Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza awali ya yote kwa niaba ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira naomba kuishukuru Kamati yetu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, lakini Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kwa kuwasilisha taarifa hiyo ambayo zimetufikia kama vile kwa niaba ya Wabunge, lakini zikijaa hoja mbalimbali ambazo kama vile ni maelekezo kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumshukuru sana Comrade Kihenzile Mwakiposa kwa kazi kubwa wanayoifanya katika Kamati yetu ya Viwanda, Biashara na Mazingira pamoja na Makamu Mwenyekiti Ndugu yangu Eric Shigongo, lakini na Wajumbe wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa Waziri wa Mazingira naomba niishukuru kwa dhati Kamati hii, kwa sababu kwa kipindi chote Kamati hii imekuwa ikitoa maelekezo kwetu kwa lengo ya kusaidia sana utendaji wa kazi za Serikali na mimi hapa naomba nikiri wazi kwanza, yale maazimio yaliyopendekezwa na Kamati tutayachukua kwa lengo ya kufanyia kazi kwa mustakabali mpana wa kuhakikisha Tanzania yetu katika upande wa mazingira inaendelea kufanya vizuri. (Makofi)

Kwa hiyo, sina jambo lolote kuhusu zile hoja za Kamati mimi naomba nizipokee kwaniaba ya Serikali tutaenda kuzifanyia kazi kwa kadri kama tulivyofanyia kazi yale ya nyuma yaliyopita, niwashukuru Wajumbe kwa kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wajumbe hawa kwa upande wangu mimi ofisini kwetu tunasema hawa wamekuwa ni walezi zaidi, wamekuwa lengo lao kuhakikisha kwamba lengo la kuishauri Serikali kwa kweli naomba nikiri wazi wamefanya kazi kubwa tena kwa ushahidi na hili ndiyo maana niseme kwa sababu hapa tumekutana Bungeni, Kamati hii toka ilipoundwa na leo tukijadili taarifa hii tunashuhudia kwamba sera mpya ya mazingira ambayo tulikuwa na sera ya mwaka 1997 Kamati hii imewezesha kutengeneza sera, kwa hiyo, Kamati nawashukuru sana Wajumbe wa Kamati kwa kwa hii kazi tuliyoifanya kubwa, lakini tunajua kwamba kuna Mpango Kabambe wa Usimamizi na Utekelezaji wa Mazingira ambao Waziri Mkuu mwaka 2022 aliuzindua mpango wa miaka kumi, kazi hii imefanywa na Kamati kwa karibu zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikwambie jambo moja kubwa, Kamati hii tunafahamu kwamba katika hoja za kipindi cha nyuma maelekezo ya Kamati ilielekeza Serikali tuje kutekeleza mpango wa kuhakikisha jinsi gani tunaenda ku-access biashara ya hewa ya ukaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikuhakikishie kwamba leo hii sasa Tanzania tumeshakuwa na mwongozo pamoja na kanuni za biashara ya hewa ya ukaa na hili ni kubwa sana kama hatufahamu, na malengo yetu ni kwamba kwa sasa ukiangalia mazingira kama hayana mchango mkubwa unaoonekana katika suala zima la pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikuhakikishie ndani ya miaka michache tunaweza tuka-notice kwamba biashara ya hewa ya ukaa huwenda zaidi ya shilingi trilioni moja kwa mwaka ikaingia kwa biashara ya hewa ya ukaa na niwaombe ndugu zangu Wajumbe tupitie kanuni na miongozo hii, itasaidia sana sana hasa katika suala zima la kuhakikisha maeneo yetu jinsi gani tunayaelekeza kuhakikisha tunavuna sasa faida kubwa za nchi yetu hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kanuni yetu hii, imeenda mbali, kwa maelekezo ya Kamati kanuni iliyotengenezwa, sasa TFS itaweza ku-access fedha nyingi, misitu iliyokuwa inatunzwa ambayo wakati mwingine wakati mwingine ilikuwa inatumika kwa ajili ya kukata mkaa, sasa itaweza kuingia katika biashara ya hewa ya ukaa. Hili ni jambo kubwa la kihistoria, lakini leo hii reference katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ambayo kwa mwaka saa hizi wanapata wastani kati ya shilingi bilioni mbili mpaka bilioni tatu na humu mnafahamu Halmashauri zingine kwa mwaka hata kuanzia mapato yote haifika hata bilioni mbili. Sasa tutakuja kuifungua nchi hii katika kila Halmashauri ambayo yenye misitu yake itaenda kujihusisha na biashara ya hewa ya ukaa. Hili ni jambo kubwa niishukuru sana Kamati kwa maelekezo yake, hapa tulipofikia na mahala pazuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara hii itagusa TFS, itagusa taasisi mbalimbali, itagusa Halmashauri, itagusa watu wenye misitu yao, lakini hata agro-forestry watu waliyopanda mimea kwa mfano mikorosho, miparachichi na kahawa, yote yataingia katika biashara ya hewa ya ukaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni faida kubwa sana ambayo imani yangu kubwa ndani ya miaka michache tutaona mchango wa biashara ya hewa ya ukaa katika Taifa letu hili ambayo mimi naamini jambo hili ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Kaka yangu Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah, mwana mazingira mzuri sana mbobevu wa siku nyingi, nashukuru sana ushauri wako mara nyingi sana unakuwa unatusaidia sana sisi na umetoa ushauri kwamba ikiwezekana tufanye nyongeza ya pendekezo la kuhakikisha kwamba ikiwezekana kila Wizara iwe na dawati kabisa la mtu wa mambo ya climate change (mambo ya mazingira).

