Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Wakati ukaguzi wa CAG unafanyika mpaka tarehe 30 Juni, 2020/2021 tulikuwa na Halmashauri za mamlaka 185, lakini mpaka tarehe hiyo walikuwa wameshakagua Mamlaka ya Serikali za Mitaa 42 sawa na asilimia 23. Pia walifanya ikaguzi maalum kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa 34. Kamati ya LAAC ilikutana na kuwahoji mamlaka nne, hiyo taarifa yote ambayo imezungumzwa hapa. Sambamba na hilo ni kwamba kulikuwa na shida ya muda na bajeti vile vile.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka Waheshimiwa Wabunge waone huu ukosefu wa muda na bajeti, madhara yake ni nini? Nikijaribu kuangalia, ukiacha mengine ambayo yametajwa hapa kule Ilemela, inawezekanaje watu ambao walikuwa ni watumishi, bado wanaingia kwenye mfumo wa Serikali na wanabadilisha ankara ambazo ni mabilioni kwa mabilioni kwamba hao watu kweli hawajulikani?

Mheshimiwa Naibu Spika, inawezekanaje kwamba kuna stakabdhi 822, yaani hazionekani! Halafu kuna makampuni 270 wanafanya biashara katika Halmashauri ya Ilemela halafu hawalipi kodi. Pia ukiangalia kwa mfano fedha ambazo ile asilimia 10 ambayo inapelekwa, mamlaka 155 fedha haijarejeshwa shilingi bilioni 47.01. Pia mamlaka 83 hawajapeleka fedha katika makundi yale matatu; vijana, wanawake na watu wenye ulemavu shilingi bilioni 6.8.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika ukaguzi maalum uliofanyika, katika mamlaka 37 shilingi bilioni 19.72 hazikupelekwa benki. Hawajaishia hapo, kwenye mashine za POS katika ukaguzi wa CAG yenye ukurasa 308 wanasema kuna shilingi bilioni 18 zilipotea au hazikwenda benki, hawajui ziko wapi. Pia wanatuambia, kuna vyanzo ambavyo ni muhimu hawakukusanya kodi au ushuru wenye jumla ya shilingi bilioni 14.3. Vilevile kuna maeneo ya levy haikukusanywa ambayo ni shilingi bilioni 6.03.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye afya wanatuambia, kwenye mamlaka 46 za Serikali za Mitaa, dawa zili-expire ambazo zilikuwa na gharama ya shilingi bilioni 3.49. Pia wanatuambia kwenye ukaguzi, nimefupisha tu, kwamba kuna fedha ambazo kuna madai mbalimbali ya mishahara na taasisi, amesema Mheshimiwa Waziri, lakini hapa walikuwa wanadai jumla ya shilingi bilioni 160 hazijalipwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia fedha ambazo zilipaswa kwenda Social Security Funds hazikupelekwa. Katika mamlaka 42 ni shilingi bilioni 183.09. Kuna miradi ya maendeleo ya wananchi ilicheleweshwa katika mamlaka 128 yenye jumla ya shilingi bilioni 195.65. Vilevile mamlaka 21, Shilingi bilioni 41.51 Wilaya ya Buhigwe iliachwa iliachwa. Sasa yako mengi ya kutaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, walipanga kupeleka vitabu Million 6.3 vilienda vitabu Milioni 1.4 yenye gharama ya Bilioni 5.18. Nachosema ni kwamba ukiangalia kazi ambayo Mheshimiwa Rais Mama Samia anayofanya na kutafuta fedha katika vyanzo mbalimbali, ukasoma ripoti ya CAG yenye kurasa 308, ukaangalia upotevu wa fedha zilizopotea, jambo hili Waheshimiwa Wabunge halipaswi kunyamaziwa. Jambo hili ni lazima Mheshimiwa Rais, achukue hatua, Serikali ichukue hatua na Bunge lazima liwe na meno. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia hata taarifa yenyewe imekuja hapa tunapewa Dakika Tano, unaambiwa ingiza kwenye Hansard hili jambo tulipaswa tujadili siku tatu, kila Kamati na siku zake na tufanye maazimio na Serikali ipewe muda ije itupe majibu. Hatuwezi kuwaambia wananchi wachangie maendeleo wakati kapu limetoba, tenga haliwezi kujaa, kuna matundu kibao. Waheshimiwa Wabunge tumekutana kwenye Bunge hili kwa ajili ya Watanzania maskini, wanatusikiliza lazima tuwe sauti kwa wasiokuwa na sauti, tufanye maamuzi sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge hili lazima kabla ya Bajeti ijao Serikali ije na mpango mkakati vinginevyo ukaguzi wa CAG ni kupoteza fedha. Fedha hizi ni nyingi kwelikweli lazima zisimamiwe. Nilikuwa nasoma ripoti naangalia kule Nyamungo ambapo wananchi wangu hawana maji, hawana barabara, watoto wanakaa chini, nikajiuliza tungeweza kuchimba visima vingapi katika Halmashauri yetu? Tungenunua magreda mangapi katika hizi fedha? Tungetengeneza madawati mangapi watoto wasome? Walimu wangejengewa nyumba ngapi? Hili Waheshimiwa Wabunge ni jambo ambalo ni muhimu, lazima tuchukue hatua na Serikali hapa lazima iwajibike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa walioiba fedha washughulikiwe, tuambiwe kwanini hawapo jela? Wako wapi na wanafanya nini? Nani anawalinda, anawalinda kwa faida ya nani, kwanini wasiwajibishwe? Kama watu wameiba fedha hawajahukumiwa utamkamata nani? Haya ni mambo ya kupendeleana, Bunge msikubali kufanya hivyo, lazima tuwawajibishe watu. Serikali isilete maneno maneno hapa watu wawajibishwe, hawa ni wezi sawa na vibaka wengine mtaani, wawajibishwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaambie ripoti hii iko mtaani, ripoti hii wananchi wanasoma, wanaelewa, wanataka kuwaona Wabunge wao wa Chama Cha Mapinduzi kwa asilimia kubwa mnachukua hatua gani? Tuanze kuchukua hatua sasa kabla ya sisi kwenda kuwajibishwa na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, ahsante. (Makofi)