Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kuchukua fursa hii kukushukuru wewe kwa kunipa fursa, lakini awali ya yote naomba kumshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyenipa nguvu na uzima. Nimeweza kuwasilisha hotuba yangu hapa, lakini nashukuru sana kwamba Waheshimiwa Wajumbe wameweza kuichangia.

Mheshimiwa Spika, kubwa zaidi, namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake makini na madhubuti sana ambao umetuwezesha kufanya kazi zetu ziende vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Muungano na Mazingira, namshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kweli wasemavyo vijana ameupiga mwingi sana Mama Samia Suluhu Hassan. Sisi ametuwezesha kuhakikisha kazi yetu inafanyika vizuri katika ushiriki wake wa pamoja kama kuiongoza nchi.

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana, kama alivyosema awali, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa msaada mkubwa wa kuhakikisha katika upande wa Muungano, akishirikiana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, Makamu wa Rais ambaye ni msimamizi wangu mkuu katika Ofisi yangu, amenisaidia sana kutimiza majukumu yetu. Mheshimiwa Waziri Mkuu yupo hapa, kwa kweli Waziri Mkuu wetu sisi ni mwalimu kwetu, amekuwa kiongozi makini na hodari sana kutuwezesha tumeweza kufika hapa. Nakushukuru wewe na timu yote ya wasaidizi wako waliokuwa karibu kuhakikisha mambo ya Bunge yanakwenda vizuri na leo hii tunakwenda kuchakata bajeti yetu ya Muungano na Mazingira.

Mheshimiwa Spika, naomba kuishukuru familia yangu kwa ujumla, kwa kweli wamenipa msaada mkubwa sana kuhakikisha natimiza vyema majukumu yangu. Halikadhalika, nawashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Kisarawe kwa kuniombea muda wote wakati natimiza majukumu yangu nikiwa katika nafasi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafahamu tuna uchache wa muda, lakini napenda kushukuru Kamati zote hizi mbili ambazo zimewasilisha maoni yake hapa. Kwa ufupi tu niseme kwamba, Ofisi yangu inapokea maoni yote. Kwa kweli maoni yote yameelekeza kwa ajili ya kuhakikisha Wizara hii inafanya na kutimiza majukumu yake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kamati ya Katiba ya Sheria imeshauri mambo mengi sana kuhusu Muungano, hili ni jukumu lake. Hivyo naomba niseme jambo moja; kwanza kipekee niishukuru Kamati ya Katiba na Sheria. Kamati hii ndani ya mwaka mmoja imeweka legacy ya kuhakikisha hoja 11 za Muungano zinatatulika. Kwa dhati niseme wazi kabisa, imefanya kazi kubwa sana na Wajumbe wa Kamati. Maoni kama mlivyowasilisha hapa, kazi yetu ni kwenda kuyachakata, kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, naishukuru sana Kamati ya Mazingira, imekuwa mwalimu na kiongozi katika upande wa Mazingira muda wote. Naomba nikwambie; katika Kamati, Kamati hii imekuwa ni mwalimu na mwelekezi. Maoni yote ya Kamati yalivyozungumzwa, kama nilivyosema, muda wenyewe ni mfupi hapa, mliyoyasema kazi yetu ni kuyatekeleza. Mimi Jafo na watu wangu ni nani tushindwe kutekeleza maoni ya Kamati? Jukumu letu kubwa ni kwenda kufanya kazi katika maoni yote kama Kamati ilivyoelekeza.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana Hotuba yangu leo hii imechangiwa na Wajumbe takribani 13. Siwezi kuwataja wote kwa ujumla wake, lakini niseme kwamba ile michango yote kama nitakayotoa hapa kiufupi na Naibu wangu aliyotoa hapa, mengine yatakuja kwa maandishi.

