Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi.

Kwanza kabisa niendelee kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na timu yake, pamoja na Katibu Mkuu pamoja na Naibu Makatibu Wakuu kwa kazi nzuri wanazozifanya. Kabla sijaendelea kwanza na mimi niunge mkono hoja, lakini vilevile niendelee kutoa shukurani zangu kwa Wabunge wenzangu wameongea vizuri sana kuhusiana na suala la Madiwani. Suala la Madiwani kukosa mishahara kupewa posho mimi naona ni kama kutokuthaminiwa, anayepewa posho ni yule mtu anayefanya kazi kwa siku ni kibarua hivi kweli Diwani amekuwa kibarua? Diwani anayefanya kazi ya kusimamia maendeleo anakuwa hatambuliki kiajira, matokeo yake analipwa posho kama vile kibarua. Mimi ninawashukuru sana Wabunge na kwa kweli Serikali imefika wakati sasa muwaone kabisa kwamba, Madiwani ni Wabunge kama walivyo Wabunge wa Majimbo na wao ni Wabunge wa Kata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Madiwani na sisi ni sawa sawa kabisa tofauti yetu na wao sisi tunakuja huku Bungeni Dodoma na wao wanabaki kwenye Halmashauri na wakati mwingine wao ndiyo wako karibu zaidi na wananchi na ndiyo wanaosikiliza shida za wananchi kila siku. Tunaomba sana Serikali iwajali Madiwani walipwe mishahara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo niendelee kumshukuru sana na kumpongeza Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha nyingi. Ninakushukuru sana Mheshimiwa Waziri unavyofuatilia kwa kweli kazi yako ni nzuri na kwa kweli kila mmoja anapongeza na tunaona juhudi zako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa iliyobaki ni kusimamia fedha hizi tuone thamani ya fedha katika miradi ambayo imetengewa fedha. Mimi noamba nitoe tu ushauri mdogo. Kuna Mwenge wa Uhuru unapita na unakagua miradi mbalimbali, miradi hii inapokaguliwa wanafanya ukaguzi wa ghafla. Wanafika pale jana na juzi tumeona mmoja ameshika sululu anachimba kwenye lami anakagua, mwingine tumeona juzi anabonyeza nondo kwa mikono. Ukaguzi huu ni wa ghafla wakati mwingine wanaweza kweli wakaibua hoja zenye mashiko, lakini wakati mwingine wakawa labda wanawaonea wale wahusika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kabla Mwenge haujafika eneo husika pawe na timu maalum iwe inatangulia inafanya ukaguzi wa kina, Mwenge unapofika wanapata ripoti wanatoa mapendekezo na maoni yao kisha wanafungua mradi au kutokufungua mradi. Wafanye hivyo badala ya kushtukiza, huo ni ushauri wangu wa haraka haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni TARURA. TARURA mnafanya kazi nzuri nishukuru sana Maswa mmetupa kilomita za lami, kuna kilomita moja kuna kilomita moja na nusu na fedha zinakwenda, lakini hawa Wakandarasi wanapoleta zile certificate mnachelewa kuzilipa, mkichelewa kulipa miradi inasimama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maswa pale kuna mradi mmoja wa kilomita moja soko la jioni umechelewa kumalizika ule mradi wa toka mwaka 2015. Kuna Mkandarasi anadai fedha ali-raise certificate wakachelewa kulipa Shilingi Milioni 188 leo ndiyo wamemlipa sasa hivi anaendelea na shughuli lakini nchi nzima mnachelewesha kuwalipa naomba mfanye kazi nzuri, mnafanya kazi nzuri lakini tunaomba muwahi kuwalipa Wakandarasi hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine katika Halmashauri yangu ya Maswa kuna jengo la Halmashauri, nawaombeni sana mtoe fedha mtujengee jengo la Halmashauri, Wilaya ya Maswa ni kongwe lakini jengo la Halmashauri ni la kizamani kabisa, tunaomba fedha tujenge Halmashauri hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna ujenzi wa stendi pale Maswa tunaomba mtujengee stendi ya mabasi, kwa kweli hali siyo nzuri tunaomba fedha mtujengee stendi ya mabasi. Huo ndiyo ujumbe wangu kwenu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, kuna mazao ya mkakati, pamba ni zao la mkakati tunalima pamba sisi, kuna korosho, kuna tumbaku, kuna kahawa, kuna chai. Mazao haya kwenye maeneo wanayolima mazao haya tumeona miradi ya kutengeneza barabara kwenye maeneo wanakolima mazao haya kwa ajili ya kusafirisha mazao haya kutoka maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maswa na maeneo mengine tunayolima pamba hatuoni mkakati wowote wa kuboresha zao la pamba, kulitengenezea miundombinu ya kusafirisha zao la pamba katika maeneo hayo. Kama miradi ya mkakati mnaitambua au mazao ya mkakati mnayatambua kwa nini pamba hamlitambui zao hili? Kwa nini mnatambua korosho, kwa nini mtambue chai, kwa nini mtambue kahawa? Mnapeleka barabara, mnatengeneza barabara nzuri katika maeneo hayo, kwa nini msitengeneze barabara za kusafirisha zao la pamba katika maeneo hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunakwenda kuivisha zao la pamba hakuna barabara, pamba imelimwa kwa wingi, watu wamevutika kulima pamba, lakini barabara ni mbovu ni mbovu haijawahi kuonekana. Tunawaomba sana TARURA muongee na Wizara ya Kilimo katika mazao ya mkakati, tunaombeni mtutengenezee miundombinu ya kusafirisha mazao haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba nikupe tip moja nafahamu. Kwenye hospitali zetu za Wilaya Madaktari wana-enjoy kuandika dawa fulani na dawa fulani hazipo. Hawatoi maoteo mapema kupeleka MSD wana- enjoy kukosekana kwa dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wana-enjoy kwa sababu gani? Dawa inapokosekana MSD akaambiwa hii dawa iko out of stock yeye anapata nafasi ya kwenda kwa washitiri na kutangaza tender kununua kwa kutumia Local Purchasing Order. Akitangaza tender hiyo akiongea na mshitiri kule deal inapigwa huko wanapata fedha. Wakurugenzi jirekebisheni muwe wazalendo katika Taifa lenu. Ukifanya hivyo unamsababisha Mtanzania kukosa dawa, akikosa dawa Mtanzania kwa kweli hili ndilo linaleta tatizo kubwa. Mheshimiwa Waziri wekeni mfumo wa kusimamia dawa kwenye Hospitali za Wilaya, Zahanati na Vituo vya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Naibu Waziri hapo anafahamu ni Daktari anajua hili. Washitiri wanafanya deal na Waganga wa Wilaya tunaombeni sana muweke mfumo mzuri kwa kushirikiana na Wizara ya Afya muwe na mfumo wa ku-monitor dawa kuanzia mwanzo mpaka inavyokwenda kutumika kwa mtumiaji. Tunaomba sana suala hilo mlizingatie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nashukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)