Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii niweze kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PIC ambayo iko chini ya Msajili wa Hazina. Msajili wa Hazina anayo Mashirika zaidi ya 230 ambayo Serikali yetu imewekeza mtaji wa zaidi ya trilioni 67.

Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa taasisi hizo yapo makampuni ambayo Serikali yetu ina hisa chache mojawapo ni kampuni ya TANICA ambayo iko Mkoani Kagera. Namshukuru Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa aliyoifanya kuhakikisha kwamba anaboresha zao la kahawa Mkoani Kagera.

Mheshimiwa Naibu Spika, juhudi ambazo Waziri wetu Mkuu alizifanya Kagera ningeomba ziende sambamba na kuboresha Kiwanda cha TANICA Mkoani Kagera. Nashukuru sana Kiwanda cha TANICA kagera ambacho Serikali yetu inamiliki hisa asilimia Saba, TANICA kilijengwa mwaka 1963 kwa hiyo teknolojia iliyojenga kiwanda hicho nyakati hizi, hiyo teknolojia haipo imepitwa na wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposema tunaboresha kilimo lazima twende sambamba na kujenga viwanda ambavyo vitaongeza thamani ya mazao ya mkulima. Mkoa wa Kagera unazalisha zaidi ya tani 34,000 za kahawa lakini kiwanda hiki ambacho Serikali ina hisa asilimia Saba kinaweza kikaongeza thamani asilimia mbili tu ya kahawa inayozalishwa Mkoani Kagera. Ndiyo maana kila mwaka Serikali inatumia nguvu sana kuweza kupambana na magendo ya kahawa kwa sababu wakulima hawana soko la uhakika la kuuza kahawa yao. Kama Serikali ingeongeza mtaji kwenye kiwanda suala la kukimbizana na kahawa au magendo ya kahawa Mkoani Kagera ingebaki historia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanda cha TANICA ambacho Serikali ina hisa chache, kina mtaji wa bilioni kumi lakini share ambazo zimelipiwa ni bilioni moja na milioni mia nne tu, zaidi ya bilioni 8.6 hazijalipwa. Nakumbuka mwaka jana tulikuwa na Kamati Teule chini ya Viwanda na Biashara, ambayo ilifanya tathmini ya hiki kiwanda na ikatoa mapendekezo kwamba Serikali kutokana na umuhimu wa hicho kiwanda cha TANICA Mkoani Kagera ilipe lile deni la shilingi bilioni 8.6 ili Serikali iweze kumiliki hisa nyingi zaidi kwenye hicho kiwanda na iweze kukipatia mtaji kusudi kiweze kuongeza thamani mazao ya kahawa Mkoani Kagera.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwenye hili pamoja na viwanda vingine ambavyo vinaendeshwa chini ya mtaji wake, maana yake vinazalisha chini ya viwango, Serikali itafute pesa iviongezee mtaji ili viweze kuzalisha kwa kiwango kinachotakiwa. Kwa kusema hivyo, tutakuwa tumewasaidia wakulima wetu ambao wanazalisha kwa wingi na wakati mwingine tunakosa masoko kwa sababu hatuna viwanda vya kuongeza thamani kwenye mazao tunayozalisha nchini, kufanya hivyo tutakosa pesa ya nje ambayo tunahitaji sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposema kuongeza mitaji kwenye viwanda, tumesikia kwenye Kamati ambazo zimesoma ripoti za leo, pesa ambayo inaibiwa kama tutaweza kuithibiti tunaweza ikatusaidia kuongeza mitaji kwenye viwanda ambavyo vinahitaji hizi pesa nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili haya Mashirika ambayo yako chini ya Msajili wa Hazina yanaendeshwa chini ya sheria na utaratibu ambao tumeuweka sisi wenyewe. Lakini cha kushangaza Sheria ya Msajili wa Hazina ni sheria ambayo ilitungwa mwaka 1959, nchi hii kabla haijapata uhuru, lakini bado tunatumia sheria kongwe ya namna hiyo kuendesha uchumi, kuendesha mashirika 237, yenye mtaji wa trilioni 67 kwa kutumia sheria kongwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia utajiri ambao tunao kwenye haya mashirika ambayo tumesema trilioni 67, kama tungekuwa na sheria ya kisasa ambayo inampa nguvu na uwezo Msajili wa Hazina, tungekuwa na utajiri zaidi ya hapo labda zaidi ya mara mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana niliongelea hili kwamba Sheria ya Msajili wa Hazina imepitwa na wakati, ni muda muafaka sasa tuifute na tutunge sheria mpya ambayo inalingana na uchumi wa sasa lakini ambayo itampa nguvu na mamlaka Msajili wa Hazina ili aweze kuchukua hatua pale ambapo inahitajika kuhakikisha kwamba Watendaji wa Mashirika haya ambayo ni ya umma pale ambapo anawapa vigezo KPI wanashindwa kuvitekeleza, pale ambapo mashirika hayana bodi lakini Msajili yupo amebaki tu kama Mshauri, ni muda muafaka sasa kumpatia nguvu, kumpatia meno ili aweze kuyawajibisha mashirika haya ambayo yanasababisha hasara, ambayo hayazalishi, na ambayo yanafanya chini ya viwango lakini kwa sasa kwa sheria tuliyonayo hayo mamlaka hana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia mashirika haya ambayo yanazalisha mali ni mfumo wa kampuni na mengine Mashirika ya Umma, mengi Serikali imewekeza lakini ukiangalia tija tunayoipata ni ndogo mno, kwa maana hiyo naomba nishauri Sheria ya Msajili wa Hazina iletwe Bungeni ifanyiwe kazi na kwa ushauri wangu ifutwe na tutunge sheria mpya na ya kisasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga hoja mkono. (Makofi)