Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Frank George Mwakajoka

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niweze nitoe mchango wangu katika Wizara hii. Awali ya yote niwashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Tunduma, pia niitumie fursa hii kumshukuru sana Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa hotuba nzuri na hotuba ambayo ikifuatwa na Mheshimiwa Nape akiitumia ninajua Tanzania hii itabadilika kwa ajili ya Wizara yake.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa ambayo nataka kuizungumzia siku ya leo ni kuhusiana na matangazo ya TBC kwa wananchi. Jambo hili linasikitisha sana, wananchi wanasikitika sana kwa kuzimiwa matangazo yao ya live ili waweze kuona Wabunge wao wanafanya nini. Tumepata taarifa hapa mara nyingi CCM wanasema wanataka kutukomesha ili umaarufu upungue, tunataka kutoa taarifa katika Bunge hili kwamba tulikotoka ni maarufu na ndiyo maana tuko Bungeni. Kwa hiyo, hatuoni sababu hata moja ambayo tunafikiri CCM watatupunguzia umaarufu, sisi ni maarufu na tutaendelea kuwa maarufu na wao wataendelea kushuka umaarufu kwa sababu wamekuwa waoga kupita kiasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema, tumepata taarifa mbalimbali hapa wanasema gharama ni kubwa, lakini kuna vyombo ambavyo vilijitokeza kwamba wangeweza kutoa matangazo kwa wananchi, jambo la kushangaza ni kwamba pia wamewekewa mgomo na sasa hivi wanafika mahala wanachambua taarifa ambazo siyo sahihi na ambazo hazina umuhimu kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa sana, Mheshimiwa Magufuli wakati anahutubia Bunge hili, alisema kwamba hii ni Serikali ya uwazi, sasa ni Serikali gani ya uwazi ambayo inaweza kufanya uwazi, bila kuweka masuala ya habari na kuweka taarifa hizi live wananchi waweze kusikia. Tunafikiri kama Upinzani tunajua kabisa kwamba Bunge ni chombo muhimu na kikao hiki ni kikao cha bajeti, ni jambo muhimu sana kwa wananchi wetu. Wananchi wanataka kujua wawakilishi wao waliokwenda Bungeni wanasema nini, ni fedha gani zinatengwa kwenda kwenye majimbo yetu na ni kazi gani ambayo Serikali itakwenda kufanya. Hatujaja hapa kuuza sura, kama wanavyosema Wabunge wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukiwauliza Watanzania, ni Waziri gani au ni mtu gani anayechukiwa sana katika nchi hii, watamtaja Mheshimiwa Nape Nnauye, kwa sababu tu ya kuzuia matangazo.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, watamtaja Nape Nnauye kwamba ni mtu ambaye anachukiwa sana katika nchi hii. Ninazungumza haya maneno kwa sababu tumejaribu kuangalia katika mitandao mbalimbali tumeona watu wanavyolalamika, wanavyolaani kitendo hiki na siamini kama Mheshimiwa Nape Nnauye atarudi Bungeni mwaka 2020.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, atang‟olewa tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie jambo lingine ambalo linahusiana na michezo, tusifikirie kama tunaweza tukabadilisha michezo katika nchi hii kama tutaendelea kuendekeza siasa kwenye masuala ya msingi. Masuala ya kitaalam yaende kwenye utaalam, na masuala ya kisiasa yaende kwenye siasa. Leo nchi hii imetekwa na wanasiasa kila jambo linalofanyika wanasiasa ndiyo wao wanalolifanya, hata jambo la kitaalam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hauwezi kupata timu bora ya Taifa, hauwezi kupata timu bora ya mpira kama hutaanzisha shule za vipaji maalum kwa ajili ya michezo, haitawezekana hii itakuwa ni ndoto ya alinacha, hata mngetenga bilioni 100 hapa, hata mngetenga trilioni 10 jambo hili halitaweza kubadilika, tutaendelea kubaki kichwa cha wendawazimu. Brazil ni nchi ambayo inatoa wachezaji wengi sana ambao wanacheza professional, lakini leo bado wanaanzisha shule za vipaji maalumu. Ukienda Ivory Coast, ukienda Ghana, ukienda Nigeria na maeneo mengine, sisi tumekalia siasa tunakaa tunazungumza humu, badala ya kuweka mipango na mikakati mizuri kwa ajili ya kutengeneza ajira za vijana wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tukubaliane kwamba mpira na michezo yoyote ni ajira kwa vijana wetu, tunahangaika ajira wakati tukitengezeza ajira za kuwawezesha vijana wetu kuwajengea viwanja na kujenga shule ambazo zinaweza zikawasaidia wao kuinua vipaji vyao, tutakuwa tumeongeza ajira katika nchi hii, lakini tunakalia siasa, tunafanya siasa hata kwenye masuala ya msingi, nataka nimuulize Waziri, wakati anakuja hapa kujibu maswali haya, anataka kujibu hoja zangu afike ajibu hoja.