Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nami niungane alipoishia Kaka yangu Profesa Kitila Mkumbo, ni kweli kuna uhitaji mkubwa wa watumishi katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano tu kwenye Halmashauri ya Mji wa Bunda, tuna upungufu wa watumishi zaidi ya 900, Halmashauri moja tu ya Mji wa Bunda. Sasa ukija Watendaji wa Mitaa wapo 38 mahitaji ni 80, upungufu 50. Ukija Walimu wa Msingi, mahitaji ni Watumishi 1,252, Watumishi waliopo ni 738, pungufu ni 514. Ukija Maafisa Ugani Kilimo mahitaji ni Watumishi 48, Watumishi waliopo ni 34, pungufu 14. Watumishi wa Afya mahitaji ni Watumishi 402, Watumishi waliopo ni 184, pungufu ni 218.

Mheshimiwa Spika, katika upande wa watalaam wa ujenzi mahitaji ya watumishi ni Tisa, waliopo ni watumishi watatu kwa Halmashauri moja tu ya Mji. Ukija Watendaji, Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Kata mahitaji ni 14 tunae Mmoja tu, Halmashauri ya Mji hiyo. Ukija Walimu wa Sayansi Na Hisabati; mahitaji 162 waliopo ni Walimu 88 na pungufu ni Walimu 74. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge hiyo ni Halmashauri moja Halmashauri ya Mji wa Bunda. Halmashauri imepata hati safi kwa uchache wa hao watumishi imagine mkitupa watumishi wa kutosha Mheshimiwa Jenista Dada Mkubwa mtupe wote 900 Mji wetu wa Bunda utakuwa kwenye hali gani? Tunahitaji watumishi wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri, nimesoma ukurasa kuanzia 55 nimeusoma vizuri, 52 mpaka 55, ukurasa wa 105 mpaka ukurasa wa 108 nina maslahi hapa. Mheshimiwa Waziri amezungumzia kulipa Shilingi Bilioni 91 ya malimbikizo ya madeni ya Watumishi wa mishahara 65,000 malimbikizo ya madeni ya mishahara kwa watumishi 65,000 Shilingi Bilioni 91.

Mheshimiwa Spika, ukisoma ripoti ya CAG yaani hii mpya latest Machi, 2022, watumishi wanawadai Shilingi Bilioni 430 ya malimbikizo ya muda mrefu, siyo mishahara peke yake kuna malimbikizo ya mishahara ya watumishi wapya, kuna malimbikizo ya watu waliopandishwa madaraja na posho za watumishi, lakini hapa mmelipa Shilingi Bilioni 91 peke yake, bado mnadaiwa Shilingi Bilioni 399 mnazilipa lini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona hapa mmetenga Bilioni 103, kutenga ni jambo lingine kulipa jambo lingine na hata hili mkifanikisha kulipa bado mtakuwa mnadaiwa Shilingi Bilioni 236. Je, mtazilipa lini? Siyo sawa Serikali kuendelea kudaiwa malimbikizo ya Watumishi ambayo ni haki yao ya msingi.

