Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami naomba nianze kwa kuwapongeza sana Wenyeviti wa Kamati ambao wamewasilisha taarifa siku hii ya leo. Kipekee kabisa naomba nimpongeze Mheshimiwa Kihenzile kwa kazi njema anayoifanya pamoja na Wajumbe wa Kamati yetu ya Viwanda, Biashara na Mazingira. Kwa kweli, niwashukuru sana kwa maelekezo, kwa mashauriano, lakini ushirikiano mwema ambao tumekuwa nao ndani ya Kamati yetu katika utendaji wetu wa kazi. Niwaombe sana tuendelee kushirikiana kwa maslahi mapana ya Taifa letu kwani tunatambua uchumi wa Taifa letu unajengwa kwenye msingi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema haya, naomba pia, niseme sisi kama Wizara kwa niaba ya Serikali tumepokea maoni yote, lakini pamoja maelekezo yaliyotolewa na Kamati yetu ndani ya wasilisho lao siku hii ya leo. Ushauri wao tumeupokea, kama ilivyo kawaida tutaendelea kushirikiana katika kuufanyia kazi. Tutaendelea kukumbushana wapi tuimarishe zaidi ili tuweze kusafiri salama katika safari ya maendeleo ndani ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, naomba niseme mambo mawili tu. Moja, ni lile tuliloanzanalo, mradi unganishi wa Liganga na Mchuchuma. Kamati yetu imekuwa na maelekezo mazuri tu ambayo kama Serikali tumeendelea kuyafanyia kazi na tulikofika ni sehemu nzuri. Niombe tu Kamati yetu, kama ambavyo wametuelekeza tuharakishe ili tuweze kufanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua umuhimu wa chuma, tunatambua umuhimu wa makaa ya mawe katika uchumi wa dunia kwa sasa, yalipigwa marufuku, lakini walewale waliopiga marufuku wameyarejea kunyumenyume makaa ya mawe na bei yake imeongezeka duniani. Tunatambua kama Serikali na tunakwenda pamoja katika milima yetu ile ya Liganga na Mchuchuma tufanye kazi kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kusema asubuhi dhamira ya Serikali ni njema katika kuhakikisha rasilimali hizi za Taifa ambazo tumebarikiwa na Mwenyezi Mungu ziweze kulinufaisha Taifa letu. Tunapoongelea jambo hili niwashukuru pia, nirejee Mheshimiwa Ole-Sendeka na Mheshimiwa Nyongo, walisema vema kuhusu mkataba ule ambao tunakiri Serikali iliusaini,tunakiri wala hakuna anayepinga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokuwa tumeusaini ule mkataba na ikagundulika kuna makosa yalifanyika, ni wazi kosa moja haliwezi kuzalisha kosa la pili. Lazima turekebishe ili tusafiri pamoja na mradi huu uweze kuwa wa mafanikio kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoendelea kulifanya jambo hili niwaombe, sisi kama wawakilishi wa wananchi, tuitambue dhamira hiyo njema ya Serikali yetu kuhakikisha miradi yetu yote ya msingi inalinufaisha Taifa letu. Tumefika pazuri, kama nilivyosema, tunafanya kazi vizuri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuhakikisha mkataba huu ambao tuliusaini tunapouvunja tusije tukaliingiza Taifa letu kwenye mgogoro mwingine. Kwa hiyo, ndio maana nimesema tumepokea maelekezo ya Kamati tutakwenda nayo kwa umakini ili tuhitimishe vyema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kidogo tu niseme, Mheshimiwa Askofu Josephat Gwajima amesema vyema kabisa wala hakukosea, lakini nimkumbushe Mheshimiwa Gwajima, tulisema kwenye Kamati mwekezaji huyu hatukatai tulisaini mkataba, lakini baada ya kusaini mkataba tumegundua tatizo, tumemwita njoo tuongee. Ameitwa zaidi ya mara tano na Serikali, hakuwahi kutokea, sasa huyo tutasema kweli bado tumbebe ni mwekezaji? Hapana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maslahi mapana ya Taifa tutasema hapana, kama kweli ni mwekezaji aje mezani tukae tuongee kwa pamoja. Pale palipofanyika makosa tuparekebishe, tuendelee kama kweli yuko serious na mkataba huu. Kama ataendelea kugoma na sisi kama Serikali tunaendelea kukusanya taarifa kutoka kulekule nchini kwake, tumtambue sawasawa kama bado kweli ni mwekezaji, then Serikali itafanya maamuzi sahihi ambayo hayataliumiza Taifa wala mwekezaji mwenyewe hataumizwa kwa sababu, tumeshampa nafasi ya kutosha ya kumwita tukae mezani, lakini amekuwa hatokei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, juu ya hili nisisitize tu maelekezo ya Kamati yako. Walituelekeza kwa sababu, tumechelewa muda mrefu, mwaka jana tumeelekezwa, ni vizuri basi tuendelee mbele kuwalipa fidia wananchi wa eneo lile. Serikali ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ni sikivu, tumepokea na kabla ya kulipa tukakubaliana humu humu Bungeni lazima tukafanye uhuishaji wa taarifa ile ya uthamini kwa sababu, ilifanyika mwaka 2015 ili tusivunje sheria tunapowalipa wananchi wetu.

