Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Janejelly Ntate James

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Spika, ahsante; na mimi nimshukuru Mwenyezi Mungu kupata nafasi ya kuchangia kwenye bajeti ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Pia nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye alimwongoza Mheshimiwa Rais na kutuletea Jenista Mhagama kuwa Waziri wa Utumishi. Nasema hivyo nina maana gani, Mheshimiwa Jenista tumekuwa naye kwenye vyama vya wafanyakazi, lakini masuala mengi tulikuwa tukimwambia anasema lazima nishauriane na Waziri wa Utumishi, na sasa amepewa mtoto alee mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nifikishe salamu za watumishi wa Tanzania wakimpongeza Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan. Wanampongeza kwa sababu gani; kwa mwaka mmoja ametoa Shilingi bilioni 300 ili watumishi wapandishwe madaraja, ametoa Shilingi bilioni 23 ili watumishi walipwe malimbikizo ya mishahara yao. Amepunguza kodi kutoka asilimia tisa kwenda nane. lakini kwenye mfuko wa jamii amepeleka Trilioni 2.17 ili wastaafu walipwe. Hakika amejipambanua kwamba yeye maono yake ni kuendeleza maslahi watumishi wa Tanzania, Mungu ambariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwa msingi huu leo nitashauri, na ninajua Mheshimiwa Jenista haya utayachukua na utayafanyia kazi nakuamini. Ushauri wangu ni kwenye upandishwaji wa madaraja kwa watumishi. Mmesema mtaendelea na zoezi la kupandisha madaraja watumishi wa Tanzania lakini upandishwaji huu una mambo matatu yote yanaongelea kupandishwa watumishi.

Mheshimiwa Spika, kuna Public Service Act Part II 6 (a) inaongelea upandishwaji wa madaraja na ujazaji wa nafasi zilizo wazi, imetaja vigezo kabisa. Lakini mwongozo wa 2013 unaendana na Public Service Act. Sasa, kuna mwongozo wa mwaka 2019, huu ndio ulikuja na kuumiza watumishi na umeruvuga mambo fulani kwenye utumishi. Mwongozo huo unasema, mtumishi aliyeanza kazi kupanda cheo ni miaka mitano, mmoja kuthibitishwa kazini minne ya kusubiri; hii ni sawasawa na umri wa mtoto kuanza shule. Lakini aliye kazini miaka minne, aliyeenda masomoni muda wake umepotea, hata pandishwa. Sasa Mheshimiwa Jenista mnaenda kupandisha watumishi vyeo, nitaomba wakati unakuja kuhitimisha uniambie mtatumia mwongozo upi kati ya hii mitatu. (Makofi)

Niende kwa watumishi ambao wanakuwa wamepewa teuzi za mamlaka ya Mheshimiwa Rais. Teuzi hizi zinapokoma watumishi hawa wanachelewa kupangiwa kazi, na kwa sababu hiyo kunakuwa kuna hasara mbili; kwa upande wa Serikali kunakuwa na hasara ya kulipa mshahara kwa mtu asiyefanya kazi; na Mungu amesema asiyefanyakazi asile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwa mtumishi mwenyewe binafsi anaweza kuwa na msongo wa mawazo, ulevi na huweza kufa kifo ambacho hakikupangwa na Mwenyezi Mungu. Hilo hilo nalo naomba uliangalie ili teuzi za watu hawa zikikoma basi wapangiwe sehemu za kazi mapema.

