Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Mariam Madalu Nyoka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Awali ya yote naomba niipongeze Serikali kwa kuendelea kufanya kazi nzuri ya kuiletea maendeleo nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie eneo la TARURA kwenye Mkoa wa Ruvuma. Mkoa wa Ruvuma ni kati ya Mikoa mikongwe nchini. Mkoa huu una mtandao wa barabara zipatazo kilomita 7,146, lakini kati ya kilomita hizo TARURA inaweza kuhudumia barabara zenye urefu wa kilomita 1,072 sawa na asilimia 15 tu ambapo hata robo ya mtandao haujafikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Ruvuma una changamoto nyingi hasa katika kipindi hiki cha masika. Changamoto nyingi tunaona kwenye barabara, barabara nyingi zimekatika, madaraja yamekwenda na maji ya mvua, vivuko vimevuka, mifereji ya maji ya mvua pia imebomoka. Naomba tuuangalie mkoa huu kwa jicho jingine kwa sababu, jina la mkoa ni kubwa, lakini ukienda kwenye uhalisia una changamoto kubwa ya miundombinu tofauti na jina linavyotamkwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa barabara chache zenye changamoto kwenye Mkoa wa Ruvuma ni kama barabara ya Mbinga kwenda Mpepai inayofika mpaka Lipalamba hii ina changamoto kubwa mno. Barabara ya Madaba kwenda Maweso ni changamoto. Barabara inayotoka Mandepwende kwenda Mtonya, Namtumbo. Barabara ya Dapori kwenda Machimbo. Barabara ya Peramiho kwenda Mdunduwalo inafika mpaka Litoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Songea Mjini pia kuna changamoto kubwa ya barabara pale ambapo barabara nyingi tunaona zinashindwa kupitika hasa kwa wakati huu. Juzi tu nilichangia kuna barabara inayotoka Majengo inapita Ruvuma, Subira kwenda Mpitimbi ina changamoto kubwa. Barabara nyingine ni Barabara ya Mkuzo inapita Muslim kwenda Mwengemshindo ni changamoto. Pia, kuna barabara inayotoka Kata ya Lizaboni inapita Heroz kwenda kwa Manya kupitia Kituo cha Afya cha Mji Mwema. Kituo kile kinategemewa na wakazi wengi wa Mkoa wa Ruvuma pia pamoja na wilaya nyingine ambazo ni jirani ya pale Wilaya ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa barabara zimebomoka mwananchi anashindwa kufika kwenye kituo kwa wakati. Tunaomba barabara ile iangaliwe kwa jicho jingine kwa sababu wananchi wale wanashindwa kufika kwenye kituo kupata huduma za afya. Tukikarabati… (Makofi)

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Barabara nyingine ni pamoja na barabara inayotoka Namakambale kuelekea…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jacqueline Msongozi, umesimama kwa Kanuni gani?

T A A R I F A

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimesimama kwa Kanuni ya 77(1) kwa sababu ya muda naomba nisiisome.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kumueleza mchangiaji anayechangia sasa kwamba, ni kweli kabisa anavyosema, barabara zilizoko katika Mkoa wa Ruvuma kupitia TARURA tunaomba zisaidike. Kimsingi kuna Barabara ya Majengo – Ruvuma, yenye kilometa Tisa ambayo kimsingi ndio inaunganisha Wilaya ya Songea Manispaa na Songea Vijijini n ani barabara ya kimkakati, wakulima wengi wanaitumia kwa ajili ya kusafirisha mazao. Ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Endelea Mheshimiwa Mariam Nyoka.

MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea taarifa hiyo kwani barabara hiyo ni muhimu mno kwa wakazi wa Wilaya ya Songea pamoja na nchi nyingine inayounganika pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye barabara nyingine ambazo ni Barabara ya Namakambale inakwenda kwenye Kata ya Mwamnono, Wilaya ya Tunduru. Barabara ya Songambele na Lupala nayo ni changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali, naomba ifanyike tathmini ya ubovu wa barabara za TARURA uliopo, madaraja, mifereji ya mvua pamoja na vivuko ili iandae mpango wa matengenezo kwa uhalisia zaidi. Pia, naiomba Serikali ifanye matengenezo ya barabara hizi kwa kiwango cha changarawe ikiambata na mifereji ya mvua. Kwa kufanya hivi barabara hizi zitakuwa za kuliko ilivyo hivi sasa, tunaona tunafanya matumizi mabaya ya fedha za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hiyo naomba…

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Mariam Madalu Nyoka kwa mchango wako. Muda wako umekwisha.

MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naunga mkono hoja. (Makofi)