Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Yustina Arcadius Rahhi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nami nafasi hii niweze kuchangia taarifa nzuri sana ya Kamati ya Kilimo, Mifugo na Uzalishaji maana taarifa imejieleza vizuri.

Mheshimiwa Spika, Watanzania bado tuna- cerebrate, tunaona maono ya nchi yetu sasa ni kwenda kutufikisha pale ambapo maazimio yetu; Azimio la Malapo, Azimio la Maputo siku moja tunakwenda kuifikia asilimia 10 kuwekeza katika sekta hizi za kiuchumi ili tuweze kuimarisha uchumi wetu. Kwa sababu nyongeza ya bajeti hii mpaka bilioni mia tisa na kitu ni sawasawa na na asilimia 1.8 ya bajeti kuu. Tunategemea bajeti tunayoenda pengine tutasogea kwenye trilioni mbili na kuendelea.

Mheshimiwa Spika, kutenga bajeti ni kitu kingine, lakini utoaji wa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo pengine ikawa ni tatizo. Nasema hivyo kwa sababu kwa bajeti ya maendeleo hadi kuifikisha tarehe 31 Desemba bajeti hii ya kilimo imeweza kutekelezwa kwa asilimia kumi na tisa na pointi. Kwa hiyo, naiomba Serikali yangu sasa kama tumeazimia kweli kuwekeza kwenye kilimo basi Serikali iendelee kutoa fedha ili miradi hii ya kilimo iliyotengewa fedha ipate kutekelezwa.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo niseme tu kwamba changamoto kubwa kwenye miradi hii ya kiuchumi yote kilimo, mifugo na uvuvi, changamoto kubwa tulikwishasema ni uzalishaji mdogo na tumeona sababu mbalimbali. Kwa mfano kwenye kilimo ilikuwa ni upatikanaji wa pembejeo kwa ajili ya bei, pamoja na kuweza kufikika kwa muda. Lakini vilevile kilimo cha kutegemea mvua ikiwepo pamoja na matatizo ya utoshelevu wa ugani.

Mheshimiwa Spika, safari hii Serikali imewaunga mkono wananchi kwa kuweza kutoa ruzuku kwa pembejeo ya kilimo ambayo ni mbolea. Pamoja na changamoto lakini tumeona nia nzuri ya Serikali jinsi ambavyo itaenda ku-solve haya matatizo yaliyotokana na usambazaji wa mbolea ya ruzuku. Hii tunaiachia Serikali, imekwisha weka utaratibu maghala yote ya Halmashauri ambayo yapo yatapelekewa mbolea kwa muda. Nafikiri kwa musimu unaokuja mbolea itasambazwa kwa vya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo tumeona impact, toka ruzuku imewekwa katika mbolea, matumizi ya mbolea yamepanda sana na kama kweli Serikali ingewahisha kwa awamu nyingine maana mbolea nyingi iliyotumika ni ya kupandia, pengine mbolea ya kukuzia ikafika kwa muda, tutaona kwamba kuna ongezeko kubwa sana la mbolea ya viwandani ambayo wakulima walikuwa hawajakubali hiyo teknolojia.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo tunajua kwamba kuna tatizo kubwa la upatikanaji wa mbegu na ni kwa sababu asilimia kubwa ya mbegu tunazotumia kwa zaidi ya asilimia 60 zinatoka nje hasa kwa mahindi, tunatumia zaidi mbegu za Seedco, Decay, Pan, Pioneer, Zamseed zote hizi tunaziingiza kutoka nje na mbegu hizi ni ghari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali ikae na iangalie namna gani inatoa unafuu katika upatikanaji wa mbegu na kwa bei nafuu. Nasema hivyo ili Serikali iweze kutoa bajeti. Ilitenga shilingi bilioni 43 kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu na bajeti hii mpaka tarehe 30 imetekelezwa kwa asilimia 35.

