Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Francis Isack Mtinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Kamati ya Maendeleo na Huduma za Jamii.

Mheshimiwa Spika, mimi nitaanza kwanza kwa kushukuru Kamati zote mbili kwa kutoa maazimio mazuri kabisa ambayo yakitekelezwa yatatusaidia sana, lakini naomba nijikite sana katika suala zima la malezi ya vijana wetu, watoto wa kiume na watoto wa kike.

Mheshimiwa Spika, niishukuru jamii na Serikali kwamba tumeweka mkazo sana kwa Watoto wakike kiasi kwamba matokeo yake tumeanza kuyaona, matokeo mazuri kabisa sekta muhimu katika nchi hii zimekamatwa na wanawake hata Bunge letu, hata nchi na zinaenda vizuri kabisa. Hili ni jambo jema ambalo tumelifanya kama jamii.

Mheshimiwa Spika, lakini mimi nataka tu nisikitike kidogo, tumesahau kabisa malezi ya watoto wa kiume. Watoto wa kiume wamekuwa kama kuku huria wale wa kienyeji ambao wanajichungia tu, hawana mtu wa kuangalia. Mambo mengi sasa hivi tunayoyafanya tunamwangalia mtoto wa kike tu, tumesahau kabisa kama mtoto wa kiume ni sehemu ya familia. Hata wazazi tumeishafikia hatua ukifika nyumbani unauliza Glory yuko wapi? Hawa yuko wapi? Ukiambiwa wako ndani wanajisomea inashia hapo, huulizi Shabani yuko wapi wala Omari yuko wapi, hata wakija nyumbani saa tano usiku. Jambo hili limefanya watoto wa kiume sasa wamekuwa siyo responsibility kabisa kwenye familia na huko tunakoenda sasa tunaandaa bomu ambalo tutakuja kushindwa kabisa jinsi ya kulidhibiti.

Mheshimiwa Spika, mimi ningeomba Wabunge, hasa wanawake wajiweke zaidi kwenye uzazi, wasiweke kwenye ule kutetea haki za wanawake, jiweke kama mzazi una watoto wa kike na wa kiume, halafu uangalie huyu mtoto wa kiume jinsi ambavyo sasa ameachwa na baadae tutakuwa na Taifa ambalo sijui litakuwa na muunganiko wa namna gani? Kwa sababu tu ukisema unajenga mabweni utasikia watoto wa kike, ukisema sijui unataka kufanya nini watoto wa kike. Sasa watoto wa kiume inatokea hata mchango wao sijui tunaandaa nini?

Mheshimiwa Spika, kwa mila na desturi za kwetu na kwa dini zetu zote haitaondoa hata siku moja kwamba mtoto wa kiume ni kichwa cha familia. Sasa sijui tunandaa hiki kichwa cha familia baadae kitakuwa kichwa cha namna gani? Kwa sababu tutafika mahala tutakuwa na watoto wa kiume ambao ni useless kwenye jamii. Angalia matokeo kama ya panya road sasa hivi, matokeo mengine yote yanaonesha kabisa watoto wa kiume, hakuna watu panya road watoto wa kike hawapo, ni watoto wa kiume kwa sababu wamesahaulika na jamii na mtazamo kiasi kwamba sasa tunatengeneza bomu kubwa sana.

Mheshimkiwa Spika, mimi nataka niitake Serikali ije sasa na mkakati maalum wa kumrudia mtoto wa kiume iliko muacha, kwa sababu tunakoenda tunakwenda mahali pa hatari sana, tumemuacha mtoto wa kiume na dunia hii haiwezi kukamilika bila wanaume, haiwezi hata siku moja, yaani itafika mahala tutaanza kuwatafuta wanaume mahala waliko, hawana uwezo wa kuzalisha kwa sababu wameishashughulikiwa vya kutosha, kwa sababu wameachwa na tutafika mahala tutakuwa sijui tuna Taifa la aina gani.

Mheshimiwa Spika, niitake Serikali sasa ikumbuke kwamba hili ni bomu tunalitengeneza na si la utani na matokeo yake tumeishaanza kuyaona, wala hayana muda mrefu yata-backfire kabisa. Kwa hiyo mimi nafikiri sasa tukae kama wazazi…

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Mtinga kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa taarifa mchangiaji kwamba inawezekana ana hoja anaijenga, lakini kiuhalisia mtoto wa kike alikuwa ameachwa mbali sana, alikuwa katika marginal group hata ukiangalia makazini ratio ya wanaume kwa wanawake bado ni ndogo sana. Hata ukiangalia composition ya Mawaziri huku ndani wanaume kwa wanawake, Mawazari wako wengi sana, popote pale utakapoenda.

