Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza katika Wizara hii. Kipekee sana nampongeza sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana katika Wizara hii. Sambamba naye nampongeza pia Naibu Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya bila kuwasahau Makatibu Wakuu wote wawili na Watendaji wote wa Wizara hii ambayo ni nyeti sana kwa kuhudumia shughuli mbalimbali za Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo ni mwaka mmoja tangu Mheshimiwa Rais alihutubie Bunge lako Tukufu, maana alihutubia Bunge hili tarehe 22 mwezi wa Nne 2021. Kwa hiyo, leo ni mwaka mmoja tangu hotuba yake aitoe ndani ya Bunge hili na katika mchango wangu nitapenda nianze na nukuu ambayo ameitoa wakati anahutubia Bunge. Alisema: “Serikali itaendelea kutekeleza kwa vitendo dhamira yake ya kuwa Serikali anayoiongoza na itaendeleza jitihada za kuimarisha maadili, nidhamu, uzalendo, uchapakazi na uwajibikaji.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia aliahidi pia kusimamia haki na stahiki za watumishi wa umma na watendaji Serikalini ili kuongeza ari ya kufanya kazi kwa bidii na kukuza uwajibikaji wa hiyari katika utumishi wa umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais na mara zote Mheshimiwa Rais alikuwa anatembea katika vitendo vyake. Na tumeona, baada ya ahadi hii alianza kazi kubwa ya kwanza kupandisha madaraja jambo hili ambalo lilikuwa limesimama kwa muda mrefu sana tangu mwaka 2016/2017 lakini kwa mkupuo alikuja kupandisha madaraja watumishi takribani 190,761. Hali kadhalika kuna watumishi wengine takribani 926,190 watapandishwa madaraja na wako katika hatua mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa mchango wangu nilipenda pia kusema eneo moja kwamba katika upandishaji huu wa madaraja kwa mkupuo, tunashukuru kwamba una faida hii; kwamba tumewapandisha kwa mkupuo lakini katika ule mkupuo kuna wale ambao sasa walikuwa wamecheleweshwa sasa kwa kuwapandisha kwa mkupuo maana yake inabidi wale wachache ambao sasa wana sifa za ziada ambazo walicheleweshwa nao tuwabaini ili waweze kusongezwa mbele zaidi ya madaraja. Hii itasaidia pia kuwapatia stahiki zao kwa mujibu wa sheria na baadhi yao wengi wanakaribia kuelekea kustaafu. Maana yake ni kwamba hata mafao yao yaweze kupangwa kulingana na madaraja hayo mapya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo tumeona pia upandishaji wa vyeo, kwamba tumeona wanaendelea kupanda vyeo katika nafasi mbalimbali; na sasa wanakaribia kufikisha watumishi takribani 25,000 ambao wamepandishwa nafasi mbalimbali katika utumishi wa umma.