Mheshimiwa mwenyekiti, tumekamilisha kazi ya uhuishaji wa taarifa ile ya uthamini ambayo mpaka sasa Serikali iko tayari ndani ya miezi hii miwili tunakwenda kuwalipa wananchi wetu baada ya uhuishaji wa taarifa yao.

WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya uhuishaji wa taarifa yetu hii ya uthamini wa wananchi wetu, tunatambua kama Serikali na bajeti tunayo. Bajeti tuliyonayo ni Shilingi 15,979,788,646.50. Hii ndiyo thamani sasa tunayokwenda kuwalipa wananchi wetu ili hata tutakapotaka kwenda kuingia kwenye majadiliano na mwekezaji yeyote tuwe eneo lile hatuna tena mgogoro na wananchi. Ni Serikali ya Mama inayosikiliza wananchi wake, na tayari kazi hii tumeshaihitimisha. Niwahakikishie wanakamati pamoja na Bunge letu Tukufu tuko makini, tutahakikisha miradi yetu yote ambayo ipo kwenye rasilimali za Taifa letu ziweze kuwanufaisha wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo napenda kulisemea, imeongelewa Kampuni moja ya SICPA. Kampuni hii ina mkataba, ninavyotambua kule Mamlaka ya Mapato, namwachia Mheshimiwa Waziri wa Fedha ataiongelea, lakini kampuni hii isichanganywe. Kampuni hii ilipokuwa na mkataba na Serikali ambapo ikimaliza kazi yake ituachie Watanzania, ilikuwa ni kwenye uzalishaji wa vinasaba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye uzalishaji wa vinasaba, kampuni ilimaliza mkataba wake na tuliwaongezea mwaka mmoja na bei ilipungua kutoka kwenye kinasaba kimoja ambacho kinawekwa kwenye lita 1000 za mafuta kutoka Dola nane mpaka Dola mbili kwa mkataba wao wa mwaka mmoja. Kwa nini tuliongeza mwaka mmoja?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliongeza mwaka mmoja kwa sababu ilikuwa watufundishe sisi TBS tuweze kuzalisha kinasaba chetu wenyewe. Tayari hatua ya kwanza kinasaba cha TBS kimeshapitishwa na taasisi zote za viwango na ndani ya miezi sita tunahitimisha na tunafunga mkataba na SICPA kwenye uzalishaji wa vinasaba. Ni Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara na ubunifu uko ndani yetu, tumeshazalisha kinasaba chetu. Hatutaingia tena mkataba na kampuni hii kwenye uzalishaji wa vinasaba vinavyowekwa kwenye mafuta yanayoingia ndani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tusichanganye mambo haya mawili. Maana kampuni hii imeitwa ni wezi; hapana ndugu zangu, tulipotoka tusirudi. Twendeni tufanye kazi na Kampuni zetu. Kampuni haziwezi kuwa mwizi kama sisi hatujawa wezi. Kwa hiyo, kama sisi tumekubali kuukataa wizi na makampuni yetu ya kibiashara hawawezi kuwa wezi. Nasi tumeamua, Serikali ya Awamu ya Sita tumeanza na kinasaba chetu, tuko tayari. Ndani ya miezi sita tuko sokoni na wala hatuhitaji tena kuingia mkataba na yeyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitamani niseme hayo mawili. Nakushukuru sana kwa fursa hii. Naiomba Kamati yetu, ushirikiano wetu ndiyo mafanikio yetu ndani ya Wizara na Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)