Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza Serikali, Waziri na watumishi wote kwa kazi nzuri wanazozifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa mchango wangu wa maandishi katika Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora katika maeneo yafuatayo; kwanza mishahara ya watumishi na kupanda madaraja. Kwa muda mrefu sasa Serikali haijaweza kuongeza mishahara kwa watumishi wa umma na kushusha moyo wa kufanya kazi kwa watumishi wengi. Hali ya mfumuko wa bei inaendelea kuathiri maisha ya watumishi wengi. Ili malengo ya Serikali yafikiwe ni muhimu kuangalia uwezekano wa kuongeza mishahara sanjari na mapunjo ya mishahara na madaraja ya baadhi ya watumishi ambao wamefika muda wa kupanda na kupunguza malalamiko ya watumishi wa umma.

Pili ni kuhusu mfumo wa OPRAS nchini; ni wazi kabisa mfumo huu ni muhimu sana kwa maendeleo endelevu, hivyo Serikali ikasimamie na kufanya kazi kwa uwazi na uwajibikaji. Hivi sasa mfumo unaonekana hauna tija kwa kuwa haujasimamiwa vizuri na kutoa matunda tuliyoyatarajia. Ni vizuri iwepo siku ya kutangaza matokeo ya tathimni ya utekelezaji wa mfumo huu kwa mtumishi mmoja mmoja na pia taasisi. Taasisi zifanyike overall performance na kutangazwa matokeo yao hadharani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu ni suala la Serikali mtandao; naipongeza Serikali kwa kuendelea kuimarisha mifumo ya TEHAMA na Serikali mtandao. Lakini kuna haja pia ya kufanya utafiti na tathmini ya mfumo huu unavyofanyakazi ii kupima mafanikio na kubaini changamoto zilizopo ili nchi ipige hatua kubwa.

Nne, mpango wa TASAF; hivi Serikali imefanya tathimini ya mpango huu na kuona haja ya kuendelea na mpango huu? Hivi sasa maeneo mengi wanalipwa watu wasioruhusiwa na walengwa wanabaki nje ya mpango. Naona ipo haja ya kuangalia mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano ni suala la rushwa nchini; sasa hivi rushwa ni kubwa sana katika miradi na zabuni katika maeneo mengi ya nchi yetu. Je, ni mkakati upi hasa ambao umeandaliwa kupunguza rushwa na kujenga nidhamu, uzalendo, uadilifu na uwajibikaji? Katika taasisi nyingi bado hali si shwari kabisa.

Sita ni kuhusu mafunzo kwa viongozi na watumishi wa umma; kwa muda mrefu wa sera ya mafunzo na utekelezaji wake bado ni kitendawili. Mafunzo mpaka sasa yanachukuliwa siyo kitu muhimu. Ni vizuri suala la mafunzo kwa viongozi wa umma, watumishi wa umma lipewe uzito mkubwa. Huko nyuma suala la leadership competence framework iliandaliwa na Chuo cha Utumishi wa Umma lakini hadi leo halijatekelezwa na hakuna mafunzo kwa kuzingatia framework hiyo. Ni vizuri Serikali ikaliangalia vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba masuala hayo hapo juu yaangaliwe na kufanyiwa kazi vizuri ili kujenga misingi ya utawala bora na utumishi uliotukuka.