Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Madini

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Madini

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia Wizara hii ya Madini mimi ni Mjumbe wa Kamati.Kwanza nianze kwa kumuunga mkono mjumbe aliyemaliza kuzungumza dadaangu tulivyopitisha hii Sheria ya kurudisha masoko kwenye maeneo husika sisi watu wa Geita ndiyo tulileta hiyo hoja humu mwaka 2017/2018 na Bunge lako Tukufu likatupitishia Sheria.

Mheshimiwa Spika, sisi watu wa Geita ni wanufaika namba moja, na watu wa Simanjiro ningewashauri waje wajifunze kwetu, kwasababu tunakusanya pale sokoni takriban bilioni tatu. Kwa hiyo ningeomba tu kila mtu amepewa neema tofauti, na Mheshimiwa aliyezungumza hii hoja aridhike maana ana utalii mwingi. Arusha ni sehemu ambayo ina utalii mwingi, tusioneane wivu tuache na hii miji midogo nayo ikue kwa kukusanya Service Levy.

Mheshimiwa Spika, suala la pili nilikuwa naomba kushauri kuhusiana na suala la refinery. Mheshimiwa Waziri anafahamu tumetengeneza refinery kubwa sana Geita pamoja na Mwanza na sisi Kamati tulienda kutembelea. Hata hivyo, ninaona kama tumewaingiza chaka wale waliowekeza ile biashara pale. Kwa mwenendo tunaoenda nao sisi wazoefu wa ile biashara; ningependa Mheshimiwa Waziri unisikilize vizuri; hii dhahabu mpaka inaenda kwenye refinery unakuwa umeshatozwa mirabaha ya kutosha, wewe unafahamu; lakini ukifika pale ukishafanya tena usafi ule unatakiwa ulipe tena asilimia sita.

Mheshimiwa Spika, haiwezekani kulipa asilimia sita ilhali hii dhahabu naweza kuibeba nikaenda nayo nje kule Dubai nikaisafisha kwa 0.25. Kwa hiyo ninaona kabisa kwamba kama mnaweza kuja na Sheria kidogo ya kibabe kwamba usisafirishe mpaka ufanyie hapa lakini hebu jiulize ungekuwa wewe ndiye mfanyabiashara. Kwa hiyo ningeomba Serikali ione namna ya kushusha hata kama ni asilimia mbili ikawa kivutio; na hizi ndizo attachment za Royal Tour ya Mheshimiwa Rais kwamba watu wanapokuja hapa waje wajifunze vitu vingi tusiweke bei kubwa watu wakawa tena watoroshaji tukaanza kukamatana na kunyang’anyana ni vizuri tukatembea tukaiga kwenye hizo nchi ambazo tayari zina refinery na watu wanapeleka kwenda kusafisha.

Mheshimiwa Spika, suala lingine, ninashauri Mheshimiwa Waziri turudishe suala la minada ya madini. Tunapofanya minada ya madini tutaingiza watalii wengi sana kuja kununua kwenye masoko, na tutangaze tuna madini ya aina gani. Watu watakuja, asiponunua dhahabu asiponunua madini atanunua hata kinyago naona tutakuwa tunaendelea kum-support Mheshimiwa Rais katika ile filamu yake ya Royal Tour. Twende mbali zaidi kwamba Mheshimiwa Rais hakuweza kumaliza kuvitembelea vivutio ambavyo viko kwenye nchi yetu. Tutakapofanya hii minada wazungu watakuja na watu wengine wageni tutapata kipato kikubwa zaidi. Kwa hiyo, nilikuwa naomba suala la minada pia liweze kurudishwa.

Mheshimiwa Spika, lakini lingine, nimesikia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, kwamba ana mpango wa kufungua duka sijui la vilipuzi. Nilikuwa naomba sana kuishauri Wizara; unajua kwanza Shirika letu la STAMICO ndiyo kwanza linaanza kupanda lina madeni na uwezo wake ni mdogo; biashara inatakiwa iachiwe watu wa Private Sector kwa sababu kwenye Private Sector sisi tunapeana kukopeshana ninaweza nikachukua kilipuzi au nikachukua carbon nakudai inabidi nikasubirie mpaka uchome.

Mheshimiwa Spika, sasa ninyi watu wa procurement sijui ugavi sijui vitu gani tunaenda kuziteketeza hizi hela wakati shirika lenyewe halijasimama tuiachie private sector ifanye hizi biashara kuliko kuingia kwenye vitu ambavyo naona hatutafanya vizuri.

Mheshimiwa Spika, lakini lingine nataka nichangie, nalo ni kuhusu dhahabu inayopelekwa sokoni. Mheshimiwa Waziri upatikanaji wa dhahabu wewe umetoka kwenye mkoa wa dhahabu ninaweza kuwa hata natembea nikakaokota barabarani pakuuza ni sokoni. Sasa, nikifika sokoni kumeanzishwa mtindo, kwamb watu wako tena wanataka mpaka niwe na risiti nilikoitoa dhahabu. Sisi lengo letu ni dhahabu na nchi yetu kimataifa ina dhahabu ambayo haina matatizo kwa nini tuanze kuhojiana? Kwa nini tusiachie uhuru watu ambao pengine wanapata dhahabu kwa njia kama za kuokota iweze kuuzwa pale sokoni?

Mheshimiwa Spika, la mwisho, mimi natoka mkoa wa Geita sisi ndiyo wanufaika namba moja wa CSR. Nimemuona mkuu wa Mkoa wa Mara anafukuzana na Afisa Mahusiano kwa sababu ya kutokutekelezeka kwa miradi. Sisi watu wa Geita ni waathirika wakubwa sana kwenye miradi ya CSR, na kumekuwa na mabishano kati ya mgodi na halmashauri nakuomba Waziri utakapohitimisha ili nisichukue shilingi yako uniambie ni lini uko tayari tuwaite GGM kwako na sisi Baraza tuje kwako ili uje utuwekee msimamo mzuri ili kazi zikaweze kwenda kutekelezeka. Nashukuru sana.