Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Tecla Mohamedi Ungele

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii nami nichangie. Napongeza juhudi kubwa za Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza miundombinu katika afya, elimu na sekta nyingine, hilo tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu unajikita kwenye Wizara ya Elimu. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii. Taarifa ya Kamati imeainisha kabisa upungufu wa walimu kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nafuatilia hata taarifa ya leo, kwa mfano Wilaya ya Kilwa kule Mkoa wa Lindi, mahitaji ni walimu 1,406 wa Shule ya Msingi lakini waliopo ni 774, upungufu ni walimu 632. Hili ni tatizo kubwa. Nini maana yake? Upungufu wa walimu unaleta kuzorota kwa elimu na mwisho wa siku matokeo mabovu kwenye ufaulu wa wanafunzi. Kwa mfano, mwaka 2022 Wilaya ya Kilwa ni asilimia 75 ya wanafunzi walifaulu Darasa la Saba na ndiyo ilikuwa ya mwisho kwa Mkoa wa Lindi. Hii inasikitisha sana. Kama wengine walivyoendelea kusema kwamba ni changamoto, kukiwa na walimu wachache, kazi inakuwa kubwa.

Mheshimiwa Spika, kingine inasabisha utoro wa wanafunzi. Mwanafunzi anakuja, lakini hapewi kazi ya kushughulika. Kama tunavyofahamu, mwanafunzi huwa anashughulishwa. Wale walioko kwenye sekta ya elimu wanafahamu na wale walimu kwamba mwanafunzi lazima ashughulishwe. Ila kunapokuwa na uhaba wa walimu, mwanafunzi anakuwa wakati fulani hana chochote cha kufanya, basi anaona kesho yake wala kesho kutwa, wala mwezi ujao, asiende shuleni, maana anapoteza muda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nini matokeo ya upungufu wa walimu shuleni? Kunakuwa na utovu wa nidhamu kwa wanafunzi. Kama tunavyofahamu, walimu hawa ndio washauri wa watoto hawa, lakini kunapokuwa na uhaba wa walimu, inaleta utovu wa nidhamu kwa watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia upungufu wa walimu unaongeza uzito wa kazi, yaani kunakuwa na increased workload. Hii ndiyo inaleta msongo wa mawazo kwa walimu hawa. Hata kimwili mwalimu yule anachoka kwa kazi nyingi. Hata Wabunge wengine kwenye michango yao walisema kwamba hata maandalizi ya masomo pia, siyo tu suala la kusimama darasani ukafundisha, lakini kuna maandalizi ya masomo, pia kuna kusahihisha, kuna kumpa ushauri yule mwanafunzi baada ya kusahihisha. Hili yote tunawapa kazi walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho wa siku unaweza ukakuta hata vitendo vingine vya walimu, behavior nyingine wanazokuwa nazo walimu shuleni, na hata wakaleta mazingira fulani ya kuwafanyia ukatili fulani watoto hawa tunaowapeleka, ni kwa sababu ya upungufu wa walimu, pia msongo wa mawazo na ndiyo hiyo inaathiri hata afya ya akili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili tusipoliangalia huko tunakokwenda walimu watakuwa na changamoto ya afya ya akili, watoto watakuwa na changamoto ya afya ya akili, hata wazazi na jamii pia. Kama tunavyoona viashiria vinavyoendelea sasa hivi. Sasa tusifike huko. Naamini kabisa tunaweza tukanusuru jambo hili. Ni wakati umeshafika kwa Wizara yetu ya Elimu pia na Wizara husika ya kuajiri, hebu tuangalie tuweke mkakati, kama siyo ajira zile permanent, basi hata za mkataba ili angalau siku hadi siku inaendelea kupunguza tatizo hili la stress, na kadhalika, hata matokeo ya wanafunzi kufanya vibaya katika mitihani yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni hayo tu nilikuwa nayo katika sekta hii ya elimu na ninashukuru sana. Ninaamini mamlaka husika imesikia, itafanya maboresho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)