Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Shamsia Aziz Mtamba

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Mtwara Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ili nami niweze kuchangia katika hotuba hii ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya nzuri na leo hii nikaweza kusimama katika Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilizungumza bajeti ya mwaka jana kuwa changamoto kubwa ambayo inatukabili hasa katika Jimbo langu kwenye masuala ya barabara ni barabara ya ulinzi ambayo imepita Kilambo – border kuelekea Kitaya mpaka Tandahimba. Barabara hii ni barabara muhimu mno hasa kwa usalama wa watu wetu pamoja na vyombo vyetu vya ulinzi. Hivyo, nilikuwa naiomba sana Serikali iingalie barabara hii kwa umuhimu wake na tunatambua hali ambayo inaendelea katika mipaka yetu kule, niiombe sana Serikali iweze kujenga barabara hii muhimu kwa kiwango cha lami ili vyombo vyetu vya ulinzi vinapofanya doria katika maeneo yale basi viweze kufika kiurahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna barabara ya uchumi ambayo inatoka Mtwara Mjini kuelekea Msimbati ambapo kuna mitambo na visima vya gesi, barabara hii nayo imesahaulika. Barabara hii ni mbovu sehemu ambapo tuna mitambo ya gesi kule barabara ni mbovu na haipitiki kabisa hasa kipindi cha masika. Hivyo, ninaiomba sana Serikali iangalie barabara hii ya uchumi ijengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa changamoto kubwa ambazo zinatukabili wananchi wa Mkoa wa Mtwara ni suala la maji, suala hili la maji bado limekuwa sugu sana katika Mkoa wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna chanzo kikubwa cha maji chanzo cha Mto Ruvuma, niiombe sana Serikali itumie chanzo hiki cha maji cha Mto Ruvuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015 uthamini ulishafanyika kwa wananchi, wananchi wangu wa Mtwara Vijij,ini hawaelewi wamenituma niwaulize chanzo hiki cha maji mtatumia lini na lini mradi huu utaanza? Maana wananchi wanashindwa kuendeleza maeneo yao kutokana na kutokulipa fidia mpaka leo.

Mheshimiwa Waziri wa Maji ninakuomba utakapokuja mbele kwenye majumuisho utueleze mradi huu ni lini utaanza na lini wananchi hawa watalipwa fidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la bandari. Bandari ya Mtwara ipo Tanzania wala haipo nchi jirani, lakini kwa masikitiko makubwa sana bandari hii imesahaulika bandari hii imesahaulika. Serikali imewekeza fedha nyingi sana katika bandari hii ya Mtwara lakini imesahaulika na haifanyi kazi ipasavyo. Hivyo, ninaiomba sana Serikali katika msimu wa mwaka huu tunataka kuona bandari ya Mtwara inafanya kazi ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka kuona korosho yote ya msimu ya mwaka huu inatumia bandari yetu ya Mtwara. Pia tunayo kila sababu ya kuitumia bandari hii kwa sababu tuna mizigo, mizigo ambayo itatoka Malawi inaweza kupitia bandari hii ya Mtwara, pia tuna cement ya Dangote inaweza kutumia bandari hii ya Mtwara. Leo hii barabara ya Lindi – Dar es Salaam ni mbovu kila siku inafanyiwa matengenezo kutokana na uharibifu wa malori ambayo inaharibu barabara hii. Serikali kama mngekuwa mnatumia bandari ya Mtwara leo hii barabara yetu isingekuwa inatengenezwa mara kwa mara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kupepesa maneno nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea viuatilifu kwa wakati kwa wakulima wetu wa korosho. Nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri naye sitamtendea haki kwa kulisimamia suala hili mpaka leo hii kutuletea viuatilifu vya korosho kwa wakati kwa wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kitu kimoja tupange utaratibu wa kugawa viuatilifu hivi ili kuondoa mkanganyiko ambao ulijitokeza kwenye msimu uliopota. Ninaiomba Serikali ni lazima kuwe na takwimu katika ugawaji wa viuatilifu hivi na takwimu maalum za kila mkulima ili wakulima wote waweze kupata viuatilifu hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya nikushukuru sana. (Makofi)