Mheshimiwa Spika, katika kuzalisha mbegu tunaomba Serikali iwezeshe taasisi ya ASA pamoja na vituo vya utafiti iweze kuwajengea miundombinu hasa miundombinu ya umwagiliaji ili mbegu hizi uzalishaji wa mbegu pia tusitegemee mvua. Tuhakikishe kwamba kuna miundombinu ya kutosha ili tuweze kupata mbegu za kutosha wananchi na zile mbegu zinazotakiwa. Kwa hiyo tunaomba Serikali iendelee kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa upatikanaji wa pembejeo za kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia niseme kwenye umwagiliaji; changamoto kubwa imekuwa ni kutegemea mvua. Tunajua kilimo cha watanzania kinatekelezwa na wakulima wadodgo wadogo kwa asilimia 90. Pia wakulima kila siku wanabaki kwenye dimbwi la umasikini kwa sababu ya kutegemea zaidi mvua. Kilimo ni ghari, mkulima atalima kwa gharama kubwa, atanunua pembejeo kwa gharama kubwa, ametimiza wajibu wake, lakini mwisho wa siku kama mvua zitakuwa haba ndio inaishia kwenye mazao yake kukauka. Kwa hiyo, kwa vyovyote vile inamrudisha kwenye njaa na kwa vyovyote vile inamrudisha kwenye umaskini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaomba kwa kipindi kilichopita Serikali imetekeleza kweli miradi ya umwagiliaji midogo midogo ya kukarabati scheme. Sasa tutegemee tena baada ya bajeti kutoka shilingi bilioni 46 mpaka shilingi bilioni 361 sasa ikawekeze kwenye miradi mikubwa ya umwagiliaji ambayo itasaidia wananchi iweze kusogea sasa kutokutegemea mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu mwingine ni kuhusu mifugo; tumeona pia chanagamoto kubwa sana kwenye mifugo na tatizo la mifugo ni kuwa na uzalishaji mdogo vilevile. Mifugo ya Tanzania inakumbwa na upungufu mkubwa wa malisho na maji, lakini na magonjwa. Tunaomba sasa Serikali iendelee kuchimba mabwawa pamoja na kuimarisha malisho kwa ajili ya mifugo. Fedha zilizotengwa kwa ajili ya malisho shilingi bilioni 8.5 mpaka mwezi Desemba ilikuwa imetolewa hela kidogo sana kama shilingi milioni 100.

Mheshimiwa Spika, tuwasaidie pia wafugaji, wamekuwa wakihangaika na wakihama kutoka sehemu moja hadi nyingine. Kwa nini sasa nyanda za malisho zikaendelea kutambulika, zikawekewa GN kama ilivyo maeneo ya hifadhi na maeneo mengine ili wafugaji hawa wasiendelee kuhangaika. Tunaiomba Serikali iwasaidie wafugaji watoke hapo, lakini vilevile na magonjwa. Magonjwa yamekuwa ni tatizo kubwa, Serikali iendelee kujenga majosho ili mifugo iogeshwe, kwa sababu magonjwa mengi ya mifugo yanatokana na Magonjwa yanayosababishwa na kupe na tunatumia fedha nyingi za kigeni ambazo tunategemea takribani bilioni 100 kununua dawa kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano kwa chanjo, ni kwa nini tusiimarishe kituo chetu cha Kibaha kikaweza kutengeneza chanjo za kutosha na kupeleka chanjo kwa wafugaji? Tumekuwa tegemezi. Vilevile tumeua veterinary centers ambazo zilikuwepo katika kata, wafugaji wamekuwa wakihangaika wakitibu mifugo yao wenyewe bila kuelewa na ndio maana tunapata usugu wa magonjwa ya mifugo.

Vilevile huko kwenye Halsmashuri unaweza ukakuta Halmashauri kadhaa haina hata daktari wa mifugo. Hebu sasa Serikali ikawekeze kwa sababu kweli Tanzania tuko proud kwamba sisi ni wa pili kuwa na mifugo mingi baada ya Ethiopia, lakini Tanzania bado sisi tuna-suffer na udumavu, Tanzania hatu-export mazao yoyote ya mifugo badala yake bado tunaingiza mazao. Sasa kama tumekubali kuwekeza kwenye mifugo tuone matokeo makubwa ili na sisi sasa tuwe na mifugo iliyo bora, tuweze kupeleka mazao ya mifugo nje kuweza kupata fedha za kigeni na kuongeza GDP. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na ahsante kwa nafasi. (Makofi)