Mheshimiwa Spika, lakini kuna watumishi ambao wanatolewa kwenye taasisi kuja kujaza nafasi kwenye Wizara za Serikali na Idara za Serikali, na hapa naomba mpaangalie sana. Watumishi wanaotoka kwenye taasisi wanakuja na mishahara mikubwa, anapofika kwenye Wizara au Idara mwingine ana mashahara kuliko hata Katibu Mkuu wake, sasa sijui hapa kumtuma kunakuwaje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la pili pale kunakuwa na watumishi ambao wameumia na wewe kuanzia vyeo vya chini mpaka wamefika vyeo vya juu. Sasa hao watumishi mnarudisha utendaji kazi wao nyuma. Lakini kama mngekuwa mnawachukua wao mkawapandisha kuwa wakuu wa Idara au wakuu wa Vitengo walio chini yao watafanya kazi vizuri sana ili nao waweze kupanda. Na kwa hili sitaficha, naipongeza taasisi ya Bunge, Bunge wameonesha mfano, Bunge watumishi wao, Wakuu wa Idara, Wakurugenzi, Katibu wao wamezaliwa humo humo kwa watumishi ambao wamewalea wenyewe. Hilo naomba ulichukue tulifanyike kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na niliwahi kuliuliza nikaambiwa vetting sasa huyu tangu akiwa cheo cha kwanza, anaenda mpaka anakuwa principal hizo vetting hazikuonekana? Zinaonekana wakati wa kujaza hiyo nafasi tu? naomba menejimenti ya utumishi wa umma hilo mliangalie.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la recategorization, mnakwenda kufanya recategorization; na niliwahi kuuliza swali la msingi nikajibiwa lakini sikuridhika, na kiti cha Spika kikasema swali la Mheshimiwa Janejelly lina logic lakini mmemjibu mnavyoelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kupunguza mshahara wa mtumishi ni adhabu kati ya adhabu tatu, lakini sasa huyu mtumishi amesoma watoto wake walikuwa wanakula mlo mmoja ili akajisomeshe anapomaliza anakuja kubadilisha kada mnamwambia tunakushusha na mshahara. Sasa kusoma imekuwa ni adhabu. Lakini niwaambie, hakuna anachokuwa anakwenda kuweka gharama, hata wage bill bajeti yake ni ile ile, nafasi yake mnaweza mkaweka hawa ajira mpya, mkaajiri, ikazibwa naye akabaki na mshahara wake. Mnapopunguza mshahara pension yake mmeipunguza, na kama Mungu ameamua kumchukua mirathi yake mmeipunguza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nishauri kwenye ajira mpya, mnatangaza, wasomi wetu wanaomba wengi, labla nafasi 1000 wameomba 20,000 lakini kwenye usahili ule walioshinda labda ni 1,800 au 2,000. niwambe fungua database, hao 1,000 wape kazi. Sasa, ikitokea mnataka watumishi wengine wa kada ile ile nenda kwenye database peleka hao. Hii itatusaidia kuajiri kwa kufuatana na umalizaji wa vyuo; lakini hii ya kutangaza kila wakati, unakuta aliyemaliza elimu mwaka 2020 anapata ajira wa mwaka 2017 hajapata ajira, nalo naomba mliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri ukiyatekeleza hayo utakuwa umetutendea haki watumishi wa Tanzania na tunakuamini haya utafanya. Una kijana hapa anakusaidia, lakini pia wamekupa timu ya watendaji ambayo ninaiamini. Umeletewa Naibu Katibu Mkuu ambaye nimefanya naye kazi, alikuwa boss wangu. Naye haya nilipokuwa nikimwambia alisema sina maamuzi, sasa amepewa maamuzi yupo menejimenti ya utumishi wa umma. Ninawaamini mkiyafanya haya mtakuwa mmemsaidia Mheshimiwa Rais, haya yote anayotaka kufanya kwa watumishi yafanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kuna jambo moja ambalo aliwaahidi watumishi, haya aliyaahidi Meimosi na ameyatekeleza lakini aliwaambia nanukuu; “Wanangu la mshahara naomba mnisubiri mwaka ujao wa fedha”.

Mheshimiwa Spika, Ninaamini Mama kauli zake anaziishi kwa hiyo Watumishi wanasubiri Meimosi kuna jambo ambalo litatajwa.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, ahsanteni sana. (Makofi)