Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Nicholaus George Ngassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kufungua dimba mchana huu wa kuchangia Hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unapoongelea masuala ya Utumishi wa Umma nchini na unapoongelea masuala ya Utawala Bora wasaidizi Namba Moja wa Mheshimiwa Rais ni hizi Ofisi mbili, Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Hawa ndiyo custodian wa mambo yote yanayohusu utawala wa nchi yetu, ndiyo custodian wa mambo yote yanayohusu Utumishi wa Umma, pia ndiyo custodian wa nyaraka zote za Serikali katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mantiki hiyo nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Jenista Mhagama Dada yetu kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Waziri wa hii Wizara. Lakini pia nimpongeze Kaka yetu Deo Ndejembi kwa kuwa Naibu Waziri.

Nimpongeze Mwalimu wangu Daktari Ndumbalo kwa kuendelea kuaminiwa kuwa Katibu Mkuu wa hii Wizara. Pia nimpongeze Xavier Daudi ambaye kwa sasa ni Naibu Katibu Mkuu wa hii Wizara ambae alikuwa ni Mtendaji Mkuu wa Sekretarieti ya Ajira wakati na mimi naingia Serikalini mwaka 2011. Tunawatakia kheri katika kazi zenu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchana huu nitachangia mambo matano ambayo ni mawazo yangu na ushauri na mapendekezo kwa Serikali ambayo naamini yatakuwa na mchango mkubwa katika kuboresha suala la Utumishi wa Umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ni mfumo wa kuomba ajira Serikalini. Tuna huu mfumo unaitwa online application portal ambao uko chini ya Sekretarieti ya Ajira. Kwa sasa tunavyo Vyuo Vikuu vingi nchini kwetu lakini pia vinatoa kozi na mafunzo mbalimbali. Mfumo wetu kwa sasa bado unawanyima haki baadhi ya Watanzania katika kuomba maombi ya kazi. Unakuta watu wamesoma kozi hapa nchini au nje ya nchi lakini wanapofika hatua ya kuomba maombi ya kazi unakuta kozi kwenye huu mfumo wetu wa kuomba kazi haupo. Naomba Mheshimiwa Waziri na Wasaidizi wako mkalifanyie hili ili kufungua wigo wa Watanzania wengi kuweza kuomba ajira zinazotolewa na Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo jingine katika mfumo huu ambalo linaonesha udhaifu wake ni wanapoandaa usaili wa waomba ajira. Unakuta wamesema tunahitaji watu wenye kozi zifuatazo, labda wanasema Business Administration, wanasema Economics and other related courses wale watu wanapoomba wakifika kwenye usahili wale watu walio-apply kwa kutumia other related courses siku ya usahili wanatolewa nje wanaambiwa kwamba kozi uliyoomba haihusiani na ajira uliyoomba.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ilitokea sana kwa watu wengi walipoomba kazi za TRA hivi karibuni walipofanya usaili. Mheshimiwa Waziri na Wasaidizi wako tunaomba pia mkalifanyie kazi hili jambo. Mfumo ufunguliwe, baadhi ya selection ziwe hata ikiwezekana mfumo uwe wa kuandika. Sasa hivi dunia ni ya sayansi na teknolojia watu wengi wamehitimu vyuo vikuu, wengine wamehitimu nje ya nchi. Kwa hiyo unapokuwa na mfumo unapokuwa na zile kozi ambazo ni common tu zinazotolewa na vyuo vya nchini, matokeo yake unajikuta watanzania wengi tunawaacha nje katika mfumo huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambao ningependa kuchangia mchana huu ni suala la Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mamlaka na Wakala kuendelea Kukaimu zaidi ya miezi sita. Mheshimiwa Waziri ukifanya utafiti, ukifanya screening katika Wizara, Idara na Mamlaka za Serikali, utakuwa bado kuna Watendaji Wakuu au Wakuu wa Idara au Wakurugenzi Wakuu bado wanakaimu na Kanuni zetu za kudumu za Utumishi wa Umma Toleo la 2009 zimeweka ukomo wa miezi sita, baada ya pale vetting inakamilika, mapendekezo yanakwenda kwenye mamlaka ya uteuzi kwa kupitia Wizara husika lakini kwa kuwa ninyi ndiyo Wizara kiongozi ni kama kiranja wa Wizara zingine kwa maana ya kwamba mna-deal moja kwa moja na mna-link moja kwa moja na Ofisi Namba Moja ya Ikulu kwa maana Ofisi Kuu ya Nchi. Kwa hiyo, tunawashauri jambo hili la upekuzi lisiwe kisingizio au kichaka cha kuchelewesha watu kuthibitishwa kazini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wanaokaimu zaidi ya miezi sita ni kinyume cha Kanuni za Utumishi wa Umma, ni kinyume cha Sheria ya Utumishi wa Umma wa nchi yetu. Tunaomba hili Mheshimiwa Waziri wewe Dada yetu ni msikivu utalisimamia vizuri na wale wenye sifa waendelee kuthibitishwa na waweze kuwa-full katika nafasi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ambalo ningependa kulichangia mchana huu ni suala la Watumishi wa Umma wanaojisomesha mafunzo ya muda mrefu. Mafunzo ya muda mrefu ni kama vile tunasema mtu amesoma digrii ya Kwanza, aliajiriwa akiwa na diploma ameenda kusoma digrii ya Kwanza amejiendeleza au alikuwa na digrii ya kwanza ameenda kusoma digrii ya pili, wanaporudi kazini kumekuwa na urasimu mkubwa sana katika kuwabadilisha madaraja