Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia kusimama mbele ya Bunge lako tukufu siku ya leo ya Ijumaa ili niweze kuchangia bajeti ya Ofisi ya Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nitangulize shukrani za dhati sana kwako wewe. Pili, naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kwa Watanzania ya kuwaletea maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, dada yetu Mhagama, kwa kazi kubwa na Naibu Waziri, hali kadhalika Katibu Mkuu na watumishi wote wa Ofisi hii, kwa sababu ofisi hii ndiyo jicho na tegemeo la watumishi wote wa Tanzania, wanafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, ningependa kujielekeza kwenye maeneo ambayo ni kama ushauri. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri katika maeneo mbalimbali alijitokeza na katika hotuba yake amezungumzia kwamba kuna umuhimu wa kufanya ukaguzi au auditing ya watumishi. Ni ukweli usiopingika kwamba hitaji la watumishi katika maeneo mbalimbali nchini ni kubwa sana, lakini ni ukweli pia usiopingika kwamba watumishi hawa kwa hakika bado hawajawekwa vizuri, kwa sababu kuna maeneo ambayo wapo watumishi wengi ukilinganisha na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajenga vituo vya afya, tunajenga shule za sekondari, tunajenga shule shikizi na zote hizi zinahitaji watumishi. Bila kufanya auditing ya kutosha, itafikia wakati haya majengo yote yatakuwa kama ni white elephant. Kwa hiyo, jambo la kwanza kabla hatujafikiria kwenda kwenye kuongeza watumishi kwa sababu lazima tukubali Wabunge wote kwamba bajeti yetu haiwezi kutosheleza kuweza kuwaajiri watanzania wote. Kwa hiyo, hatua ya kwanza ni kufanya auditing ya kutosha. Hebu leo tuchukulie mfano kuna Maafisa Ugani Kinondoni au Ilala wanafanya kazi gani? Wakati katika majimbo ya vijijini hakuna Afisa Ugani. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri jambo hili lina umuhimu mkubwa sana sana kufanya auditing na auditing ndiyo itakayosaidia kuhakikisha kwamba watumishi hawa wanaenda kutatua changamoto ya ajira kwenye maeneo yetu huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, naomba nizungumzie suala la kukaimu. Suala la kukaimu imekuwa ni changamoto kubwa sana. Kwenye vikao vyetu unakuta Kaimu Mkurugenzi, Kaimu Mtendaji, kwa nini iwe hivyo? Kuna kitu kinaitwa Tange katika utumishi wa Serikali. Tange ndiyo inayoonyesha seniority ya watumishi ameanza kazi lini, ana elimu gani, tange hii haifanyi kazi? Hii ndiyo ambayo inaenda kutatua changamoto ya promotion. Unapomweka mtumishi kwenye nafasi ya kukaimu miezi sita, mwaka mmoja humtendei haki hata mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii sisi ambao tuliofanya kazi Serikalini miaka ya nyuma huko, kulikuwa na utaratibu nadhani utaratibu huu bado unaendelea kufanya kazi, kitu kinaitwa succession plan. Leo Katibu Mkuu anapokaribia kustaafu anajua yupo Naibu Katibu Mkuu, anajua yupo Mkurugenzi watu hawa wanaijua taasisi vizuri, kwa nini uende ukamkaimishe mtu kutoka eneo lingine wakati institution memory ya taasisi hiyo wapo watu wanayoielewa. Kwa kiasi kikubwa hii inadhoofisha utendaji wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba turudi kwenye historia, turudi kwenye utaratibu, kwa sababu mtu kafanya kazi miaka 20 au 25 unaenda kumtoa mtu eneo lingine hata kuandika dokezo hawezi, hili jambo halina afya hata kidogo katika utendaji wa Serikali. Nakuomba Mheshimiwa Waziri, twende turudi kwenye utaratibu huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, wapo watu mnapokuwa mnawateua kwenye baadhi ya mashirika wanawaondoa watumishi, wanaondoa watumishi takribani 30 mpaka 40 halafu analeta tena kibali cha kuomba kuajiri watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, hawa watu wanaoteuliwa na Mheshimiwa Rais wanapokuwa wanaondoa watumishi kuwapeleka maeneo mbalimbali, asitoe kibali cha kuajiri tena kwa sababu watumishi wale wengine ni very senior, hili jambo halina afya hata kidogo na hili jambo Mheshimiwa Waziri kwa kweli….

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge nimeona umesimama.

T A A R I F A

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti,…

MWENYEKITI: Ni kanuni gani Mheshimiwa.

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, 77(1) nataka kumpa taarifa mzungumzaji kwamba wapo wanaokaimu zaidi ya miaka miwili, mitatu mpaka minne na kinachotokea ni kwamba anakuja kuletwa mtu mwingine kuthibitishwa kuwa Mkuu wa ile Idara. Kwa hiyo wanawaacha hawa watu wakiwa na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo sonona, pressure na magonjwa mengine. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kigua unapokea taarifa ya Mheshimiwa Amandus.

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru na nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge anachozungumza ni sahihi na jambo hili halitoi motivation kwa watumishi wetu…

MWENYEKITI: Unapokea taarifa.

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa.

MWENYEKITI: Ahsante, endelea.

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kusema kwamba, dhana hii kwa kweli si dhana nzuri, tuendelee kuwaamini watumishi wetu, watumishi ambao wanafanya kazi kwa weledi mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine katika eneo langu la Jimbo la Kilindi, wapo watendaji ambao ni darasa la saba ambao wamefanya takribani miaka 20 sasa hivi, lakini watumishi hawa wapo baadhi yao ambao wamestaafu lakini hawajapata pension kwa sababu wamekosa sifa. Sasa fikiria Mtanzania huyu ambaye ulimwambia afanye kazi za utendaji wa kijiji na hivi ninavyozungumza ni kwamba watumishi hawa tayari Mkurugenzi wa Halmashauri wa Jimbo la Kilindi alikwishaleta barua Ofisi ya Rais, Utumishi miezi sita hawajatoa majibu, wengine wanakaribia kustaafu hawapati pension, tunatoa ujumbe gani kwa Watanzania? Naomba sana Mheshimiwa Waziri jambo hili liweze kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, tuangalie namna ya kuwapa motivation watumishi wetu, motivation siyo cheo tu au motivation siyo fedha tu, hata wakati mwingine mtumishi anapofanya vizuri unamwandikia barua ya reward ya kumshukuru kwamba kafanya kazi vizuri hiyo ni njia moja ya kum-reward. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja hii. Nakushukuru sana. (Makofi)