Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote napenda kuipongeza sana Wizara na watendaji wake wote.

Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa juhudi alizochukua kukutana na asasi zisizo za Kiserikali ambazo zinafanya kazi ya kuhifadhi mazingira. Wana asasi wamefarijika sana kwa kuwatambua kwa sababu sisi wana asasi zisizo za kiserikali tunafanya kazi kubwa sana kuisaidia nchi hii kuhifadhi mazingira yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kututambua kwako Mheshimiwa Waziri tumefarijika sana. Tunachoomba, tunapokuja Wizarani kwako, sisi wana asasi utupe ushirikiano wa kutosha ili tuweze kutekeleza majukumu yetu pale ambapo tuna kwama.

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la mazingira, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa juhudi zinazofanywa katika kuhifadhi mazingira ikiwemo upandaji miti. Hata hivyo nataka niishauri Serikali, kwa msamiati wa upandaji miti, ni bora sasa twende na msamiati wa Uoteshaji wa Miti. Kwa sababu tunapopanda miti, baadaye hatujui inakua au haikui; lakini tukiotesha tutaifuatilia tangu tumeipanda mpaka inakua na kuona imefika hatua gani? Tunapanda miti mingi lakini mingi inakufa njiani, kwa hiyo, ni bora tuoteshe miti ili kuisimamia miti hii tuone inakuwa endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nijikite kwenye upande wa Muungano. Muungano wetu umefikisha miaka 58, ni safari ndefu, tumeanza mbali; na Muungano huu ni Tunu na Hazina ya Tanzania. Mpaka kufikia miaka 58 Muungano huu umepitia changamoto nyingi sana mpaka kufikia hapa. Changamoto ya kwanza ya kuhakikisha Muungano huu hauendelei, ni pale alipouawa Rais wa Kwanza wa Zanzibar Mheshimiwa Abeid Amani Karume. Hilo ndilo jaribio la kwanza la kutaka kuona Muungano huu hauendelei. Tusishangae kwamba bado Muungano huu kuna watu wanautazama kwa jicho la husuda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika miaka 58, chochote kinachokua kinakuwa na changamoto. Katika kukua kuna changamoto za Muungano, na changamoto hizi hazitaisha kwa sababu Muungano huu unakua na nchi inabadilika na dunia inabadilika na miundombinu inabadilika. Kwa hiyo, changamoto zitaendelea kujitokeza kila Muungano huu unapoendelea kukua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachoshauri, Serikali iendelee kuzitatua changamoto hizi pale zinapojitokeza kwa wakati muafaka ili kuepusha manung’uniko, chuki na kejeli kwa Muungano huu. Tukizitatua changamoto zetu kwa wakati muafaka, Muungano huu utaendelea kudumu na kupendwa kwa muda wote na hakutakuwa na manung’uniko na chokochoko zozote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni imani yangu na ni imani ya Watanzania kwamba viongozi wetu wana dhamira ya dhati katika kuuendeleza Muungano huu kwa vitendo kwa faida ya nchi zetu mbili za Muungano kwa maana ya Zanzibar na Tanzania Bara. Dhamira zao za dhati zilianzia kwa waasisi wa Muungano huu; Marehemu Mheshimiwa Abeid Amani Karume na Marehemu Mzee Nyerere. Hao ndio waasisi. Marais waliofuatia baada yao, akina Mzee Jumbe, Mzee Mkapa, Mzee Ali hassan Mwinyi na mpaka sasa tunaye Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akishirikiana na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni imani yangu kwamba wataendeleza nyayo na mema yote yaliyoanzishwa na waasisi wa Muungano huu kuutekeleza na kuusimamia Muungano huu kwa vitendo kwa maslahi ya wananchi wa Tanzania, maslahi yetu Watanzania na vizazi vijavyo vya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)