lakini pia kuwabadilisha kada. Kwa mfano, kama mtu anahitaji kufanyiwa re-categorization unakuta mtu alikuwa ni Katibu Muhtasi ameenda kusoma amepata degree ya Human Resource tuchukulie mfano rasilimaliwatu anatakiwa aje afanyiwe re- categorization awe Human Resource Officer lakini mpaka aje afike hiyo hatua atasugua sana miguu, atapambana sana na mabosi matokeo yake ni urasimu mtupu na inatengeneza mazingira ya rushwa katika Ofisi za Umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Wizara mlisimamie hili jambo wale wanaostahili mpaka Mtendaji Mkuu au Mamlaka ya Ajira inapotoa kibali cha mtu kwenda kusoma maana yake imeshajiandaa. Sasa unapotoa kibali mtu akirudi kazini unaanza kumfanyia urasimu tunakuwa hatuwatendei haki Watumishi wa Umma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la Nne ni suala la mikataba ya huduma kwa mteja. Maboresho katika Civil Service ambayo yalianza miaka ya 1995 wakati huo Katibu Mkuu Kiongozi alikuwa Martin Lumbanga, yalikuja na mapendekezo mengi ikiwepo suala la kuanzisha Client Service Chatter mikataba ya huduma kwa mteja. Sasa lengo hapa ni kuhakikisha mteja kwa maana ya kwamba ama Mtumishi ndani ya Taasisi au mteja anayetoka nje ya Taasisi kupata huduma ya viwango lakini kwa wakati, tunaomba hili Mheshimiwa Waziri mlisimamie.

Mheshimiwa Naibu Spika, kila Taasisi ihakikishe wana mkataba kwa mteja na ioneshe huduma inayotoa, mteja atatumia siku ngapi kuipata. Kama akiwa anatakiwa kulipa malipo ya awali au amekamilisha maombi, application aambiwe siku 14 kama ni umeme utafungiwa ili kuwe hakuna ujanja ujanja wa kutafuta link na connection. Kama ni suala labda Mfumo wa Jamii au Hifadhi ya Jamii ukikabidhi maombi yako ndani ya miezi mitatu umepata fedha zako. Hii itasaidia sana kutoa malalamiko, itasaidia kutoa usumbufu kwa Waheshimiwa Wabunge katika kuhakikisha wanafuatilia mambo mbalimbali ambayo tu ni mfumo ungewekwa na yangekuwa yamerahisishwa katika kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo jingine la tano na la mwisho ambalo ningependa kulichangia mchana huu ni suala la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. Katika historia ya nchi yetu mwaka 1984 Serikali ya kwanza ya Mwalimu Nyerere ilileta Bill of Rights humu Bungeni. Ndiyo ikawa msingi wakuwa na haki za binadamu katika Taifa letu na zikaingizwa katika hii Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Ibara ya 129 na Ibara ya 130 imeeleza majukumu ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, kwa ridhaa yako ningeomba ninukuu mambo mawili ama matatu ambayo ningependa niyachangie kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma Ibara ya 130 Sehemu ya Kwanza, majukumu ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. Jukumu Na. (b) Kufanya shughuli za kupokea malalamiko ya uvunjifu wa haki za binadamu kwa ujumla, kufanya uchunguzi juu ya mambo yanayohusu haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora, kufanya utafiti, kutoa na kueneza nchini elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu na utawala bora na ikibidi kufungua mashauri mahakamani ili kuzuia vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu na kurekebisha haki inayotokana na kuvunjwa huko kwa haki za binadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba nichangie kwa kifupi. Hii Tume yetu ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa sasa Mheshimiwa Waziri kama vile bado imelala. Tunaomba muende mkawaamshe kidogo hususani kwenye suala la kutoa elimu ya haki za binadamu na utawala bora kwa Watanzania. Mfano mzuri, ninyi chini ya ofisi yenu mnayo TAKUKURU. TAKUKURU wanajitahidi sana kutoa elimu kwa wananchi, wana vipindi kwenye Vyombo vya Habari, wanakwenda mpaka kwenye ma-group ya WhatsApp na hii mkiifanya tume ya haki za binadamu mfanye vizuri ndiyo itakuwa shock absorber mtapunguza hata yale maswali Mheshimiwa Rais yuko sehemu ana ziara unakutana na mabango ya wananchi wanalalamika. Unakuta Mheshimiwa Rais yuko amealikwa kwenye sherehe za siku ya Mahakama au siku ya Sheria Duniani, Mama au Baba anatoka na bango amedhulumiwa haki zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii Tume itasaidia sana kupunguza migogoro, itasaidia kupunguza manung’uniko ya wananchi lakini kiujumla itawasaidia nyinyi Watendaji wa Serikali ndiyo maana composition yake imewekwa watu ambao wana weledi pia hata upatikanaji wao imeshirikisha vyombo vikubwa vya nchi, lengi likiwa ni kuweka watu ambao ni credible wataisaidia Serikali, watamsaidia Mheshimiwa Rais na watawasaidia ninyi katika uendeshaji wa kazi zenu za kila siku na kuzipunguzia taasisi nyingine shughuli kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, waamsheni, waambieni waingie field hawa siyo Criminal Investigation Department hawa ni ombudsmen hawa ni watchdog wa Serikali, watawasaidia na tutasonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naunga mkono hoja. (Makofi)