Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Agnesta Lambert Kaiza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili nami kwa uchache niweze kuchangia katika Kamati ya Katiba na Sheria, Kamati ambayo mimi mwenyewe ni Mjumbe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze Kamati ya Katiba na Sheria kwa kazi nzuri iliyotukuka ambayo imeweza kuifanya chini ya Mwenyekiti wetu na niseme kwamba naunga mkono kwa asilimia 100 kile ambacho kimewasilishwa hapa katika Bunge lako tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita leo katika kuchangia suala zima la ushirikishwaji wa wadau katika kutunga sheria. Taarifa ya Kamati imeweka bayana umuhimu wa kutanua wigo kwa ajili ya wadau kushiriki vyema kabisa katika kutoa maoni yao katika utungwaji wa sheria, na tunafahmu vyema kabisa kwamba zipo faida nyingi sana ambazo tunazipata kama Taifa pale ambapo ushiriki wa wadau unakuwa ni ushiriki uliokamilika kwa maana ya kupata muda mzuri, muda wa kutosha kudadavua, kupitia sheria zote ili hata wanapokuwa wanatoa maoni basi, watoe maoni ambayo yanaendana na uhalisia wa wananchi ambao wanakwenda kutekeleza sheria hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mapendekezo hayo mazuri ya Kamati, niseme kwamba lipo tatizo moja kwa upande wa Serikali na tatizo hilo ni kuleta miswada kwa Hati ya Dharura hapa Bungeni, miswada ambayo mara nyingi inakuwa haina udharura ndani yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapokuwa unaleta muswada Bungeni kwa Hati ya Dharura, wote tunafahamu kwamba, lazima kuwepo na udharura kweli kweli, na tunafahamu kwamba, udharura wenyewe ni pale ambapo huenda nchi ipo hatarini au nchi iko katika vita au kuna udharura mkubwa kiasi kwamba jambo hilo lisipotungiwa sheria kwa Hati ya Dharura nchi itakuwa katika hatari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi ni mashahidi katika Bunge lako hili tukufu, ipo mifano mingi sana ya miswada ambayo imeletwa hapa Bungeni kwa Hati ya Dharura, lakini haikuwa na huo udharura, na kwa sababu, ililetwa bila wadau kuwa wametoa maoni yao kikamilifu sheria hizi zilivyopitishwa tu kwa muda mfupi zilirudi Bungeni kwa ajili ya marekebisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti sisi ni mashahidi katika Bunge lako hili tukufu, ipo mifano mingi sana ya miswada ambayo imeletwa hapa Bungeni kwa hati ya dharura lakini haikuwa na huo udharura na kwa sababu ililetwa bila wadau kuwa wametoa maoni yao kikamilifu, sheria hizi zilivyopitishwa tu kwa muda mfupi zilirudi Bungeni kwa ajili ya marekebisho na unapoona kwamba Bunge ambalo linaaminiwa na nchi kwamba Wabunge tumepewa jukumu la kutunga sheria tunatunga sheria ambayo inakwenda kwa wananchi na muda mfupi inarudi kuonekana kwamba kile tulichokitunga hakikuwa na uhalisia hii inakuwa ni aibu kwa Taifa, lakini pia tunakuwa tunachonganisha sasa Bunge na wananchi, lakini pia tunakuwa tunamchongea Mheshimiwa Rais ambaye lazima asaini zile sheria sasa zianze kwenda kutumika. Sasa zinakuwa zimetumika na zimerudi kwamba hazina tija, Mheshimiwa Rais naye tunakuwa tumemweka katika wakati mgumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mifano ya baadhi ya sheria ambazo tulizitunga na muda mfupi tu zikarudishwa hapa Bungeni. Sheria ya kwanza ni Sheria ya Habari; sisi ni mashahidi sheria hii ilirudi na ni kwa sababu hatukutoa mwanya wa wadau kudadavua na kutoa maoni yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria nyingine ni Sheria ya Vyama vya Siasa; Serikali ilileta muswada huu wa Sheria ya Vyama vya Siasa kwa hati ya dharura na haikuwepo udharula wowote ule na kimsingi muswada huu ndio muswada pekee ambao ulipaswa kutoa wigo mpana wa wadau kuweza kuchangia, kudadavua kuweka mpaka midahalo ili tunapokuja Bungeni kupitisha tuwe tumepitisha jambo ambalo ni sahihi, lakini nao pia ulirudishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria nyingine ni Sheria ya Takwimu; huko nje kwa wananchi, wananchi tunaowaongoza wanatuamini sisi Wabunge waliotuchagua wakiamini kwamba sisi ndio wanasheria wao ambao tunakuja kuwatungia sheria ambazo zitakuwa ni rafiki ili ziweze kutekelezeka, lakini matokeo yake tunatunga sheria ambazo mwisho wa siku zinakuwa ni mzigo, zinakuwa hazitekelezeki na ni kwa sababu ya Serikali kuleta miswada kwa hati ya dharura ambayo haina udharura wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili naomba nishauri sasa; Serikali nafahamu kwamba inatambua nini maana ya neno udharura inajulikana na wote tunafahamu. Ituletee miswada ya hati ya dharura ambayo kweli kweli ina hati ya udharura, I mean ina uhitaji wa haraka wa kutungiwa sheria kwa hati ya dharura. Lakini kama si hivyo basi Serikali inapaswa kuleta hii miswada ya sheria kwa maana kuhakikisha wadau wote wameshiriki kikamilifu na ikibidi sisi Wabunge ambao ndio wadau namba moja, sisi ndio watunga sheria, sisi ndio wapitisha sheria, sisi wenyewe nje ya wadau wengine tunapaswa kudadavuliwa moja kwa moja hii miswada kabla hata haijaja Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.