Kwa hiyo, nilikuwa tu nataka nimpe taarifa kwamba bado watoto wakiume hawajafikia kiwango cha kuwa kama ni vulnerable kama unavyosema. Bado mtoto wa kike anatakiwa apewe kipaumbele ndiyo maana Serikali inawekeza hata kwenye mashule na kwingineko kuweza kumnyanyua huyu mtoto wa kike sasa ambaye pia ni victim katika mambo mengi mengi hata ukatili ambao tunazungumzia humu ndani. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Francis unaipokea taarifa hiyo? Mheshimiwa Francis Mtinga.

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, huyu ni mate wangu tumesoma naye. Taarifa yake naipokea lakini mimi sijasema watoto wa kike hawana umuhimu; wana umuhimu mkubwa na ndiyo maana wanaongoza nchi leo na inaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachosema tumewasahau watoto wa kiume, tunatengeneza bomu la hatari, tutakapokuja kuwarudia hatutaweza, leo tumeweza kumchukua mtoto wa kike kwa sababu aliachwa, tumemfikisha hapa tulipofika, lakini jinsi tunavyomuacha mtoto wa kiume nyuma tutakapo mrudia hatutaweza ni bomu ambalo ni baya.

Mheshimiwa Spika, kwa mtoto wa kiume madhara ni makubwa, ameongelea ubakaji sasa watoto wa kiume wanalatiwa, sasa tunafika mahala…

SPIKA: Mheshimiwa Mtinga, hebu tuelewane kidogo hapo; ukiwa na watoto wawili mmoja wa kike, mmoja wa kiume kwa hali ilivyo sasa hivi utamlipia ada yupi kati ya hao wawili? (Makofi)

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, mimi kama baba nitalipia watoto wangu wote ada.

SPIKA: Haya huyo ni wewe; mzazi wako wa kizazi chake ulipokuwepo wewe mtoto wa kiume na mtoto wakike alikuwa anamlipia ada yupi? (Makofi)

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, historia inaonesha kwamba mtoto wa kike aliachwa nyuma, mimi sijakataa, na tumefanya juhudi kubwa kama Taifa kumkomboa mtoto wa kike na tumefanikiwa kiasi kikubwa. Nachofanya naikumbusha jamii...

SPIKA: Sawa sasa, ngoja tunaenda taratibu, ngoja kwanza.

Hoja yako ni nzuri na ni nzito, nataka ufike mahali unaposema kwa kumtazama mtoto wa kike mtoto, huyu mtoto wa kiume anaachwa nyuma wakati huyu wa kike mpaka sasa hivi kitakwimu yupo nyuma, anajaribu kusogezwa alipo huyu wa kiume na siyo kwamba wa kiume kaachwa, huyu msichana ameshampita huyo wa kiume halafu bado wa kiume kaachwa. Ni kwamba wa kike anasogezwa pale alipo wa kiume sasa, kama unazo takwimu tutaenda kwa takwimu, lakini aliyekupa taarifa hapa naye kaja na takwimu angalia hata humu ndani Wabunge wanawake wako wangapi humu ndani asilimia yao? (Makofi)

Wabunge wanaume humu ndani mko asilimia ngapi? Kwa hiyo, hoja yako ni nzito, lakini ujumbe unaoutuma ni kana kwamba mtoto wa kike ameshamkuta huyu mtoto wa kiume, ameshampita mtoto wa kiume, ameachwa wa kiume nyuma, hapana. Mtoto wa kiume bado yuko mbele anavutwa wakike amkute wakiume ili waende wote pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mtinga dakika moja malizia mchango wako. (Makofi)

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, mimi nafurahi jinsi ulivyomalizia umenielewa kwamba mtoto wa kike tumemfikisha mahala pazuri na tutaendelea, lakini watoto wa kiume tusiwaache nyuma kwa sababu tunatengeneza bomu ambalo litakuja kutushinda. Kwa hiyo nakushukuru. (Makofi)

SPIKA: Sawa.

Mheshimiwa Mtinga nilikupa dakika moja na haya makofi lazima ujue yanaonesha wingi wa wanaume humu ndani, ndiyo yanaonesha wingi wa wanaume humu ndani kwa sababu hakuna namna wanawake watapiga makofi yafikie ya wanaume. (Makofi)

Haya sekunde thelathini malizia mchango wako (Makofi)

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante naomba nimalize hoja yangu kwa kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wote hasa wanawake, wabebe nafasi ya uzazi zaidi tusiwe feminist, tukumbuke katika uzazi tunawatoto wa kike na wa kiume wote wanahitaji huduma ya jamii na huduma ya familia, ahsante. (Makofi)