Mheshimiwa Spika, kuna suala ambalo naomba niseme kwa ujumla wake. Kuna maombi mahsusi ya kwenda kushughulikia hoja za Muungano zilizobakia. Naomba niseme kwamba tulikuwa na hoja takribani 25. Katika kipindi hiki cha uchakataji wa hoja za Muungano, tulipofika mwaka 2020 hoja saba ziliweza kutatuliwa kati ya hoja 25, tukabakiza hoja 18. Naomba niwashukru Viongozi Wakuu, ndani ya kipindi hiki cha mwaka mmoja kama nilivyosema, tumeweza kutatua hoja 11. Ni legacy ya kwanza imewekwa katika utatuzi wa hoja za Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niwahakikishie wote, imani yetu na kazi yetu kubwa tutakwenda kuifanya, sisi hatulali, tutahakikisha miongoni mwa changamoto, zile hoja saba za Muungano tutakwenda kuzifanyia kazi. Halikadhalika, na hata zile ambazo tumezifanyia kazi, tutakwenda kuhakikisha tunaweka utaratibu mzuri wa kisheria na kila kitu. Lengo kubwa hoja zile ambazo imefanyiwa upembuzi ziweze kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, ndugu yangu amezungumza hapa masuala ya kikanda na Kimataifa, ni miongoni mwa hoja ambayo imefanyiwa kazi mwaka 2020. Kazi yetu kubwa sasa hivi ni kuweka utaratibu mzuri kama utaratibu wa TFF na wenzake, yote haya ni masuala ya ushiriki katika masuala ya kikanda na Kimatiafa. Tutayafanya haya vizuri. Lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba tutakwenda kuweka katika utaratibu mzuri.

Mheshimiwa Spika, naomba niwashukuru sana Wabunge mbalimbali hasa kutoka Zanzibar, kwa sababu mmekuwa mkitoa hoja; Mzee wa Mtambwe kule na maeneo mengine; dada yangu wa Pandani na maeneo mengine, wote kwa ujumla wake, mmenisaidia sana kuhakikisha wakati natimiza majukumu yetu, kuna masuala ya kimuungano na masuala ya kimazingira. Kama tunavyofahamu kwamba masuala ya kimazingira yapo huku upande wa Bara na Zanzibar kuna Wizara ya kimazingira, lakini Mazingira ni crosscutting issue, huwezi kutofautisha na upande mmoja. Ndiyo maana hata baadhi ya miradi yetu mingine tunaitekeleza kule Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, naomba niwahakikishie Wabunge wote mlichangia humu ndani, kwa upande wa kimazingira nitashirikiana na mwenzangu Waziri wa Zanzibar katika Ofisi ya Makamu wa Kwanza Rais anayeshughulika na masuala ya Mazingira. Tutaenda kujadiliana kwa pamoja. Kwa mfano, siku nilipoenda kwa ndugu yangu Sumai, pale Nungwi, kweli ukifika pale unakuta hali ni mbaya.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge alichokisema ni kweli. Nami naomba niseme, nimekuta kuna shida kubwa ya maji, na ndiyo maana katika utashi huu hata Zanzibar wana mradi mkubwa sana wa maji, lakini walikuwa wana changamoto ya upatikanaji wa suala zima la mchanga na kokoto. Tumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hoja ile sasa imepata ufumbuzi kuruhusu mchanga uende kule kwa ajili ya miradi ya maji kwa sababu kuna changamoto ya mchanga katika utekelezaji ule.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa ujumla wake miradi hii mingine ya kisekta naomba niwahakikishie, kwamba tutashirikiana kwa pamoja kwa kuwa hii ni nchi yetu sote. Naomba niwaambie ndugu zangu uongozi ni dhamana. Licha ya kufanya kazi kama unatenda kazi lakini uongozi ni sehemu ya ibada. Unapofanyakazi kwa kuwahudumia watu na kupata tija na kupata mafanikio makubwa na wewe Mungu anakulipa. Kwa hiyo naomba niwahakikishie, kwamba yale yote ambayo yamejadiliwa hapa tutajitahidi kushirikiana kwa pamoja kwa mustakabali mpana wa Taifa letu hili. Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naafiki.