Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia jioni hii ya leo. Nami nianze kwanza kuwapongeza Wenyeviti wa Kamati ya Miundombinu, Mwenyekiti wa Kamati ya Maji, Kilimo na Mifugo kwa taarifa zao nzuri ambazo wameziwasilisha hapa Bungeni.

Mheshimiwa Spika, nami ni Mjumbe wa Kamati ya Maji, Kilimo na Mifugo. Niungane na wajumbe wenzangu kwanza kukubaliana na hoja ambazo zimeletwa na Kamati.

Mheshimiwa Spika, tumeweza kutembelea miradi mingi sana iliyopo katika kamati yetu. Miradi mingi tumekuta kuna baadhi ya changamoto ambazo ziko katika miradi ya maji. Kwa mfano tulienda katika mradi ule wa maji wa Mwanza. Tulikuta Serikali inajitahidi kupeleka fedha lakini fedha zinakuwa hazipelekwi kwa wakati. Kwa hiyo, changamoto yake tunakuta kwamba miradi haikamiliki kwa wakati lakini pia miradi inapokamilika inaongezeka gharama zake kwa sababu kwanza kabisa wale wakandarasi msipopeleka fedha kwa wakati kunakuwepo na penalty katika ile miradi. Kwa hiyo, tunajikuta kwamba miradi mikubwa tunatekeleza kwa gharama kubwa sana. Kwa hiyo, nilikuwa ninaiomba Serikali katika hii miradi ambayo inatekelezwa mikubwa hasa ya maji, fedha zipelekwe kwa wakati ili hii miradi iweze kutekelezwa kwa wakati na kusiwepo na ongezeko.

Mheshimiwa Spika, vilevile niendelee kuchangia kuhusiana na Wizara ya Maji, nilikuwa naomba tuwe na Sera ya Uvunaji Maji ya Mvua kwa sababu kumekuwa na mvua nyingi sana katika nchi yetu kwa baadhi ya mikoa ambazo hizi mvua sasa zinasababisha hata mafuriko, zinasababisha uharibifu mkubwa sana wa barabara zetu hasa za vijijini. Kwa hiyo, kukiwepo na Sera ya Uvunaji Maji maana yake maji yatakwenda kwenye ile mikondo au watatengenezewa mabwawa makubwa ambayo baadae sasa yatakuja kufaidisha kwamba yatasaidia hata umwagiliaji katika miradi ya kilimo lakini vile vile yatasaidia hata bajeti ya barabara za vijijini zitapungua.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu tumekuta kwamba barabara nyingi za vijijini zinaharibika kutokana na mafuriko ambayo yanasababisha barabara nyingi kuharibika kutopitika wakati wa mvua, lakini barabara nyingi na madaraja mengi yanasombwa wakati wa mafuriko yale ya maji, kwa hiyo, sasa kama tutakuwa na sera ya uvunaji maji ya mvua utasaidia sana hata bajeti ya utengenezaji wa barabara ambazo zinakwenda katika vijiji vyetu. Kwa hiyo, miundombinu itakuwa mizuri kwa sababu wananchi wataweza kupata maji kwa wakati na vilevile tutaweza kufaidika kwamba barabara nyingi hazitatengenezwa kila wakati.

Mheshimiwa Spika, pia naomba nizungumzie kuhusiana na kilimo cha mboga mboga na matunda. Serikali niipongeze imeweza kuhamasisha sana kilimo cha matunda na mboga mboga na hasa hata hizi parachichi. Nilikuwa naomba tulivyotembelea tumekuta kuna changamoto nyingi sana kwamba kamati yetu ilikuwa inaomba sasa Serikali ifanye miundombinu kuwepo na miundombinu kwa ajili ya usafirishaji wa haya mazao katika airport zetu na katika bandari zetu. Vilevile itenge eneo maalum la green belt katika bandari zetu ili iweze kusafirishwa kwa uhakika. Tumeona kwamba nchi kama Kenya wanakuja kuchukua kwa mfano parachichi kupeleka kwenye nchi zao na matokeo yake sasa wao kwa sababu wana miundombinu rafiki katika airport zao wana miundombinu rafiki katika bandari zao, unakuta hata parachichi zetu wanazichukua na kwenda kuona kwamba wao ndiyo wanaozisafirisha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe pia Serikali hiyo logistic za usafirishaji hata barabarani unakuta bado haya mazao yakisafirishwa askari wanayasimamisha kiasi kwamba hakuna logistic nzuri za kusafirisha haya mazao.

Mheshimiwa Spika, vilevile tulivyotembelea katika baadhi ya taasisi tumekuta kuna changamoto ya wafanyakazi. Hawa wafanyakazi wamekuwa wakipata mikataba ya kufanya kazi katika taasisi hizo, mfano tulivyotembelea shamba la ASA kule Arusha, tumekuta wafanyakazi wanapewa mikataba kufanya kazi katika hayo mashamba lakini linapokuja suala la ajira unakuta wale wafanyakazi ambao tayari wameweza kujengewa uwezo mkubwa unakuta ajira ikija hawaajiriwi. Kwa hiyo, Serikali inaajiri wafanyakazi wapya kabisa kiasi Serikali inakuwa haifanyi vizuri sana, wanakuwa wanaanza upya kuwafundisha.

Mheshimiwa Spika, pengine sasa uwepo mkakati wale wafanyakazi ambao tayari wamepewa mikataba na wana uwezo wa kufanya ile kazi wapewe kipaumbele cha kuendeleza ule mradi ili isiwepo wakati wa ajira, wale ambao tayari wameshafanya pengine miaka miwili au mitatu hawapatiwi ajira, hilo lingeangaliwa.

Mheshimiwa Spika, pia nipongeze kazi nzuri ambayo inafanywa na Wizara ya Maji na Wizara ya Kilimo katika miradi ambayo tumeipitia. Kwa mfano tulikwenda kwenye miradi ya Dar es Salaam tumekuta kwa kweli kulikuwa kuna upungufu mkubwa hakuna mtu ambaye hakai Dar es Salaam. Changamoto zilikuwa nyingi sana. Pia wana changamoto ya wafanyakazi. Unakuta kwamba wafanyakazi wengi wanapewa mikataba lakini wakati wa ajira bado unaona wana uwezo wa kuwalipa wale vijana lakini Serikali inachelewesha zile ajira kiasi kwamba sasa wangekuwa pengine wangeweza kukusanya mapato mengi sana lakini wanakuwa mapato yale hayakusanyiki kwa sababu ya uhaba wa wafanyakazi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, pengine hilo nalo lingepewa kipaumbele hizi mamlaka zenye uwezo wa kuajiri vijana basi waweze kuajiriwa kwa wakati ili waweze kufanya kazi ambayo watakusanya mapato kwa wakati.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele ya pili Mheshimiwa.

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, ninaunga mkono hoja zote.