Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi kupata nafasi ya kuweza kuchangia mada zilizoko mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, ninapenda tu kuiuliza Serikali kwa wenzetu wa TANROADS. TANROADS katika bajeti ambayo tuliipitisha katika Bunge lako Tukufu ni asilimia 24 tu peke yake zimeweza kutoka kwa ajili ya kufanya kazi, katika asilimia hizo 24, asilimia 7.2 ndiyo zimejenga madaraja, kwa hiyo barabara nyingi sana katika Taifa hili zinachelewa sana kujengwa.

Mheshimiwa Spika, barabara ndiyo maendeleo, wewe unaona wakati wajumbe hapa wakiuliza maswali ya barabara zao kwenye Majimbo. Usipokuwa na barabara imara na usipokuwa na barabara wakulima hawawezi kufanya chochote kwa sababu bidhaa zinapanda, barabara hazifikiki na wale wakulima hawafikiwi mapema. Ninapenda kujua kwa Serikali na hasa Wizara ya Fedha, kwa nini fedha haziendi kwa wakati ili kuweza kuwasaidia hawa watu?

Mheshimiwa Spika, nilijaribu kuuliza wakasema kipindi cha manunuzi labda kinachukua muda mrefu, labda ifike wakati hata Sheria ya Manunuzi iweze kubadilika, kwa sababu kuna baadhi ya miradi inachelewa kwa sababu zile Sheria zinamlolongo mkubwa sana, kama ikibidi basi Serikali ilete ile sheria upya turekebishe ili mambo yaweze kwenda kwa kasi kama tunavyotaka ili mambo yaende. Barabara ni kilio kikubwa sana kwa Wabunge kwenye majimbo yetu, barabara hazipitiki, barabara zimekuwa zinachukua muda mrefu sana kwa usanifu, mchakato na lugha kama hizo, tunahitaji kubadilika.

Mheshimiwa Spika, misamaha ya kodi kwa TANROADS. TANROADS inapotaka kufanya kazi, misamaha kwenye Wizara ya Fedha inachelewa kutoka na hii inapelekea wasiweze kufanya kazi kwa haraka. Kwa hiyo, tunaomba Serikali isimamie hilo ili tuweze kuwasaidia ndugu zetu. Kwa upande wa TANROADS hao hao, naomba utaratibu wa kupima mabasi kwenye mizani nafikiri nia ilikuwa njema hapo zamani, lakini sasa hivi basi linajulikana linabeba abiria kiasi gani, basi likishapima mwanzo likapime na mwisho hapa katikati wasipime kwa sababu inaongeza msongamano na foleni kwenye barabara. Kuna wakati mabasi yanakaa masaa mawili hadi matatu yakisubiri kupimwa, mimi nafikiri uchumi ni muda, unapopoteza muda uchumi pia unapotea. Kwa hiyo, ninashauri ikiwezekana wenzetu wa TANROADS waruhusu mabasi yapimwe mwanzo wa barabara na mwisho wa barabara hapa katikati kama wanafikiri wanaongeza mizigo kwa magari mengine ni sahihi lakini kwa mabasi nafikiri abiria wanapata shida sana, kwa hali hizi za kupima mizani inachukua saa nzima masaa mawili watu wako kwenye foleni.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la TCRA, kumekuwa na shida kubwa sana ya utapeli kwenye simu. Message zinazoingia kwenye simu bila mteja kukubali kupokea message. Kwa mfano, mganga maarufu kutoka sehemu fulani, wanapata wapi hizo namba, wanafanyaje? Kwa hiyo, tunaomba TCRA itusaidie. Siyo hivyo tu, wanatuma meseji ninaamini Viongozi hapa tunapata message wanasema kuna shida kuna kitu fulani nitumie, ukituma tuma kwenye namba hii na usipojitambua labda mwenyekodi alikudai ukajichanganya ukatuma hela imeondoka. Tunaomba watusaidie TCRA na hasa Serikali ikiwawezesha TCRA kuweza kusimamia majukumu yao na kuhakikisha wanazuia huu wizi wa mitandao ambao umekuwa ni mkubwa sana.

Mheshimiwa Spika, ninafahamu Waziri anaehusika amesimamia vizuri hili kuhusu uzimaji wa laini. Zipo laini nyingi sana ambazo zimesajiliwa, zingine zimesajiliwa kwa njia ambazo jina la Mwakagenda lipo lakini siyo laini ya kwangu, amesema vizuri Mheshimiwa Waziri tunataka zizimwe na kweli zizimwe ili tuweze kujua walio genuine ni nani na ambao siyo genuine ni nani. Kwa hiyo, mimi naunga mkono suala la kuzima laini na hasa wale ambao hawajahakiki mjitahidi mhakiki ili msiweze kuzimiwa laini zenu.

Mheshimiwa Spika, ninaipongeza TBC kwa maana ya kwamba imejenga Studio mpya pale Dar es Salaam lakini na Dodoma pia na imeweza kufanya vizuri, tumewekeza pesa nyingi sana zaidi ya Bilioni Kumi, mwisho wa siku usipowekeza kwa wafanyakazi, unakuwa hujafanya lolote. Kwa hiyo, Wizara hii ihakikishe, pamoja na kutengeneza Studio zetu vizuri ikiwepo Radio Tanzania ile ya zamani wamei-modify imekuwa nzuri lakini wafanyakazi walipwe posho wanapokwenda kwenye kazi zao, kwa sababu wao ndiyo wanaolisaidia Taifa hili. Mheshimiwa Rais akienda mahali wanaenda, walipwe posho kwa wakati ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tupo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, tunaangalia channel za wengine, wafanyakazi wanavaa nguo nzuri kwa kudhaminiwa na maduka pamoja na makampuni. TBC inahitaji kufanya kitu kama hicho ili wafanyakazi wetu waonekane na mwonekano mzuri na waweze kufanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia usikivu mipakani kumekuwa na shida, huko bado kunahitaji kuongeza fedha kwa ajili ya kutengeneza mitambo tuweze kusikia habari za huku kwetu. Ukienda Tunduma, Kyela, Kyerwa na sehemu zingine kama Kigoma unakutana na redio za nje ya nchi ambazo ziko kwenye hizo sehemu. Unakuta redio Malawi inasikika Kyela, kwa hiyo tunaomba usikivu uweze kuongezeka. Pia wanahitaji OB Van, tunaamini Serikali itaongeza fedha kuhakikisha mitambo ya TBC inakuwa mizuri.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo nizungumzie kuhusu TBA. TBA ilipoanzishwa Sheria yao ilikuwa inataka kuhudumia tu mambo ya kiserikali na nyumba za kiserikali, sasa hivi tunaingia kwenye utandawazi, tulete Sheria Bungeni ili TBA waweze kufanya biashara, kwa sababu kama real estate kama watu binafsi wanatajirika, hata hawa watu tukiwawezesha wanaweza kufanya kazi vizuri sana. Kwa hiyo, naomba sheria iletwe ili TBA ibadilike na hawa watu waweze kukopa na siyo tu kukopa waweze kushirikiana na mashirika mengine wakaweza kujenga na kuisaidia Serikali kupata nyumba nyingi sana na zaidi ya yote tuweze kuhakikisha hata Wabunge wanaohitaji nyumba kama Dodoma waweze kupata kwa sababu hawa TBA wanahitaji fedha ili waweze kufanya haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, ninaunga mkono hoja za Kamati na mapendekezo ya Kamati ambayo wameyatoa katika Bunge lako, tunaamini Serikali itayafanyia kazi. Ahsante. (Makofi)