Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Deus Clement Sangu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa fursa hii ili na mimi niweze kutoa mchango wangu katika hoja iliyo mezani, hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza nichukuwe nafasi hii kuipongeza Serikali; mimi binafsi katika jimbo langu kwa mara ya kwanza tumeweza kupata fedha nyingi za maendeleo ambazo zinafikia takribani bilioni tisa. Ni rekodi kubwa, na mimi pongezi zangu za dhati za wanakwela zimfikie Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo nitoe tu ahadi kama Mbunge na Baraza langu la Madiwani tutasimama kidete kuwahakikisha fedha hizi zinafanya kazi iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili naomba nitoe mchango wangu, na nitaanza kuchangia katika sekta ya bandari. Bandari ni key driver ya uchumi ndani ya nchi. Sisi kama Tanzania tuna bahati, upande wa Mashariki wa nchi tuna Bahari ya Hindi ambapo tuna bandari, upande wa Magharibi ya nchi tuna Ziwa Tanganyika ambako ndiko kunapatikana Mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kumekuwa na sintofahamu ya muda mrefu. Hapa ameongea ndugu yangu Mheshimiwa Kandege, kwamba kati ya mikoa inayotajwatajwa kuwa na umaskini na hali duni ya maisha ni mikoa ya Rukwa, Katavi Kigoma na sisi tuna Ziwa Tanganyika ambalo tunapakana na nchi ambazo zina fursa ya kufanya biashara na nchi yetu kupitia ile mikoa mitatu. Kule tuna Burundi, DRC na Zambia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe tutaarifa. Juzi tu hapa kuna ugunduzi umefanyika wa copper ndani ya nchi ya DRC kule Katanga kuna deposit ya copper ambayo wanaweza wakafanya uchimbaji kwa miaka 100 ijayo. Sasa fursa pekee ambayo tunayo, wao wanategemea kusafirisha raw materials katika extraction ile ya copper ambayo ni sulphur ambayo wanaipitishia Bandari ya Dar es salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa taarifa tu ile biashara ya sulphur
ambayo wanapitisha Bandari ya Dar es salaam imeweza ku-trigger namba za mapato ndani ya mapato ndani ya Bandari ya Dar es salaam. Yale mapato waliyokuwa wanaweza kuyafanya kwa mwaka mzima kwa mwaka huu kwa mara ya kwanza wataweza kufikia ndani ya kota mbili kwa maana ya miezi sita. Ni achievement kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa shida ambayo imekuwa ni kikwazo biashara hii tusifanye vizuri na DRC ni mzunguko. Wakichukuwa mzigo huo Bandari ya Dar es salaam wanalazimika wapitishe Zambia ndipo waende Lubumbashi. Mzunguko mrefu sana ilhali sisi tuna short cut ya kupitia either Kasanga, Kalema ama Kigoma kwenda upande wa pili wa DRC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi mpaka tunavyoongea mwaka wa tatu tuna bajeti kwamba tunanunua meli. Ziwa Tanganyika hatuna meli, tangu Liemba iondoke kwenye matengenezo, tangu MV Mwongozo iondoke hatuna meli. Sasa, tutaweza ku-utilize opportunity hii ya DRC, iliyokuja, kwa namna gani? Wataanza kufikiria kutukimbia, wataenda Bandari ya Walvis Namibia au Beila kule Mozambique au wataamua kwenda Durban South Afrika. Sasa naomba, Mheshimiwa Waziri Mkuu tumewekeza kwenye Bandari zetu za Kasanga, Kalema pamoja na Bandari ya Kabwe. Sasa zile bandari kazi yake ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo hili ambalo hatuwezi pia pamoja kwamba bandari zitakamilika, upande wa pili wa kule DRC miundombinu ya barabara ni shida. Kutoka pale Moba upande wa pili kwenda kufika Lubumbashi ni kilometa 700, kilometa hizo hazipitiki. Kwa hiyo kama nchi lazima pia tufanye mazungumzo ya pamoja na nchi ya DRC kama wenzetu wa Uganda walivyofanya, tukaingia hata katika ubia wa kutengeneza barabara ili tuwende ku-utilise opportunity iliyoko ndani ya nchi ya DRC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Serikali, mikoa yetu hii itafunguka; leo hii bodi ya mazao mchanganyiko mmeanzisha ghala kule Lubumbashi, mahindi yetu yataendaje? Ina maana tutapitisha Zambia ndipo tukauze kwenye soko la DRC? Haiwezekani, hatuwezi tukategemea boti za watu binafsi kama nchi kusafirisha mizigo yetu ambayo inaenda ku-trigger uchumi wa mikoa mitatu kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tena, Mheshimiwa Waziri Mkuu, jambo ambalo mimi nimekuwa nikipata shida wakati huu, kumekuwa misconception ya kuchanganya kana kwamba Mkoa wa Rukwa na Katavi ni mkoa mmoja. Tayari mikoa hii imeshakuwa tofauti. Katavi wanajitegemea na Rukwa inajitegemea. Leo hii kuna mradi huu ambao tumepata fund kutoka kwenye European union agri-connectivity kwa ajili kutengeneza miundombinu ya barabara ku-support productivity kwenye kilimo. Mikoa yote ya Nyanda za Juu Kusini ipo, ikiwemo Katavi, lakini Rukwa wameturuka, sisi Wana-Rukwa tuna shida gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo niombe sana, tunapokuwa tunaangalia kwa upana namna ya kuweza, leo hii tumeongelea hapa, nimemsikia ndugu yangu hapa anaongelea habari ya uwanja wa ndege wa Sumbawanga. Ule uwanja wa ndege wa Sumbawanga ni miaka sita sasa, kila bajeti ipo; na nilivyokuwa namwona Mheshimiwa Waziri anajibu hapa nikatikisa kichwa, kwamba na mwaka huu wananchi tunaenda kuwaambia kwamba imo kwenye bajeti tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwaambie kama inashindikana mwaka huu kutekeleza ni bora tuiondoe kwenye bajeti ili tujuwe kwamba mwaka huu hatuna uwanja wa Sumbawanga. Niendelee kusihi sana asubuhi tulikuwa na jambo la mbolea limeongelewa na Mheshimiwa Waziri amejibu sana. Kama hatutafufua kampuni yetu ya mbolea Tanzania TFC tusitegemee kwamba suala la mbolea tutapata suluhu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeongea habari ya ruzuku, ni sawa, lakini mnapowapa nguvu private operator kwenye suala la mbolea ambayo ni sensitive kwa usalama wa chakula cha nchi ni shida. Hili shirika letu ambalo liko taabani tangia mwaka 2014 limekufa; na hili shirika si la juzi, limeanzishwa mwaka 1968 kwa dhumuni la kusaidia usalama wa upatikanaji wa mbolea ndani ya nchi; lakini tulilitwishwa mzigo wa madeni limekufa halipo kabisa. Kwa hiyo inatakiwa Serikali tuchukuwe hatua ya haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba tumeahidi kwenda kuweka ruzuku ili tupate mbalea nchini, nawasihi sana tuifufue Kampuni ya Mbolea Tanzania ili itusadie Watanzania wakulima maskini ambapo mwaka huu mbolea ni kilio cha nchi. Ukifika kule kwetu tumeenda mpaka 140,000 kwa mfuko mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa nafasi hii. Haya yalikuwa ya kwanga niliyotaka kuchangia katika Ofisi ya Waziri Mkuu ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)