Mheshimiwa Spika, kwa mtindo huu ukiangalia unakuta mtumishi anaanza kuidai Serikali alipoajiriwa tu ana malimbikizo ya mshahara, haya akipandishwa madaraja bado lile daraja alilopandishwa haliendani na mshahara anaotakiwa kulipwa, bado ana malimbikizo. Haya, imefika tena kustaafu bado anaweza akaa miaka 20 hajalipwa kisa utaratibu wa mafao haujafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dada yangu Mheshimiwa Waziri naomba unisikilize hilo nimesema la madeni, bado wastaafu wetu wanacheleweshwa kulipwa mafao yao. Ukiuliza sababu ni kwamba majalada yao maandalizi ya mafao hayajafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe mfano mpaka tunavyoongea kwenye taarifa mpya ya CAG majalada 571 hayajafanyiwa kazi, kuanzia mwaka wa kwanza mpaka wa 28. Mstaafu amestaafu waliokaa miaka mitatu ambao hawajalipwa ni 391. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kaanza kwenye stress za kucheleweshewa mshahara, kulundikiwa malimbizo anakutana nayo tena huku kwenye kulipwa kiinua mgongo chake, siyo sawa kwa watumishi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, waliokaa miaka mitano hawajalipwa mafao yao baada ya kustaafu wako 59. Waliokaa Miaka Kumi ni Wastaafu 54. Miaka 20 wapo Wastaafu 17. Waliokaa miaka 15 ni Wastaafu 25. Waliokaa miaka 25 ni Wastaafu 18, Waliokaa miaka 28 ni Wastaafu Saba, jumla ni Wastaafu 571 ya wastaafu wa Taifa hili waliotumikia Taifa lao kwa jasho na damu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa huku hatuwapandishii mishahara, tukiwapandisha madaraja malimbikizo lukuki, tukiwaajiri malimbikizo lukuki, Serikali mnaanza kudaiwa na wafanyakazi wanapoajiriwa, wanapopandishwa madaraja na wanapostaafu hamuwalipi kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri naomba sana tuwatende haki wafanyakazi na watumishi wa Taifa hili ambao wanatumikia Taifa hili kwa jasho na damu na hawalalamiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa kuna kipindi wamekaa miaka Mitano hawajapandishwa mishahara wapo tu wanalijenga Taifa lao. Sasa Mheshimiwa Waziri hapa nimelizungumzia bado taasisi zako kuna taasisi 15 na Mheshimiwa Spika nakupongeza, taasisi yako inapeleka michango wengine hampeleki. Nitolee mfano shirika la reli haijapeleka michango ya watumishi Shilingi Bilioni 99. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Maji ndiyo wamekuwa sugu maana hata penalty hawalipi wanadaiwa penalty huko Shilingi Milioni 441 hawajapeleka. TRA wakusanya mapato pelekeni michango ya wafanyakazi. Bodi ya Mikopo, Mfuko wa Bima, nitaje na wengine?

WABUNGE FULANI: Taja! (Makofi)

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, pelekeni michango ya watumishi kwa mujibu wa Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Serikali ndiyo wasimamizi lakini taasisi zenu zinaongoza kutopeleka michango na hii ina athari kwenye kiinua mgongo cha watumishi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine ninyi ndiyo mnachangia hii mifuko kufa, tuliwaomba hapa actuarial valuation hamjaleta, sasa CAG ameamua kufanya kwa mlango wa nyuma. Kwenye ripoti ya mwaka huu kwa mujibu wa Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2018 inasema mifuko walau iwe na ukwasi wa asilimia 40.

Mheshimiwa Spika, PSSSF, mfuko ambao ndiyo unaosaidia Watumishi wa Umma una ukwasi wa asilimia 22. Mlivyolipa kale kahela Shilingi Trilioni Mbili kwa hati fungani, kidogo ndiyo kamesaidia imefika asilimia 30 lakini bado ni chini ya sheria inavyotaka. Sasa nauliza na CAG amependekeza Shilingi Trilioni 2.45 iliyobaki mnailipa lini ili kuokoa huu Mfuko?

Mheshimiwa Spika, hii ni 399 bado ya madeni mengine. Sasa mkiangalia mzizi wote ninyi ndiyo mnatengeneza tatizo, ninyi ndiyo mnatupa ahadi hapa na bado hamtekelezi kwa wakati na bado wafanyakazi mfuko wao una hali mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi mnawezaje kupata guts za kuwahamasisha sekta binafsi wapeleki michango wakati ninyi wenyewe hampeleki michango? Ninyi wenyewe hamlipi madeni. Sasa huu ni mfuko wa wafanyakazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu NSSF mna madeni sugu ya Shilingi Trilioni 1.5 Serikali hamjapeleka, Mheshimiwa Waziri naomba tuilinde hii mifuko tutimize wajibu wetu, tusaidie wafanyakazi wetu, please!

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi).