Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ningependa kwa dhati kabisa kwanza nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya katika kuleta maendeleo kwenye Taifa letu. Leo hii niseme kwa dhati kabisa, nimefarijika sana; kwa sababu moja tu, Bunge lililopita nilijenga hoja kwa habari ya jambo la OPRAS. Nilieleza mapungufu ya OPRAS; na nikaainisha mapungufu yote ya OPRAS na leo hii nasema nimefarijika kwa sababu Serikali Serikali hii ni sikivu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hii ni sikivu kwa maana na nampongeza kwa dhati Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Wizara ya Utumishi na Utawala Bora; amekwenda muda mfupi tu mama yangu huyu, muda mfupi tu, lakini tunaona Wizara inakuja na mabadiliko chanya kwa Taifa hili. Sasa kwa sababu hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, nampongeza pia Naibu Waziri, lakini nampongeza na Katibu Mkuu Dkt. Ndumbaro, Mwalimu wangu kwa kweli kazi kubwa inafanywa na ni nzuri kwenye Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze kwenye mchango wangu. Katika hoja yangu niliyoieleza hapo kuhusu OPRAS, wizara au Serikali imekuja sasa na mpango bora kabisa katika upimaji wa utendaji kazi wa Taasisi za Umma ambao naamini unakwenda kuweka tija kwa Taifa letu. Kwanza wamekuja na Mfumo wa PEPMIS (Public Employees Performance Management Information System, mfumo huu ni mfumo ambao unakwenda kuwa mbadala wa OPRAS kwa maana ya kila mtumishi mmoja mmoja anakwenda kupimwa sasa, lakini haitoshi siyo tena kujaza makaratasi, sasa hivi ni mtandao. Kwa hiyo, tunaona watumishi wanakwenda kutendewa haki lakini watawajibika pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine wamekuja na mfumo mwingine wa PIPMIS (Public Institutions Performance Management Information System). Mfumo huu, ni mfumo ambao unakwenda kuweka makubaliano baina ya Serikali na Taasisi zake. Jambo hili ni jema ndiyo maana nimesema nimefarijika sana siku ya leo. Sasa katika hili, nimeona nitoe maoni angalau mawili, ni jambo jema lakini nami niboreshe kidogo kwenye maeneo mawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, mifumo hii yote miwili imetajwa kwa Kada ya Viongozi wa Kisera. Sasa Viongozi wa Kisera hawa ni kuanzia level ya Wizara, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na kadhalika. Sasa nashauri jambo moja, nashauri kwenye maboresho hayo hayo tuje na KPI, tuongeze KPI. KPI kwa maana ya Key Performance Indicators. Key Performance Indicators ni viashiria muhimu vya utendaji kazi; sasa hivi vitatusaidia hawa Wakuu wa Taasisi kwa mfano; Waziri lazima awe na Key Performance Indicators, kwa sababu tuna Mpango Mkakati wa Miaka Mitano na tuna Mpango Kazi wa Mwaka Mmoja. Tukimpa Waziri kwa mfano, Waziri wa TAMISEMI, akapewa Key Performance Indicators za Mpango Kazi wa Mwaka mmoja alionao, kupitia Mpango Mkakati wa Miaka Mitano, anaweza kupimwa vizuri na Mheshimiwa Rais kuliko kuangalia sasa Vyombo vya Habari kama anakwenda ziara na nini, hii itasaidia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika kwenye maeneo haya wasimamizi wa Taasisi kwa maana ya viongozi wa kada za utendaji nao wapewe key performance Indicators. Wakurugenzi wa Halmashauri Key Performance Indicators, twende kwenye level ya ma-CEO wa Makampuni au Mashirika ya Umma key performance Indicators; ndani ya mwaka mmoja atatuletea mpango kazi wake na tutampima kupitia mpango kazi aliotulewa na mwisho wa mwaka atueleze kama ame-perform kwa kiwango gani, kama kuna mapungufu aeleze. Mamlaka ya Nidhamu itakuwa sasa na uwezo wa kutathmini kwamba huyu amefeli kwa sababu hatukum-finance au kwa sababu kitendea kazi au rasilimali fedha, amefeli kwa sababu ya uwezo wake. Mwisho wa siku watu wa-vacate ofisi wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa dhati kabisa hii inakwenda kumsaidia Mheshimiwa Rais na nasema kwa dhati. Mheshimiwa Rais sasa hata kuwa na kazi ya kutafuta nani anafanya vizuri na hafanyi vizuri. Nampongeza tena Mheshimiwa Waziri, Mama yangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nimesikia kidogo kwamba baadaye tutakwenda biometric, nadhani tusiishie tu hapo. Nilipokuwa hapa Dodoma Mkurugenzi wa Jiji nilianzisha mfumo mmoja, nilifunga camera ofisi zangu zote, kwa hiyo ilikuwa nikikaa ofisini naangalia Idara ya Ardhi nikiwa ofisini, nikiwa kwenye mkutano, nikiwa kwenye kikao chochote namwona mtumishi kwenye ofisi kama anamhudumia mwananchi au anafanya mambo mengine ambayo siyo kwa shughuli zake za kila siku. Kwa hiyo, nilikuwa na uwezo wa ku-detect kila mtumishi, popote nitakapokwenda, nikiwa nakunywa chai naangalia simu yangu, ofisi yangu ipo hapa. Ndiyo siri ya mafanikio hapa Dodoma! (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisipoteze sana muda, leo hii nimefarijika sana, naunga mkono hoja na Mungu awabariki watu wa Wizara. (Makofi)