Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya mimi kuchangia hizi Wizara. Kwanza nawapongeza Wenyeviti wote wa Kamati ya Viwanda na Kamati ya Maliasili na Utalii, wamefanya vizuri na wametupa taarifa za kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea mimi nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa dhana yake ya Royal Tour. Maana tunapozungumza Maliasili sasa Watalii wamesukuma hela za kutosha kwenye nchi yetu na maeneo yetu ya hoteli porini kule yamejaa. Zamani wakati Mheshimiwa Rais anafanya hili jambo, watu wengi waliona mchezomchezo lakini matokeo yake sasa mwenye macho haambiwi tazama. Iko wazi kabisa kwamba ile dhana imetoa matunda ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa kitendo chake na dhana yake ya kuanzisha ile Tume ya Haki Jinai ambayo sasa itatazama utendaji kazi wa maeneo mbalimbali ya taasisi zetu Polisi, Magereza,TAKUKURU na Kitengo cha DPP. Kwa hiyo, hii dhana ni nzuri sana tutazame kitu gani tunapata haki kwa namna gani. Kwa hilo wazo tu la kuanzisha hiyo Tume ya Haki, nampongeza sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijikite kwenye hoja zetu na sasa nianze na TANAPA, TAWA na Ngorongoro. Toka Awamu ya Kwanza ya Urais ambayo yote ni ya Chama cha Mapinduzi suala la TANAPA, TAWA na Ngorongoro tumekuwa tukiwaachia mapato yao kwa ajili ya kulinda hifadhi zetu za Taifa ambao ni urithi wetu wa Taifa. Kwa sababu ya Corona hiyo 2019 ikabidi mapato yao yarudishwe kwenye Hazina kwa maana kwamba watawasaidia kupeleka bajeti, kwamba mapato yao yamepungua kutokana na Watalii kutokuja nchini. Sasa naona ni wakati muafaka wa kuwapa mapato yao kwa sababu vitendo vinavyoendelea sasa hivi, hata ule wingi wa mifugo kwenda porini, lakini pia kutolipa vizuri malipo ya kifuta machozi, hii dalili kwamba mapato kutoka Hazina kwenda TANAPA, TAWA na Ngorongoro imekuwa shida sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uendeshaji wao umekuwa wa shida mno, hawawezi kufanyakazi kwa kusubiri takwimu zitoke na hela zitoke Hazina waandike voucher, waende wapige sijui mfumo umekataa, sijui kitu gani, mambo mengi tu yametokea. Kwa hiyo, tunaomba sasa bajeti hii inayokuja na Wizara ya Fedha ielewe wazi kwamba bajeti yao itapita endapo watakubali fedha za TANAPA na TAWA ziende zikafanye kazi ya kulinda maliasili zetu ambazo ziko pale ndani. Kwa hiyo nafikiri kwamba hili ni wazo ambalo Kamati imelileta na sisi tunaliunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo la pili, ninataka nizungumzie pongezi za watu wa Ngorongoro kuhama kwa hiari lakini kwa kuwapa haki zao. Sasa wakati naipongeza Ngorongoro kwa haki hizo, niende kwenye vijiji vitatu vya Wilaya ya Bunda ambavyo ni Nyatwali, Serengeti na Tamao vinahamishwa na TANAPA kwa hiari, kwa sababu vile vijiji vina registration ni haki yao kukaa pale. Lakini style inayotumika kuhamisha vile vijiji haifanani kabisa na style inayohamisha watu kutoka Ngorongoro, wakati wazo ni lile lile. Kwa hiyo, mimi naomba sasa vile vijiji vitatu vipewe haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, juzi wamekuja Mawaziri nane kwenye maeneo yale. Wale watu wanadai tuwape milioni 3.5 badala ya Milioni Mbili kwenye heka moja, kwa hiyo tunaomba kama haki zote haziwezi kufanana lakini at least bei halisi, thamani ya ardhi yao ipande kutoka milioni mbili kwenda milioni nne ili wapate haki sawa waweze kuhama kwenye maeneo yao ambayo ni haki yao, registration wamepata na ni haki yao kuishi pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba sana Serikali ya Mheshimiwa Mama Samia, ni Serikali yetu ya CCM ninaomba sana ifikirie jambo hili, kutoa watu kwenye maeneo waliokaa kwa miaka mingi na kuwapa thamani ndogo ya ardhi, wanahama wanalia, wanatoa machozi siyo vizuri sana kufanya jambo kama hili, tunaomba tufikirie namna ya kuongeza thamani ya valuation ya ardhi yao ili wapate haki sawa na watu wengine walivyohamishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye chombo kinaitwa ETS, sasa hapa niende kwa sauti ndogo. ETS wanaita ni Electronic Tracking System ambayo inaendeshwa na kampuni ya SICPA. Kampuni hiyo ililetwa na TRA kwa maana ya Serikali kwamba isaidie kukusanya mapato yetu, mimi naipenda sana ile kampuni kwa sababu inatuonesha mapato yako wapi! Lakini system inayotumika kuilipa ile kampuni ndiyo siipendi. Kwa sababu ile kampuni inapata bilioni 75 kwa mwaka na ina watumishi 15 tu na hakuna mahali bilioni 75 inaenda. Bilioni 75 inakusanywa na kampuni inaenda, inapelekwa nje hakuna mahali hiyo hela inaenda kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo matatizo makubwa ya madawati kwenye shule za msingi, bilioni 75 zinaenda, kwa nini ziende? Kama ni hivyo, hizo hela kwa nini sasa tusitengeneze mpango ikawa Serikali inatumia kidogo kwa ajili ya kufanya maendeleo? Mbaya zaidi hizi fedha zinalipwa na makampuni ya kwetu. Makampuni ya uzalishaji, makampuni ya Viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati kampuni inaingia kulikuwa na kampuni 19, wakaongeza bei ikawa bei kubwa kiasi hicho, sijui dola 18.6, sijui wanaita kwa track 1,000, lakini kwa sasa tunayo makampuni yamefika karibu 51, naambiwa ni 27, kama ni hivyo mpango wa hiyo kampuni ilikuwa ilete vile vifaa, ile mitambo iliyokuwa nayo baadae baada ya miaka mitatu ibaki na Serikali, ibaki na TRA ndiyo wakusanye. Kwa nini mpaka sasa hiyo mitambo ipo na inakusanywa na mtu wa SICPA, kuna nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukigusa maeneo hayo unataka kuuawa kuna nini hapo? Nataka kuuliza Mwenyekiti kuna nini hapo? Kwa nini watu wanakusanya bilioni 75 wanapeleka nje sisi tuna matatizo makubwa kiasi hicho. Nilikuwa nafikiri tulitazame hili jambo vizuri tuone linakwendaje.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka tu kumpa taarifa mzungumzaji ya kwamba TCRA walikuwa wanamfumo unaitwa TTMS kwa ajili ya kuratibu simu zinazoingia hapa nchini na kuratibu kazi zote za kampuni za simu. Mtambo huo uliwekwa na mwekezaji baada ya muda ameukabidhi Serikalini. Alichozungumza mzungumzaji hapa nakiunga mkono kabisa hawa walioweka mtambo wa ETS, kama muda umefika wauwasilishe Serikalini na Serikali ndiyo waendelee kukusanya kama walivyofanya TCRA.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita Getere unaipokea hiyo taarifa?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naikubali kwa mikono mitatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiomba ni kwamba kampuni ile kwa maana ya mfumo wao wanafanya kazi nzuri sana lakini fedha inayolipwa na wawekezaji, makampuni halafu mbaya zaidi mpango wa kulipa hiyo fedha unapangwa na TRA. Wao wanapanga wameleta mtu atusaidie kukusanya mapato ni sawa, lakini malipo yao hata hawa-share. Unapanga na TRA na ela zinakusanywa zinaenda kwenye hiyo kampuni, sasa tunajiuliza kwa nini hiyo Kampuni kama imemaliza muda wake, hizo fedha zisikusanywe ziingie Serikalini halafu Serikali ione namna ya kumlipa huyo sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini akusanye yeye, kuna mpango gani kwa huyu mtu mkataba wake umeisha halafu bado anakusanya hela? Kwa hiyo, mimi nasema mpango wake na kampuni yenyewe, mfumo wenyewe ni mzuri sana, system ya kukusanya hela ndiyo tunaiwekea mashaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye upande wa ardhi, ninaiomba tu Serikali iiongeze Wizara ya Ardhi hela, suala la migogoro ya ardhi ni mingi sana.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE NA URATIBU): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE NA URATIBU): Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango mzuri ambao Mheshimiwa Getere anautoa, isije ikaenda kwenye public kama vile fedha hii ambayo kampuni hii inalipwa ni fedha ambayo ilitakiwa ilipwe Serikali, isije ikaenda hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kimsingi ETS inasaidia kudhibiti productions ya products nyingi zinazozalishwa kwa mara moja kama soda au juice au bia zile ‘tatatata’ inagonga zile alama. Kwa hiyo, ile inamsaidia kwanza mwenye kiwanda kuweza kujua bidhaa zake amezalisha kiasi gani kwa ajili ya usalama na kujua kiwango alichozalisha, kwa hiyo inadhibiti. Ni system ambayo inadhibiti, pia inaisaidia Serikali kujua kilichozalishwa ili iweze kuchukua kodi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, isije ikaonekana kwamba fedha hii ambayo inalipwa ilikuwa ni fedha ya Serikali, ni fedha ambayo Serikali kwanza inapata faida ya kujua kilichozalishwa ili iweze kudai kodi yake, pia mwenye kiwanda anapata faida ya kudhibiti uzalishaji wake. Kwa hiyo, siyo fedha ya Serikali ila tu hoja yake inabakia tu kwamba mbona hizi fedha zinachukuliwa na makampuni na zinapelekwa nje kutoka ndani ya viwanda vyetu? Sasa hilo ni jambo jingine.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Getere unapokea hiyo taarifa.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa ameeleza vizuri, hoja hatujasema kwamba hiyo kampuni haifanyi vizuri, inafanya vizuri. Hoja ya kujiuliza ni kwamba ni kwa nini Serikali imeleta hiyo kampuni kusaidia mapato ya Serikali lakini mipango yake ya malipo inatokana na wazalishaji wenyewe? Kwa nini wawawekee wazalishaji mzigo mkubwa wa kulipa malipo ambayo wao hawakushiriki kufanya malipo hayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna kampuni zingine zenye bei nafuu zinazoweza kufanya kazi kama hiyo hazitakiwi kwenye hii nchi, kwa nini? Kwa hiyo hilo jambo liwe hivyo? Tunayo mashaka na hilo eneo lifuatiliwe. (Makofi)

