Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Nashon William Bidyanguze

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kwanza kukushukuru kwa kunipa nafasi hii, lakini pia naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya ya kuweza kusimama hapa Bungeni niweze kuchangia kwenye hotuba hii ya Waziri wa TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya yote naomba nimshukuru Rais wetu mpendwa Mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kuifanya katika nchi yetu na hasa katika Jimbo langu la Kigoma Kusini. Nimeshuhudia na wananchi wameshuhudia kupata madarasa 196 kwenye eneo la Sekondari na madarasa kwenye shule shikizi. Ni jambo kubwa sana na shule hizi zimekuwa ni mpya zaidi sasa kuliko shule zile za msingi. Naomba katika eneo hili shule za msingi nazo Mheshimiwa Waziri uzione kwamba zimebakia chini sana na zimebaki na majengo mabovu sana nimeona kwenye hotuba yako ya bajeti umeonyesha kutenga fedha kwa ajili ya shule kongwe naomba na mimi kwenye Jimbo langu liangalie sana ziko shule nyingi ambazo kwa kweli zina majengo mabovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano iko shule moja katika Kata ya Itebula na ni shule yenyewe ya Itebula kwa kweli mpaka watoto wamehama kujaribu kusomea kwenye vyumba vichache ambavyo kidogo kuna nafuu na mimi kwenye mfuko wangu wa Jimbo nimepeleka fedha pale angalau nijaribu kuokoa hali ya shule ile na hali ya wale watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kwenye eneo la ahadi za viongozi wakuu. Nakumbuka Mheshimiwa Hayati Magufuli wakati anaomba kura kwenye Jimbo langu eneo lile la Uvinza aliahidi kilometa tano za barabara ya lami lakini nashukuru kwamba angalau kuna kilomita mbili zinaendelea kujengwa. Lakini pia aliahidi kilomita tano Nguruka bado hata kilomita moja haijajengwa, sasa naomba Mheshimiwa Waziri kwenye eneo hili la ahadi za Viongozi wetu Wakuu kwa kweli uweke nguvu sana kwa sababu inapunguza imani ya wananchi na Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Magufuli aliahidi kutoa Shilingi Milioni 10 kwenye kituo cha afya pale Kazulamimba wananchi wanashangaa hivi ni kweli Milioni 10 inaweza ikashindikana kupelekwa pale Kazulamimba ambapo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais ni jambo la kushangaza sana na mimi wamekuwa wakinisumbua sana wanasema Mheshimiwa Mbunge ni namna gani Milioni 10 haijafika. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri upeleke Milioni 10 Kazulamimba kwa sababu tayari wameshajenga boma wanahitaji kuendeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa alitoa ahadi ya kupandisha hadhi kituo cha afya cha pale Nguruka na kilishapanda hadhi kwa hiyo tunasubiri Mheshimiwa Waziri uweze kuleta fedha kwa ajili ya kujenga sasa majengo kwa ajili ya kuendeleza sasa hospitali ile ambayo ilishapandishwa hadhi. Nilijenga hoja wakati ule naomba kura wananchi na Mheshimiwa Rais alikuwepo kwamba Nguruka mpaka kwenye hospitali ya Wilaya ilipo ni umbali wa kilometa 100 kwa hiyo Mheshimiwa alikubali kuongeza hadhi ya kituo kile na kilishapanda hadhi naomba uweke fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna ahadi ambazo alipokuja Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Ummy Mwalimu alikubali kujenga kituo cha afya chenye hadhi ya hospitali zaidi kidogo ya kituo cha Afya kule ukanda wa maji, eneo moja linaitwa Lukome na ninashukuru Serikali fedha Shilingi 250,000,000 zimeshakuja na ujenzi unaendelea naomba kwenye bajeti hii Mheshimiwa Waziri uongeze fedha ili tuweze kumalizia ujenzi wa hospitali ile kwa sababu inakuwa ni hospitali ya rufaa kwa sababu eneo lile na Mheshimiwa Ummy alitengeneza historia kutoka Makao Makuu ya Wilaya kwenda Kalya ni kilometa 300 kwa hiyo unaweza ukaona ni eneo kubwa sana ambalo linahitaji huduma hiyo ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Waziri Ummy alikubali kufungua barabara ambayo inatoka Kalya kwenda Sumbawanga, alikubali kutoa Shilingi Bilioni Moja na Milioni Mia Tano, naomba ahadi hiyo uiandike ili kusudi mwaka huu wa fedha tuweze kupata hiyo fedha tuweze kufungua hiyo barabara. Pia aliahidi kujenga jengo moja la wodi ya wanaume na watoto pale kwenye kituo cha afya cha Kalya, naomba ahadi hizi Mheshimiwa kwa sababu wewe sasa ndiyo umeingia kwenye kiatu ambacho alikuwa amevaa Waziri Ummy hili jambo uweze kulichukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vinginevyo kwakweli mambo yanaenda vizuri na naomba nipongeze…

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze kwa mchango wako.

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, na niseme naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)