Mheshimiwa Spika, jambo hili linaonesha ile dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais ya kuongeza ari na uwajibikaji Serikalini, na hii pia inachagiza, ni sehemu ya motisha, ya watumishi ya kuendelea kujitoa na kuendelea kuwajibika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nataka niseme moja ambalo ninaamini kabisa kwamba kwa ninavyomwamini Mheshimiwa Rais hawezi akaacha lipite hivi hivi; hili la kuhusu kupandisha mishahara ya watumishi wa umma. Hili ni jambo ambalo muda mrefu sana halijafanyiwa kazi, takribani sasa ni miaka sita. Lakini kwa ahadi hizi ambazo ameendelea kuzitimiza hata hili ninaamini siku ile ya Meimosi ambayo ndiyo aliyotoa ahadi na haya yote ameweza kuyatekeleza ndani ya kipindi cha mwaka mmoja naamini kabisa kwamba inawezekana kabisa kwa bajeti hii iliyotoka, Trilioni 36 mwaka 2021/2022 na hii ya mwaka 2022/2023 ambayo tunasoma takribani Trilioni 41 sitaki kuamini kwamba fedha zote hizi zinakwenda kwenye miradi, ninaamini kabisa kwamba na watumishi safari hii na wenyewe watatoka kifua mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo hili ni muhimu sana, kuongeza motisha ya wafanyakazi kupitia mishahara kwasababu kwanza tutambue watumishi hawa ni sehemu ya kodi za Serikali, kupitia mishahara yao Serikali inakusanya kodi; kwa hiyo tunapowaongeza maana yake pia tutaongeza kodi hapo baadaye kupitia mishahara ya watumishi, kwa hiyo kwa hali ilivyo sasa ya mfumuko wa bei na upandaji wa gharama mbalimbali za maisha, mimi naamini kabisa kwamba ni wakati sahihi kabisa kwa watumishi nao sasa kuweza kuonwa kwa jicho hili la huruma la Mheshimiwa Rais na wenyewe sasa waweze kupambana na hali hii ya kimaisha, lakini pia kuongeza tija na uwajibikaji katika utumishi wa umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo ningependa kulichangia ni katika fungu 40 ambalo sasa hili ni fungu maalum kwa ajili ya Ofisi ya Rais Ikulu; hili fungu ni muhimu sana. Na katika bajeti hii ambayo imepita tumetenga takribani Shilingi bilioni 24.5 na hadi mwezi Machi zimeshatumika bilioni 18.3. Hili ni eneo muhimu sana Waheshimiwa Wabunge, hizi ndio fedha ambazo zinamwezesha Rais kufanya kazi hizi kubwa ambazo tumeziona katika kipindi hiki kifupi. Hii ndiyo kazi kubwa ambayo zile trilion zilizokuja kwenye madarasa kwenye maji, kwenye afya na maeneo minjini yote zimetokana na fungu hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni vizuri sana tumtengee Rais fedha hizi za kutosha aweze kuzunguka maeneo mbalimbali katika dunia; lakini pia zimesaidia hata kukuza mitaji na uwekezaji, kwasababu tumeona hata hivi karibuni Mheshimiwa Rais alikuwa katika Falme za Kiarabu amefanya kongamano kubwa la expo kule ambako amekutana na wafanyabiashara na wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali. Hii yote ni mitaji ambayo inatokana na kazi nzuri sana ya fungu hili. Kwa hiyo fungu hili ni vizuri sana hata wakati wa kupitisha tupitishe kwa sauti kubwa ili sasa tumpe funguo Mheshimiwa Rais ya kwenda kututafutia mafungu mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halikadhalika Filamu ya Royal Tour ambayo ameizindua hivi karibuni kule Marekani, na tutaanza sasa uzinduzi wake katika Taifa letu, hili nalo ni eneo mahsusi sana la kimkakati kwa ajili ya kukuza utalii wa Watanzania. Tunaona kabisa kwamba dhamira njema hii ya Mheshimiwa Rais kupitia kazi ambayo ameifanya katika filamu ile yeye mwenyewe kuwa kama ndiye tour guide namba moja wa Taifa sasa iwe wake up calls kwa tasnia nzima ya utalii, lakini pia na Wizara nyingine zote kufungamanisha eneo hili la utalii, na pia kukuza uwekezaji na mitaji katika maeneo mengine kwa sababu sasa Tanzania inatangazika katika maeneo mbalimbali duniani kupitia hiyo loyal tour. Kwa hiyo hapa ndipo nilipotaka nielezee kumuhimu mkubwa sana wa fungu hili la 20 ambalo ni ofisi mahsusi ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Eneo la mwisho ambalo nilitaka kulichangia ni eneo la uhaba wa watumishi katika maeneo mbalimbali ya huduma za kijamii hasa elimu na afya. Tumeona kwamba kuna ahadi ya ajira mpya takribani 32,000. Tunaomba sana hivi ajira zitangazwe kwa haraka na zibainishwe vizuri, maana wametokea matapeli ambao wanachanganya vijana wetu. Kwa hiyo ni vizuri kwenye tovuti za Serikali mambo haya yawe hadharani ili wananchi waweze kupata fursa ya kuomba ajira hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)