Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kupata nafasi hii, lakini pia ningependa kufanya masahisho ya jina langu, naitwa Cosato David Chumi, sio Chumu kama ulivyokuwa umesema na hilo la kwanza ni Cosato siyo Cosota. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kuishukuru Wizara, lakini pia kuishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kuja na Wizara ambayo siyo tu ita-deal na michezo na habari lakini pia ita-deal na sanaa. Naipongeza sana na ninawapongeza watendaji wote kwa hotuba hii na maandalizi yote ya bajeti yao. Najua ndiyo tunaanza; mwanzo ni mgumu lakini pia mwanzo ni muhimu, lazima tuanze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumpongeza Waziri Kivuli Mheshimiwa Sugu. Huyu bwana, ndugu yangu, nashangaa hajanitaja katika watu waliochangia mafanikio yake, kwa sababu toka akiitwa II Proud, baadaye Mr. II; halafu Sugu na sasa hivi Mheshimiwa. Tumefanya naye kazi Arusha kule, mvua ikanyesha, onyesho likabuma; lakini namshukuru kama promoter niliyekuwa nimeandaa onesho lile hakunidai, maana yake mvua ilinyesha, onesho likabuma. Kwa hiyo, nakupongeza brother, tumetoka mbali. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimesikia kwamba kutakuwa na mechi ya Wabunge wa Simba na Yanga; na mimi nakubali. Huko nje tumetaabika sana, lakini kwenye mechi hiyo napenda kuwahakikishia wapenzi na mashabiki wa Simba tutahakikisha kwamba tunawafuta machozi. Timu yetu kabambe, yupo Mheshimiwa Godfrey Mgimwa hapa, yupo Mheshimiwa Nassari, tafadhari uanze kuja mazoezini tuwafute mashabiki machozi humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo ya utangulizi, nianze kwa kuzungumzia mchezo unaopendwa sana kama wenzangu walivyosema mchezo wa mpira wa miguu (soka). Mimi nasema hii soka yetu bila vifaa na viwanja vya michezo ni bure. Kwa hiyo, naishauri Serikali kwa kushirikiana na TAMISEMI, kwanza tuanze kulinda viwanja katika shule zetu maana huko ndiko ambako vipaji vinatoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila vifaa, bila viwanja, hatuwezi kwenda kokote. Pia kodi ya vifaa vya michezo; leo hii kijana anayecheza mpira, kiatu chake siyo chini ya shilingi 40,000. Hata hawa TFF nina taarifa kwamba wameleta mipira size mbili, tatu na nne ambayo ilikusudiwa kwa ajili ya kugawa kwenye shule kama kifaa cha kufundishia kwa sababu nacho ni kifaa; wameshindwa kuigomboa kwa sababu wanadaiwa kodi karibu dola 18,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba Mheshimiwa Waziri tunapokusudia kuinua michezo, hebu tuangalie viwanja shuleni, viwanja mitaani kwa kushirikiana pia na Wizara ya Ardhi. Watu wa Mipango Miji wanapopanga mipango, watenge pia maeneo ya viwanja; lakini pia Serikali za Mitaa kwa maana ya TAMISEMI, wavilinde viwanja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niulize, hivi sisi football yetu, hii soka yetu Mheshimiwa Waziri ni ya ridhaa au ni ya kulipwa? Kwa ufahamu wangu naambiwa ni ya ridhaa, lakini ndani yake humo humo tunaambiwa kuna wachezaji ma-pro; wako akina Ngoma, akina Kiiza, wanalipwa madolali ya pesa. Sasa hebu tuirasimishe ieleweke moja, iwe ya kulipwa, tui-commercialize ili ituongezee mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hiyo timu yetu ya Taifa sijui kama Charles Boniface Mkwasa analipwa marupurupu kama waliyokuwa wanalipwa wale makocha wa kigeni. Tafadhali, hebu tujaribu kuwajengea uwezo makocha wetu wazawa, lakini pia tuwalipe kama tunavyowalipa wageni. Sasa kama sisi