Mheshimiwa Mwenyektii, bahati nzuri sana katika sheria yetu kifungu namba 30, lakini vifungu namba 33, 34 na 35. Kifungu 30 kinatoa mwongozo wa uundwaji wa madawati katika suala zima la Wizara za Kisekta, lakini kifungu namba 33 kinatoa mwongozo kila Wizara kiwe na dawati la mtu wa mazingira na climate change na kifungu cha 34 kimetoa mwongozo kwa mikoa yote na kifungu cha 35 kimetoa mwongozo katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa, mwaka jana lilizungumzwa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikuhakikishie tulitoa maelekezo yapi? Leo hii naomba nikuhakikishie Halmashauri zote 184 tuna huyu mtu katika dawati tayari, lakini mikoa yote 26 na Wizara zote na hili nishukuru sana katika mkutano uliyofanyika mwaka huu, tunashukuru kwamba zaidi ya watu hamsini kutoka Taasisi za Serikali hawa ni watu wale focal person waliweza kushiriki katika mkutano wa climate change mwaka huu.

Kwa hiyo, niseme kwamba jambo hili bahati nzuri limeishafanyika, kwa hiyo, kazi kubwa sasa sisi ndani ya Serikali kuhakikisha vitengo hivi tunavipa nguvu zaidi viweze kuwa na bajeti ya kutosha kuhakikisha ajenda ya mazingira inaenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba kwa ujumla naomba niwashukuru sana Watanzania. Leo kwa mara ya kwanza unapita mitaani unakuta watu wana matoroli wanauza miti mitaani, ilikuwa haipo jambo hili. Hili sasa limetoke nchini mwetu na mimi niliwaambia wenzangu kwamba sasa tutafika mahali tuwahamishe ngedere na tumbiri warudi mijini tuweze kuhakikisha miti inapandwa katika maeneo ya miji na hili naamini tunakokwenda na hasa nikishirikiana na Dada yangu Mheshimiwa Pindi Chana katika suala zima la Maliasili kule na tumejiwekea mikakati ya kutosha kwamba wenzetu kupitia TFS jinsi gani tunahakikisha upandaji wa miti katika suala zima la miji yetu tupate suala zima la miti ya matunda na miti mbalimbali iweze kupandwa. Ndugu zangu ajenda ya mazingira ni ya kwetu sisi sote, niwaombe Watanzania tumeshuhudia wanyama wakifa kule Longido, kule Simanjiro na Kiteto hali ya ukame ilikuwa kubwa sana, tuna kila sababu kutunza mazingira, kila mtu a-feel jambo hili kwamba ni jambo la kwake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tumeshuhudia vyanzo vya maji Bwawa la Mtera ambalo linaloweza kuzalisha megawati 80; lile la Kidatu kwa megawati karibu
204 zilishusha uzalishaji wake kutokana na ukame, tusipofanya hivi kila mtu kuguswa na mazingira tutakuwa tumeiweka nchi yetu katika hatari kubwa sana.

Niwaombe Watanzania tuungane pamoja, niishukuru sana sasa hivi watu birthday wanasherekea kwa miti, kila jambo ni jambo la miti, tuungane watanzania wote tuhakikishe ajenda ya mazingira ni ya kila mmoja wetu kwa ajili ya kuinusuru nchi yetu Mama Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)