikisha kwamba inaendelea kufanya tafiti hizi na tafiti hizi ziweze kushuka kwa wachimbaji wengi wadogo na walio wa chini.

Mheshimiwa Spika, leo hii tafiti nyingi ambazo zinafanyika zinaishia kwenye makabrasha ofisini ninaomba sana taasisi ya GST iweze kufanya kazi hii na ihakikishe inatohoa kwenye lugha nyepesi na rahisi ambazo zitaweza kuwafikia wachimbaji wetu wa kule chini, ziweze kufika kwenye ngazi za Mkoa, kwenye ngazi za Wilaya na wachimbaji wetu wa kule Nyang’hwale wachimbaji wetu wa Chunya, wachimbaji wetu wa Matundasi Sangapi na maeneo mengine waweze kuzipata hizi na waweze kunufaika pamoja na hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona taasisi ya GST ilichukua ushauri wetu, mwaka jana tuliwaambia hapa waanzishe maabara kwenda kwenye Mikoa yetu, nashukuru sana nimeona kwenye taarifa hapa maabara hizo sasa zimeanza kuanzishwa tumeona Geita kule zimefunguliwa maabara hizi. Ninaomba sasa Serikali kwa kuwa imeanza kufungua maabara hizi na sisi watu wa Nyanda za Juu Kusini, watu wa Mkoa wa Mbeya na hasa Wilaya ya Chunya ambako ndio wachimbaji wakubwa sana wa dhahabu tuhakikishe kwamba maabara hizi sasa zinaenda kuanzishwa haraka zaidi ili wachimbaji wetu hawa wapeleke sampuli zao pale, wawe na uhakika na kile ambacho wanaenda kukichimba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo pia hata ule uchorongaji, nimeona hapa wameagiza mashine za uchorongaji, mashine hizi zitakapofika tuhakikishe kwamba zinaweza kuwafikia wachimbaji wetu hawa.

Mheshimiwa Spika, wachimbaji wengi wanachimba sasa hivi katika hali ya kubahatisha hasa wale wachimbaji wadogo, leo GST wanasema kwamba wanaboresha kanzidata yao ya miamba ni jambo zuri sana, lakini kuboresha peke yake haitoshi! Waboreshe hizi kanzidata na taarifa hizi za miamba ziweze kuwafikia wachimbaji wengi wadogo, wachimbaji hawa watakapoweza kupata taarifa ambazo ni nzuri na sahihi ndivyo watakavyoweza kuongeza uzalishaji wao na wakiongeza uzalishaji wao ndivyo ambavyo wataweza kulipa kodi kwa Serikali na Serikali itazidi kupata mapato na tutaona nchi yetu itazidi kupaa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia …

SPIKA: Sekunde thelathini.

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, basi nitaleta mchango wangu kwa maandishi lakini ninapongeza na ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)