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wale vijana ambao walikwenda Brazil, wakaenda wakachukua kombe la Coca-Cola wako wapi wale vijana kama kweli Serikali hii ina dhamira ya kweli ya kuendeleza michezo na kuinua vipaji vya watoto na wananchi katika nchi hii. Wale watoto wako wapi, aje atuambie kama ni utaratibu, kama kweli vijana wanaotoka Tanzania wanakwenda kushiriki kombe la Coca-Cola nchini Brazil wanashinda wanakuja na kombe halafu vijana wale Mwaka mmoja wanapotea mpaka leo hawaonekani, leo tumekaa humu tunasema tunataka kutengeneza bajeti, ni bajeti ya aina gani tunayotengeneza ya kuinua michezo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote ni maigizo, ni maigizo ndani ya Bunge hili na lazima Serikali ya Chama cha Mapinduzi iendelee kupokea ushauri na isipoendelea kupokea ushauri tutaikuta ikisuasua mwaka 2020 kwa sababu haitaki kufuata ushauri tunaoutoa katika Bunge letu hili hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninataka kulizungumza hapa ni kuhusiana na wasanii. Leo ukienda kwenye redio zetu na televisheni zetu asilimia 90 ya nyimbo zinazopigwa na kuoneshwa kwenye tv ni wageni ndiyo wanaooneshwa. Tunataka uzalendo wa namna gani, tunataka tuwafundisheje wananchi wetu wapende miziki yetu na kuwathamini wasanii wetu kama hatutaweza kuchukua hatua. Ni lazima Serikali ikae na iangalie ni namna gani itawajengea uzalendo wananchi, kuhakikisha kwamba wanawapenda wasanii wao na wanatumia nafasi ya kujinufaisha kwa kutumia nguvu za wasanii wao.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tufike mahala tukubaliane, kwamba Serikali hii haijajipanga na la lazima ijipange, leo asubuhi nilikuwa najiuliza nasema, hivi kwa bajeti ilivyooneshwa humu katika bajeti hii ambayo imesomwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, nikawa nafikiria nikamuuliza Mheshimiwa Sugu nikasema, hivi kuna siku Nape amewahi kuwa mwanamichezo mpaka amepewa Wizara hii. Maana yake niliona ni maajabu yaliyomo humu, haya ambayo tunayazungumza hakuna hata moja lililoandikwa humu, sasa jambo hili ni la ajabu sana, Waziri unapimwa kutokana na mambo ya msingi ambayo yanaoneshwa humu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kwamba bajeti hii, hata TFF hawajashirikishwa, na ndiyo maana mambo ya msingi ambayo yalikuwa yanatakiwa yahusu mambo ya soka kwenye nchi hii hayaonekani humu. Tunaona tu semina zinakuwa nyingi, semina elekezi zinakuwa nyingi, hatutaweza kwenda huko, ni lazima turudi tuangalie misingi ya kujenga nchi yetu. Haitajengwa nchi hii kwa sababu tu ya kuzungumza na kuja kucheka cheka humu ndani, kuna watu wengine wanasimama humu ndani, amesimama Mheshimiwa Malembeka, anazungumza hapa anasema eti akina mama wamepewa mimba, inawezekana na yeye imegoma mimba, tutajuaje.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanamke yeyote ni wajibu wake kubeba mimba, na hiyo ni mipango ya Mwenyezi Mungu, siyo mipango ya binadamu. Leo anakuja Bungeni badala ya kuchangia hotuba hii, anaanza kuzungumza mambo ambayo hayastahili. Ni lazima Serikali ifike mahala ibadilike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza haya maneno wengine wanasema ukiwa humu huonekani, ukiweka maji kwa wananchi watakukubali, kuweka maji siyo hisani, ni kodi za wananchi. Serikali lazima ifanye hivyo kwa sababu imepewa mamlaka ya kufanya hivyo, na inakusanya kodi za wananchi. Kwa hiyo masuala ya msingi ni lazima tufike mahala tuyajenge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ndugu zangu Watanzania, kwa nini tusijiulize miaka yote Filbert Bayi amestaafu kukimbia, mpaka leo hakuna mchezaji hata mmoja anayewakilisha vizuri nchi yetu huko nje, kwa nini hatujiulizi? Kwa nini tunaendelea kulala usingizi? Kwa sababu tu ya mambo ya kisiasa, tunatoa takwimu za uongo humu, wakati takwimu sahihi hatutaki kuzichukua na tuzifanyie kazi. Kutokana na hali halisi na kichefuchefu nilichonacho, ningeomba kwa kweli niishie hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii.