Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuwa machangiaji wa kwanza. Ni-declare interest kwamba ni Mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii. Kwa maana hiyo, naunga mkono mapendekezo yote ambayo yamesomwa mbele ya Bunge lako siku ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, natamani nikazie mambo kadhaa ambayo tumeyaweka kama maelekezo na maagizo, na mwishoni yatakuwa maazimio ya Bunge hili Tukufu. La kwanza ni zoezi hili la kuhamisha watu; wananchi walioridhia kuhama eneo la Ngorongoro kuhamia eneo la Msovela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo matatu ambayo tumeyaweka kwenye taarifa yetu. La kwanza ni Serikali kupitia Wizara ya Ardhi kuhakikisha inaharakisha kufuta GN ambazo kimsingi zinakwamisha uendelezaji na upangaji wa matumizi bora ya ardhi ya eneo la Msovela kwa ajili ya kuhakikisha wale wananchi wanaohamia pale hawapati usumbufu wowote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni Serikali kuhakikisha angalau inatoa fedha kwenye kaya zaidi ya 1,500 ambazo zimeridhia kuhama. Ila sasa Wizara ya Maliasili na Utalii inapata changamoto hiyo kwa sababu ya upataikanaji wa fedha. Nichukue nafasi hii kuwashukuru; sina maana kwamba hawajafanya kazi, kwani wamefanya kazi kubwa na nzuri sana, lakini Serikali iharakishe ili kuona namna gani hawa wananchi ambao wameridhia kwa mapenzi yao wanahamia haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ni maboresho ya sheria ya eneo la Ngorongoro ili angalau mwishoni tupate matumizi bora ya eneo lile kuondoka kwenye eneo la matumizi ya mseto na kuwa na matumizi ambayo ni sawa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la nne ni mradi wa Seven Eleven wa Kawe. Mradi huu ni wa Shirika la Nyumba; na kama tulivyosema kwenye Kamati, Serikali imekuwa ikipata hasara kubwa sana kupitia huu mradi. Kwa sasa umesimama na mkandarasi anadai zaidi ya Shilingi bilioni 44, hiyo ilikuwa ni mwezi Januari. Mpaka sasa ukienda deni ni zaidi ya Shilingi bilioni 54, na tunavyozidi kuchelewa kutatua mgogoro huu kila mwezi fedha hii inaongezeka. Tunatamani sana Serikali iingilie ione namna ya kuingilia mgogoro huu iweze kuumaliza na tusiendelee kupata hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tano ni TANAPA. Mwaka 2019 TANAPA walikuwa na hifadhi wanazozisimia 16, lakini kuanzia 2016 tukaongeza hifadhi sita, sasa hivi wana hifadhi 22. Usimamizi wa hifadhi hizi ni mgumu sana, tulikuwa tunaomba angalau Serikali waweze kuongeza fedha ili watu hawa waweze kuendana na ongezeko hili la hifadhi ambalo tumeliongeza kwenye maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo hapa ambapo kimsingi natamani sana Bunge hili na Kiti chako kiweze kuweka msisitizo. Kuna jambo ambalo kimsingi linagusa maslahi ya Taifa hili. Nasi kama Kamati tumelileta ili angalau litoke kama azimio kwa ajili ya utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mradi wa uboreshaji wa usalama wa milki za ardhi ambao Serikali kwa maana ya kupitia Wizara tumepewa mkopo wa USD milioni 150. Kwa fedha ya Tanzania ni zaidi ya Shilingi bilioni 345, lakini lengo la fedha hizi lilikuwa: moja, ni kuimarisha usalama wa taarifa za ardhi; pili, ni kuimarisha miundombinu na upimaji; tatu, kujenga majengo ya ofisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunasema kupitia Kamati, tunadhani fedha hizi maeneo zilikopelekwa fedha hizi ambazo ni za mkopo, hazina tija moja kwa moja na mashiko kwenye maslahi mapana ya Taifa na wananchi na lengo kubwa la kutatua migogoro ya ardhi nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Bunge hili, tunao Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao kimsingi 2020 mpaka 2025 unasema tuwe tumepima asilimia 50, tuwe tumepanga matumizi ya vijiji angalau asilimia 50 ya vijiji vyote. Leo tuna vijiji zaidi ya 12,319 tumepanga matumizi vijiji 2,600 peke yake, maana yake hatuendani na kasi ya mpango. Vijiji 2,600 ni toka uhuru, lakini toka 2020 vijiji vilivyopangwa havizidi 200 peke yake, maana yake hatutakidhi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunayo Ilani ya Chama cha Mapinduzi, inazungumza hivyo hivyo kwamba mwaka 2020 mpaka 2025 tuwe tumepanga matumizi kwa asilimia 50. Tuna vijiji hivyo 2,640, tunayo hotuba ya Mheshimiwa Rais. Mwaka 2021 hapa, Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo na dhamira yake ya Wizara hii kuhakikisha angalau inapanga matumizi bora ya ardhi katika maeneo mengi ili kutoa ukakasi na urasimu kwa wawekezaji wanaokuja kuwekeza ndani ya nchi. Yote hii inaendana na kasi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, ni Wabunge namna ambavyo tumekuwa tukichangia humu ndani ya Bunge. Migogoro mingi ya sekta ya ardhi inasababishwa na kutokuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi ngazi ya vijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili liko wazi, kila Mbunge akisimama kuchangia humu ndani atakwambia namna mgogoro uliopo kati ya wakulima na wafugaji, namna mgogoro uliopo kati ya muwekezaji anayekuja kuwekeza na mwananchi, namna mgogoro uliopo kati ya mwananchi na mwananchi, namna mgogoro uliopo kati ya maeneo ya hifadhi na wananchi husika kwenye eneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, solution ya kuondoa haya yote, ni kupanga matumizi bora ya ardhi katika maeneo yote. Sasa sisi toka uhuru tumepanga matumizi vijiji 2,640. Kamati inasema nini kwenye hili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tumepata fedha zaidi ya Shilingi bilioni 345 na hapa wameelekeza kupanga matumizi vijiji 250 peke yake, Kamati inasema, kwa kuwa vijiji vilivyosalia 9,670 havijapangwa na havijaelekezwa mpango wa matumizi bora ya ardhi. Fedha hii ya mkopo ielekezwe zaidi ya asilimia 50 kupanga matumizi bora ya ardhi nchi nzima. Hii itakuwa ikakidhi haya manne niliyoyasema. Inakwenda kutekeleza mpango wa maendeleo, itatekeleza hotuba ya Mheshimiwa Rais, itatekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, na pia itakuwa inajibu yale maombi ya Bunge hili, namna bora ya kutatua migogoro ya nchi yote kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ningeomba sana kwa msisitizo. Ukipiga vijiji 9,600 vilivyosalia, mpango wa matumizi bora kijiji kimoja ni Shilingi milioni 15 peke yake. Nilikuwa naangalia kwenye mkopo wetu tuliokopa sisi; Shilingi bilioni 345 unatakiwa utoe Shilingi bilioni 145 peke yake kwenda kutatua na kutengeneza historia ya nchi hii kwa kupanga matumizi bora nchi nzima. (Makofi)

Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, hii ndiyo inaweza ikatutengenezea historia ya nchi hii kwa mara moja kupanga vijiji 9,600 kwa wakati mmoja. Kwa sababu toka uhuru tuna vijiji 2,600 peke yake, badala ya hizi fedha kuelekezwa kwenye maeneo ambayo kimsingi tukiyatazama hayana tija. Mfano, nitayasema maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi, ukichambua namna ambavyo Wizara maeneo ambayo inakwenda, ni fedha ya mkopo. Tunaelekeza fedha hizi mathalan kwenda kuandaa leseni za makazi zaidi ya milioni moja. Sipingani na hili, lakini tunakopa na tumeelekeza zaidi ya Shilingi bilioni 160 kwenye utekelezaji wa zoezi hili; tujiulize, leseni ya makazi ina-expire kwa miaka mitano peke yake. Taifa hili tumefikia mahali tunaelekeza mkopo wa Shilingi bilioni 160 kupeleka mahali ambapo baada ya miaka mitano ina-expire. Yaani baada ya miaka mitano, mnarudi kutafuta fedha nyingine kupanga eneo, fedha ya mkopo wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa natamani, kama tuna mpango wa kuboresha leseni za makazi, isitoke kwenye bajeti na isionekane fedha ya mkopo inakwenda maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tumeelekeza fedha hizi kutoa semina kwa watumishi zaidi ya Shilingi bilioni tano. Tumeelekeza fedha hizi, kufanya valuation ya rates ambazo ziko sokoni.

Ndugu zangu, anayetaka kununua kiwanja, rate ya square meter moja ya kiwanja au unataka kununua nyumba; square meter moja ya nyumba inakuwa determined na soko lenyewe linavyokutana kati ya mhitaji na mnunuzi. Hatuna sababu kama Serikali kukopa Shilingi bilioni tano kuelekeza kwenye maeneo ambayo rate yake inakuwa determined na soko husika. Yaani tunakopa fedha kupeleka Shilingi bilioni tano mahali ambapo tunaweza kutumia fedha za mradi kuelekeza kwenye maeneo hayo. Haileti tija yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumekopa fedha, angalia kwenye huu mkopo, tunatenga contingency (fedha ya dharura) bilioni 17 kwa ajili ya kuja kulipa mkopo, hizi fedha zote ambazo naziainisha hapa tulikuwa tuna uwezo wa kuzipeleka na kukubaliana kama Bunge na kutoa maelekezo angalau Serikali iweze kupitia maeneo haya ya huu mkopo waende wakapange matumizi bora ya vijiji vyote nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hii nje tu ya kuondoa mgogoro, nje tu ya kwamba itakuwa imetatua mgogoro wa ardhi nchi nzima, lakini itakua; moja, imeongeza thamani ya ardhi maeneo yote nchi nzima; pili, kwa kutengeneza mpango bora wa matumizi ya ardhi, mwananchi mmojammoja atakwenda kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili kwa sababu tumelisema sisi na tumeliona kwamba lina ukakasi kidogo kwa namna maelekezo ya hii fedha inapokwenda, tunaomba Bunge hili kwenye maazimio tuishauri Serikali iweze kupitia upya mkopo huu na iende kwenye maeneo ambayo yana tija, iende kwenye maeneo ambayo yanamgusa mwananchi moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wananchi wetu kule wanapigana kati ya wakulima na wafugaji, wanaondolewa maeneo ya hifadhi. Kwa nini tusiende kupanga matumizi bora ya ardhi ya vijiji hivyo? Tunatengeneza historia leo kwa miaka mitano kuonekane tumepanga matumizi ya vijiji 9,600 wakati miaka 50 ya uhuru tumepanga…

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi tumeshauri, tunaomba Bunge hili angalau muweze kuona ili fedha hii iende kwa maslahi mapana ya Taifa. Nashukuru sana. (Makofi)