Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Juma Othman Hija

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tumbatu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kukushukuru wewe kwa kunipatia nafasi hii ya kutoa mchango wangu katika hotuba hii ya makadirio na mapato ya Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira) kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Mheshimiwa Spika, pia napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake na watendaji wake wote kwa kutayarisha na hatimaye kuiwasilisha hotuba hii katika Bunge lako tukufu kwa ufasaha na umakini mkubwa.

Mheshimiwa Spika, katika kuchangia hotuba hii napenda kuchangia katika maeneo yafuatayo; nikianza na fedha za Mfuko wa Jumbo; napenda kuipongeza na kuishukuru Serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka mpango huu wa Mfuko wa Kuchochea Maendeleo katika Majimbo yote nchini.

Mheshimiwa Spika, kama inavyosomeka dhana ya mfuko huu ni kuchochea maendeleo, lakini kwenye baadhi ya majimbo mengine huwa haikidhi dhana hii; kwa mfano katika majimbo ya Zanzibar kama inavyojulikana kuwa mwaka 2015 ulifanyika ukataji mpya wa majimbo, majimbo mengine yameongezeka sana. Miongoni mwa majimbo hayo ni jimbo la Tumbatu.

Mheshimiwa Spika, kiasi ya fedha tunachopata ni kile kile tangu jimbo halijaongezeka, hivyo basi tunaomba Serikali ichukue hatua maalum ya kuongeza fedha katika majimbo hayo yaliyoongezeka.

Mheshimiwa Spika, pili ni kuhusu tathmini iliyofanywa juu ya Taasisi za Muungano; napenda kuipongeza Serikali kwa kufanya zoezi hili. Hili ni jambo muhimu sana ili kujua mahitaji ya taasisi hizi. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri amesema kuwa ni taasisi 20 ndio zilizofanyiwa tathmini, lakini Mheshimiwa Waziri hakuzitaja. Ushauri wangu katika jambo hili kwa Serikali ni kuzitaja taasisi hizi ili nasi tuzitambue kwa manufaa ya wananchi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, tatu ni kutoa elimu kwa umma kuhusu Muungano; napenda kutoa pongezi za dhati kwa Serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua hii ya kuwaelimisha wananchi wa Tanzania. Ni dhahiri kuwa mpaka hii leo baada ya miaka 58 bado wapo watu hawajui maana ya Muungano.

Mheshimiwa Spika, zoezi hili haliwezi kufanikiwa kwa asilimia kubwa kutokana na vyombo vinavyotumika kueneza elimu hii. Kwa mfano wananchi wa vijijini hawawezi kuwa na redio, tv, mitandao ya kijamii au majarida yaliyotajwa katika hotuba hii. Hivyo ushauri wangu katika jambo hili ni kutafuta njia sahihi ya kuwafikia wananchi wa vijijini.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.