Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon Ally Juma Makoa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kondoa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE ALLY J. MAKOA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi tena ya kuja kumalizia hoja yangu. Kabla ya hapo, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge ambao wamepata nafasi ya kuchangia kwenye hoja ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii. Tulipata Wabunge 11 ambao walichangia hoja yetu. Ninawashukuru sana kwa michango mizuri na nimeona michango mingi imeendana na mapendekezo na ushauri wa Kamati ambapo Kamati yangu ya Ardhi, Maliasili na Utalii imetoa kwa Serikali.

Mheshimiwa mwenyekiti, mambo machache tu ya kufafanua. Unajua kama Kamati tuliona deal la Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kama limekubali vile baada ya programme ya Royal Tour na ndiyo ikapelekea kushauri baadhi ya mambo katika Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wajumbe wengi wamechangia kuhusiana na taasisi hizi za Wizara ya Maliasili, TANAPA, TAWA na NCAA Mamlaka ya Ngorongoro kwamba ziongezewe fedha ili ziweze kufanya majukumu yao kulingana na hali ya sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mfano tu kwamba TANAPA Bunge hili liliweka lengo la kukusanya shilingi bilioni 257.5 kwenye bajeti lakini wakati tunapitia utekelezaji wa bajeti TANAPA mpaka kipindi cha December ilikuwa imeshakusanya shilingi 2,051,000,000 ambayo ni sawa na asilimia 97 ya tengo lote. TAWA walikuwa na lengo la kukusanya shilingi bilioni 63.8 lakini mpaka kufikia kipindi hiki cha nusu mwaka wameweza kukusanya kwa asilimia 62. Ngorongoro walikuwa wana shilingi bilioni 148, hadi kufikia nusu mwaka wamekusanya shilingi bilioni 98.5 ambayo ni sawa na asilimia 66.6.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeyasikia maneno ya Mheshimiwa Dkt. Mwigulu hapa kwamba ukitaka kuvuna lazima upande. Ndiyo maana ile ile kwamba tunasisitiza Serikali izihudumie vizuri hizi taasisi ili ziweze kufikia malengo ambayo Mheshimiwa Rais anayategemea. Ndiyo maana yeye mwenyewe ameamua kujitoa katika kuhakikisha Wizara hii inatoa mchango unaostahiki kulingana na hifadhi zote na nyingi tulizonazo katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wajumbe wamezungumzia pia suala la mkopo wa Shilingi bilioni 345. Kamati iliona iko haja ya malengo yale yale yaliyowekwa na Wizara ya kuboresha mfumo wa ILMIS pamoja na kuimarisha mpango wa ardhi. Kamati iliangalia kwa undani sana suala hili na iliweza kupata maelezo kutoka Wizarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Kamati tuliona, kama tungeweza kuongeza upangaji wa vijiji, maana yake tungekuwa na faida ya kwamba kwanza tutaondoa migogoro katika nchi hii; na pili, tutaboresha data base za Wizara katika kila Mkoa kama maeneo yetu yatapimwa; tatu, tutakuwa tumetekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi; nne, tutakuwa tumetimiza Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano; tano, itajibu maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoweza kuyatoa katika Bunge hili kwamba, Wizara ya Ardhi ihakikishe kwamba inapanga matumizi bora ya ardhi nchi nzima ili kurahisisha na kuondoa urasimu kwa wawekezaji wanapokuja nchini kuwekeza katika sekta ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haya yote tuliyaona na tukaona ni muhimu sana. Hata kama Wizara ingeamua kuvipima vijiji vyote ambavyo vilibaki, pesa ambayo ingetumika ni Shilingi bilioni 145, ambapo Wizara ingebaki na Shilingi bilioni 200 ambayo ingeweza kupangia majukumu mengine ya kuimarisha mfumo na vitu kama hivyo. Haya yalikuwa ni mawazo tu ya Kamati na ndiyo tumeyaleta mbele ya Bunge lako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali iendelee kuangalia haya mapendekezo ili kuweza kufikia malengo ya kuipima nchi yetu yote ili kuondokana na migogoro ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema haya, nakushukuru tena wewe na niwashukuru Waheshimiwa Wabunge na sasa ninaomba kutoa hoja.

MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.