timu ya Taifa makocha wetu hatuwajali, je, vilabu, vitawajali akina Jamhuri Kiwelu? Vitaanzia wapi? Hebu tuoneshe mfano katika hili. Kocha wa timu ya Taifa alipwe kama tunavyowalipa wale wageni. Nina hakika akilipwa vizuri tutayaona matunda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia kuhusu mchezo wa riadha; wenzetu nchi jirani Kenya na Ethiopia mchezo huu umewasaidia sana kutangaza utalii wa nchi zao. Leo hii New York Marathon, Tokyo Marathon humkosi Mkenya wala Mhabeshi. Hebu tuuone huu mchezo; nina hakika kuna ndugu zangu kule kwa akina Mheshimiwa Massay Flatei wanaweza kabisa, wako hata Singida kwa jirani yangu hapa Mheshimiwa Mama Mlata. Hebu tuwekeze pia nguvu katika mchezo huu kwa sababu itatusaidia kututangazia utalii na utalii unaongoza katika kutupa mapato ya fedha za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze sasa kwenye sanaa. Napenda kuwapongeza wasanii wa Jimbo langu la Mafinga Mjini. Nafahamu wanaishi kama watoto yatima, lakini wanajikongoja. Ninaamini kwa mipango mizuri, tutafika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza, hivi hii BASATA kazi yake kubwa ni kuwafungia tu wasanii? Kama ikiwa katika filamu, tuna Bodi ya Filamu, inakagua filamu ndipo inatoa kibali ziendelee; kwanini pia katika suala la muziki, video tusiwe na utaratibu huo? Kwa sababu moja, video imeshaingia mtaani, imeshafanya damage katika jamii kimaadili, lakini pia kuna damage ya msanii, ameingia gharama. Leo hii unakuja unamfungia, ulikuwa wapi BASATA? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, hata COSOTA na Bodi ya Filamu, kazi zao namna wanavyofanya wamejielekeza tu pale Dar es Salaam, usiwaone hawa akina Singo Mtambalike hawa, akina Richie hawa; toka wameanza kufanya hizi kazi, utaratibu wa kutunza kazi za ndani kwa kweli siyo mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kuna kitu kinaitwa zaga zaga; ukienda Kariakoo pale watu wametandika chini hizi filamu za kutoka nje za series, zinauzwa shilingi 1,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, msanii wetu unamtaka aweke sticker, lakini pia hata hiyo sticker yenyewe kuipata mpaka uende Dar es Salaam. Sisi tunataka mapato, sticker ya TRA mpaka uende Dar es Salaam. Kwa nini tusiweke utaraibu sticker zipatikane pia mikoani na katika ofisi za TRA kuwarahisishia hawa wasanii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, hata hizi ada, COSOTA na BASATA, kama unataka kuandikisha filamu, dakika moja ni shilingi 1,000; kwa ujumla ukitaka kuandikisha masuala haya, uwe registered na BASATA na COSOTA na Bodi ya Filamu, sio chini ya shilingi 340,000 na msanii atoke mkoani ajigharamie nauli, malazi na bado hata akifika hapo ofisini ushirikiano anaoupata ni wa hali duni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali ielekeze BASATA pia katika kutoa elimu kwa wasanii kupitia Maofisa Utamaduni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema tayari nina kitambaa cheupe, ndugu yangu Waitara baadaye twende kwa King Kiki tukapeperushe kitambaa. Jamani kazi na dawa. Pia, tunawaunga mkono hawa wasanii, huyu mzee ametoka mbali. Kwenda kwetu pale kama Waheshimiwa Wabunge, tunamtia moyo.
MHE. COSATO D. CHUMI: Hata kama hatumpi chochote ndugu zangu, nadhani Sugu utawashawishi wenzako huko, hebu twende tukamtie moyo huyu mzee na kama hauna kitambaa, mimi nitakuazima; kama huna kitambaa, wewe chukua hata karatasi tukapeperushe. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja.