Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Eng. Isack Aloyce Kamwelwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. ENG. ISACK A. KAMWELWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Innocent Bashungwa pamoja na Naibu Mawaziri David Silinde na Festo Dugange, Wabunge wenzangu wamesema hawa Mawaziri wanafanya kazi vizuri, wanatusikiliza Wabunge lakini wanasikiliza mpaka wananchi wetu. Tunawapa hongera sana na mnamsaidia vizuri sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze pia Katibu Mkuu Prof. Liziki Shemdoe, wiki iliyopita mimi pamoja na timu yangu ya Halmashauri yangu tulikwenda ofisini kwake kumtembelea tulikuwa na hoja nne baada ya masaa sita hoja moja alikuwa ameshaijibu na hoja hiyo nilikuwa nimeomba Mwalimu wa jinsia ya kike kwenye Sekondari ya Kata ya Ilunde ambayo ipo na kidato cha tatu na ina wasichana wengi lakini haikuwa na mwalimu wa jinsia ya kike. Katika muda wa masaa sita alikuwa ameshampanga tayari mwalimu wa kike na ninaimani kwamba mwisho wa mwezi huu ataripoti kwenye ile sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika masuala yaliyotupeleka yalikuwa manne katika muda wa masaa 24 yote walikuwa wameshayatekeleza. Ndio maana mimi Wizara hii ile timu ya Katibu Mkuu, Naibu Katibu, Naibu Makatibu Wakuu pamoja na Wakurugenzi ushirikiano niliouona jinsi walivyotuhudumia nimewaita kwamba hawa ni 24 hours action, wanafanya kazi vizuri na kwakweli Wizara hii ikienda namna hii kweli inatekeleza maagizo ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ambayo ameiandaa vizuri na aliisoma vizuri kwa sauti ya kusikika tena kwa utaratibu, ukurasa wa pili alizungumzia jinsi alivyotumia fedha alizotoa Mama yetu, fedha za UVIKO amechambua ni maeneo gani ambayo fedha ile ameitumia, katika vitu alivyovieleza ni pamoja na ununuzi wa magari ya ofisi, lakini pamoja na ununuzi wa magari ya wagonjwa, sasa Mheshimiwa Waziri nikuombe nina Kata moja ya Ilunde ipo mbali sana na Makao Makuu ya Wilaya, katika hayo magari niombe gari moja lipelekwe kwenye ile Kata gari la Wagonjwa Kata ya Ilunde.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwasababu hauwezi ukapiga simu mtu anaumwa gari litoke kilometa 100 limchukue mgonjwa halafu limrudishe tena kilometa 200 tutakuwa tuna risk maisha ya mgonjwa. Mheshimiwa Waziri nikuomba sana kwamba utakaponunua magari kumbuka gari moja liende kwenye hiyo Kata inaitwa Kata ya Ilunde.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri pia umenijengea hospitali ya Wilaya kwenye Jimbo langu kuna gari moja tu, sasa kitakuwa ni kitu cha ajabu kwamba hospitali ya Wilaya haina gari la wagonjwa inaazima gari kwenye kituo cha afya ambayo ulitupa mwaka jana, niombe sana hili Mheshimiwa Waziri ulikumbuke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru sana Serikali katika bajeti ya Wizara hii, sio hii tunayoiomba sasa hivi ila hii ambayo tunaitekeleza tunaimaliza mwezi Juni, Serikali ilitoa bilioni 22.87 kwa ajili ya kulipa madeni ya wazabuni, nikushukuru sana Mheshimiwa Waziri kwamba sekondari yangu ya A-Level ya Inyonga umetoa shilingi 72,000,000 kulipa madeni ya wazabuni lakini nikuombe bado kuna wazabuni wanadai shilingi 175,000,000 tena wazabuni hawa ni akinamama lishe sehemu kubwa, na wale ambao wamepewa asilimia 10 na Halmashauri wamepewa zile fedha na bado mkawafanyisha biashara nyinyi wenyewe, sasa ni kitu cha ajabu kwamba mnashindwa kuwalipa na kama ukishindwa kuwalipa maana yake na wao watashindwa kurudisha zile fedha tulizowakopesha zile asilimia 10.

Niombe sana Mheshimiwa Waziri kabla hatujafunga mwaka hii shilingi 175,000,000 tuitoe ili hawa wazabuni hawa ambao tumewakopesha fedha sisi wenyewe tuweze kuwalipa na wao waweze kulipa kwenye Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna watumishi wenzenu Mheshimiwa Waziri, wapo Walimu wanadai malimbikizo ya shilingi 136,000,000, kuna wafanyakazi wengine wasio Walimu wanadai zaidi ya Shilingi 789,000,000 niombe pia kwasababu hawa ni watumishi wenzenu hebu walipeni ili mambo yaweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri hii Wizara kwenye bajeti ya mwaka huu…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Eng. Isack Aloyce Kamwelwe, muda wako umekwisha.

MHE. ENG. ISACK A. KAMWELWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)