Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon Haji Makame Mlenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chwaka

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. HAJI MAKAME MLENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii ya kuwa miongoni mwa wachangiaji katika Ofisi hii ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira. Niseme tu kwamba Muungano huu una tija sana na ndiyo maana leo na sisi tuko hapa tunajilabu na kusema ambayo tunayazungumza kupitia suala hili la Muungano. Katika mchango wangu nitaonyesha faida ambazo nimezipata ndani ya Jimbo langu kupitia suala hili la Muungano, lakini hasa mchango wangu utaenda kuzungumzia suala la mazingira katika upande wa hifadhi hai ya mazingira.

Mheshimiwa Spika, Tanzania tumepata bahati ya kuwa na hifadhi hai zisizopungua sita. Katika hifadhi hai hizi sita ambazo zimetambuliwa na UNESCO kuwa hizi tayari zimeshafikia katika kiwango cha hifadhi hai. Kutokana na ziara ya mama ya uzinduzi wa Royal Tour, hifadhi hizi nina wasiwasi kwamba zinaweza zikazidiwa na wageni. Kwa hiyo niseme tu kabisa kwamba hifadhi hizi tuweze kuziangalia kwa kiwango kikubwa, kwa sababu hizi hifadhi hai tusiweze kupoteza asili ambayo ipo ndani ya hifadhi hizo kwa sababu tutakapopoteza asili ya hifadhi hai, tunaweza kupoteza ile huduma ambayo tunaweza kuitoa kwa wale wageni ambao tunawatarajia watakuja katika kutembelea hifadhi hai hizi.

Mheshimiwa Spika, matarajio yetu makubwa ni kwamba, wageni watakapokuja waweze kupendezwa na hifadhi hai hizi ili wawe na ndoto za kuweza kurudi, lakini pia wakazisimulie vizuri ili kuweza kuongeza tija ya kupata wageni. Hifadhi hai hizi ambazo zipo katika nchi yetu ya Tanzania ikiwemo Ngorongoro, Lake Manyara, Serengeti, East Msambara, Gombe na Jozani Chwaka. Kwa bahati nzuri Hifadhi ya Jozani iko katika eneo la Jimbo la kwangu na imepata bahati ya kusajiliwa toka mwaka 2016, lakini kwa bahati mbaya sana hifadhi hii haijakamilisha utaratibu ambao unaotakiwa na UNESCO ikiwemo uzinduzi wa hifadhi hai.

Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, tarehe 24 na tarehe 25 baada ya kuzungumza, walikuja Zanzibar wakafanya kikao pamoja na Idara ya Mazingira pamoja na Idara ya Misitu na kwa bahati nzuri walinialika nikashiriki katika kikao hicho cha kuweza kuona namna gani tunaondoka katika hatua ile ambayo tulikuwa nayo mwanzo ya kutokufanya uzinduzi, lakini hivi sasa mazungumzo yanaenda ili kuweza kufikia hatua ya uzinduzi.

Mheshimiwa Spika, tarehe 25 tulitembelea katika eneo lile la Jozani ambalo linategemewa kuwa hifadhi hai pale ambapo tutakamilisha utaratibu kama ambavyo umeelezewa. Hata hivyo, namwomba tu kaka yangu Waziri Jafo, najua watu wake wamekuja kumpa habari na wamefanya kazi nzuri, Wizara yake inafanya kazi nzuri, lakini ningefurahi sana hata yeye mwenyewe akawa miongoni mwa watembeaji katika eneo hilo ili tuweze kuona namna gani tunaenda kuitengeneza Jozani ili ifikie katika kiwango kizuri.

Mheshimiwa Spika, wakati niko mdogo nilikuwa kijijini kwangu tunazungumza kwamba msitu hautaweza kumalizika hata siku moja, kwa sababu kweli kulikuwa na msitu ambao ulikuwa wewe mwenyewe unaogopa kutembea, lakini leo hii misitu hii hakuna, misitu ile imebakia katika eneo chache hili la Jozani.

Mheshimiwa Spika, zamani wakati tunatembea, ilikuwa ukienda kazini msituni maana yake unakutana na wanyama tofauti tofauti wakiwemo chui leo chui haonekani, lakini ukirudi mnakaa mnasimuliana, unakuta leo mwenzako anakwambia tumekutana na chui, huyu anakwambia tumekutana na nani, lakini leo hakuna, uoto huu tunautegemea sana katika eneo la Jozani. Naomba tuliangalie sana na Mheshimiwa Waziri basi, naomba siku moja tufuatane twende Jozani.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umekwisha.

MHE. HAJI MAKAME MLENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)