Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Mohamed Lujuo Monni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hoja hii muhimu ya Waziri wa Utumishi. Kwanza kabisa nachukua fursa hii kumpongeza Waziri mwenyewe, lakini pia kumpongeza Naibu Waziri, Katibu Mkuu na wataalam wote. Kipekee kabisa niwapongeze watumishi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama umewahi kuwa mtumishi kidogo tu unafahamu hali halisi iliyopo huko. Watumishi wa Tanzania wanafanya kazi kwenye mazingira magumu, nami nafahamu watu wengi wamejaribu kuchangia hata chanzo cha kuhama, mimi Jimbo langu ni la vijijini, unaweza ukaenda kwenye zahanati ambayo iko kijijini kabisa lakini unakuta mtoto wa kike ana miaka 23 anafanya kazi huko na yupo huko anafanya kazi vizuri. Kwa hiyo kipekee kabisa niwapongeze watumishi wa Tanzania wanajitolea na wanafahamu hali halisi ya nchi yetu, niwapongeze sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu hapa ni moja tu. Naomba niendelee kuongelea kuhusu changamoto ya upungufu wa watumishi tulionayo. Hili tatizo ni la Kitaifa, lakini naomba nitoe mfano kwa Wilaya ya Chemba na hasa kwa watumishi wa afya. Nilimsikia Daktari Chaya, jirani yangu Manyoni yeye ameongeza watumishi wa afya, angalau yeye anafika asilimia 50. Mimi kwenye Kada ya Afya nina asilimia 27 tu. Mahitaji ya watumishi kwa ujumla ya Kada ya Afya ni 838, lakini tulionao ni 173, sawasawa na asilimia 22 tu. Mnaweza mkafikiria ni kwa namna gani sasa unaweza kuhudumia hawa watu wetu walioko huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme maneno kadhaa, sisi tuna vituo vya Afya vinne, tuna kituo cha Afya kipya sasa hivi ambacho tumejengewa na KOICA kipya kabisa ambacho kimejengwa kama Hospitali ya Wilaya. Hata hivyo, hivi tunavyoongea hakina mtumishi hata mmoja na hatuwezi kukifungua kwa sababu hakuna watumishi, lakini tumejengewa na wafadhili. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, kituo hicho kipo kule Soya na katika maeneo ambayo tulifanya vibaya kwenye kura ilikuwa ni kwa sababu hiyo. Tukaenda kutafuta Mfadhili huko akatoa bilioni 1.2 amejenga Kituo cha Afya. Kituo cha Afya kipo tayari na wamenunua kila kitu na vifaa, lakini hakuna watumishi, hakuna namna ambavyo tunaweza kukiendesha kile Kituo cha Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Waziri wa Utumishi lakini pia nimwombe Waziri rafiki yangu Mheshimiwa Bashungwa pale aangalie kwenye watumishi hawa wanaoajiriwa, watupelekee kule. Hospitali ya Wilaya ipo tayari, lakini nataka niwaambieni Wilaya ya Chemba hakuna Daktari wa Meno hata mmoja, yaani wilaya nzima pamoja na kuwa tuna Vituo vya Afya vinne, tuna Hospitali ya Wilaya, tuna Vituo vya Afya viwili ambavyo viko tayari havina Madaktari, lakini Wilaya nzima ukitaka kwenda kutibiwa meno lazima uende Kondoa au lazima uje Dodoma. Niwaombe sana, niwaombeni sana hawa wanaowaajiri angalieni sana Wilaya ya Chemba. Ni kweli Wilaya ya Chemba ilikuwa sehemu ya Kondoa, sasa kila kitu kipo lakini watumishi hatuna. Nataka niombe hili lizingatiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili na la muhimu sana, tuangalie juu ya ikama ya uwiano, yaani unaweza ukashangaa sana kwamba hizi Wilaya zingine sijui ziko wapi. Utakuta wakati Wilaya ya Chemba ina asilimia 22 ya Watumishi wa Kada ya Afya, zipo Wilaya zina asilimia 88, sasa hii haiwezi kuwa sawa hii, yaani Tanzania hii Wilaya moja ina asilimia 22, Wilaya nyingine ina asilimia 87 na watumishi hao hao wanaajiriwa na Serikali, hii haiwezi kuwa sawa. Ni lazima tuangalie njia nzuri ambayo walau tutagawana watumishi hawa pamoja na kuwa kuna upungufu kila mmoja apate walau kwa kiwango kile ambacho kinastahili. Hilo lilikuwa la muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, sina mambo mengi, nafahamu kuna shida kwenye Kada ya Elimu lakini angalau kwenye Kada ya Elimu tuko asilimia 49, upungufu uliyopo ni kama asilimia kama 51, hivyo tuangalieni huku ambako Wilaya zetu zimeanzishwa juzi juzi na Wilaya za vijijini na ni ukweli kwamba wakati mwingine unaweza ukashangaa sana wanasoma taarifa za namna gani kwenye Afya Wilaya fulani imefanya, halafu unalinganisha Wilaya ambayo ina asilimia 22 ya watumishi unailinganisha na Wilaya ambayo ina asilimia…

MWENYEKITI: Weka mic yako vizuri Mheshimiwa Mbunge.

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nasema kwamba, unataka kulinganisha wilaya hiyo na wilaya ambayo kimsingi haina watumishi wa afya wala watumishi wa elimu. Niwaombe sana sana, nimesimama hapa kwa ajili ya ombi hilo maalum Kituo cha Afya Soya ambacho tayari kimekamilika, kimejengwa na wafadhili wa KOICA, watuletee watumishi wa afya ili hospitali ile ifunguliwe na tulishamwomba na Waziri Mkuu aje aifungue. Sasa anafunguaje wakati hakuna hata Daktari mmoja. Pia tumeshawatumia database kule TAMISEMI wanafahamu kwamba kuna idara ambazo kabisa hatuna Madaktari kama nilivyosema Idara ya Meno. Niwaombe sana, waliangalie hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)