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ole-sendeka taarifa.

T A A R I F A

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kumpa taarifa rafiki yangu humu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuambie mahusiano yaliyopo kati ya SICPA na baadhi ya Wizara ambayo inafanya kazi nayo ni mahusiano ambayo siyo ya kawaida. SICPA ilishindwa tenda kadhaa katika vinasaba ilipokuwa inashindanishwa na kampuni zingine ikabebwa mara mbili na muda wake ulipoisha wameendelea na fedha walizokuwa wanazikusanya hawajalipa kodi na Serikali haioni, ni uchochoro mwingine katika swala la vinasaba vya mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili lilizungumzwa na Mbunge wa Gairo na hakuna mtu aliyetoa maelezo yaliyojitosheleza. Pale kuna ufisadi, Serikali iangalie na ilete taarifa kwenye Bunge hili juu ya ufisadi wa SICPA na walivyokuwa wanabebwa kama watoto wapendwa katika mradi huo na mkitaka ushahidi nitawaletea walivyoshindwa tenda zote na zote wakabebwa, SICPA hiyo! (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita Getere unaipokea taarifa hiyo.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naikubali kwa mikono miwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua kuna vitu vinaletwa, yaani sijui kuna nini sasa! Kwa sababu tumeshakaa Kamati ya Viwanda, Kamati ya Fedha, Kamati ya Sheria tukazungumza hilo tatizo, tukalitolea maamuzi kwamba huyu mtu aangaliwe upya...

MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa ya mwisho hiyo.

T A A R I F A

MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa taarifa mzungumzaji kwamba mkataba wa SICPA pia uliisha muda wake na Kamati tulishauri Serikali kwamba wasitishe kuendelea kupata huduma kutoka kwa SICPA kwa ajili ya gharama zao ni kubwa, zipo kampuni ambazo zinazo uwezo wa kufanya huduma kama hiyo kwa bei ya punguzo la asilimia 70 chini ya ambayo SICPA anaendelea kuitoa. Kwa masikitiko makubwa ushauri wa Kamati yetu haukuzingatiwa SICPA muda wake umeisha lakini mpaka sasa hivi bado wanaendelea kufanya huduma hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni zetu nyingi za Kitanzania zinalia sana, kila mtu analia hawana msaada. SICPA wanaiibia nchi yetu, wanasababisha mfumuko mkubwa wa bei kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita Getere unaipokea hiyo taarifa?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea lakini kwa maelezo kwamba hatutaki SICPA itoke, ila kama kuna mbadala wake uje. Tunataka bei ya SICPA ipungue kwa wazalishaji wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)