Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon Salim Mussa Omar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Gando

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SALIM MUSSA OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu muumba mbingu na ardhi na vilivyomo kwa kutujaalia tumefika hapa tukiwa hai na wazima. Pili, ninakushukuru wewe kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee leo nitajikita katika suala zima la maafa katika ukurasa 69 na ukurasa wa 70 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka juzi mwaka 2019 nilipata fursa ya kwenda kutembelea museum tatu nchini Marekani, ikiwemo ya Titanic Museum iliyoko pale Branson, pamoja na World Trade Centre iliyoko pale New York pia JF Kennedy iliyoko Texas.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matukio haya yalinipa msisimuo wenye mfanano sawa na baadhi ya matukio yaliyotokea ndani ya nchi yangu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na janga la Titanic lilotokea na kupelekea kufariki kwa watu takribani 1,500. Tukio hili linafanana na ajali ya boti yetu ya MV Spice iliyotokea Zanzibar na kuondoka kwa Wazanzibari wasiopungua 1,370. Hali kadhalika tukio hili la Titanic linafanana sana na ajali iliyotokea ya MV Bukoba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kama Mbunge, napenda kuishauri Ofisi ya Waziri Mkuu ni wakati sasa wakutengeneza museum za digital ambazo zitapelekea kizazi kijacho kuweza kuwa na kumbukizi na Taifa kuweza kujipatia kipato katika museum kama hizi, haswa nilipoona kwamba kiingilio katika museum ile ya Titanic ilikuwa ni takribani Shilingi Laki Moja sawa na Dola ya Kimarekani 49.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kama tutakwenda katika muundo kama huu yanapotokea maafa makubwa kama haya na kuweza kuyawekea museum maalum, tunaweza hata kukusanya kipato ambacho kinaweza kikasaidia hata angalau kuwasomesha wahanga wale ambao wazee wao waliathirika kwa kiasi kikubwa, katika Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiachana na majanga kama haya pia yaliyojitokeza nilijionea pia mfanano mkubwa sana niliyoiona katika museum ya JF Kennedy na tukio lilotokea pale Zanzibar tarehe 7 Aprili, 1972 la kupigwa risasi hadharani Rais wetu wa kwanza wa Zanzibar Hayati Mzee Karume.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo bado halijatengenezewa museum hasa yakuweza kutueleza ilikuwaje na unaweza ukakuta hata mwanafunzi wa Chuo Kikuu sasa hivi asiwe na picha halisi ya kukueleza namna gani lile tukio lilitokea siku ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo haja sasa Mheshimiwa Waziri Mkuu ofisi yako iweze kutengeneza museum mahsusi ya kuweza ku-display hasa historia muhimu kama hizi. Ukienda Zanzibar leo pale ofisi kuu utamkuta Mzee Baraka Shamte atakuelezea ilikuwaje lakini Mzee Baraka Shamte hataishi milele, tutengeneze digital museum ambayo itaweza ku-display matukio muhimu ya kihistoria kama haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo hata ile museum yetu iko pale kwa Mwalimu Nyerere Butiama pia tuangalie namna gani ya kuweza kuitengeneza iwe katika hali ya kidigitali zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema mchango wangu uende katika masuala hayo ya maafa ili tuweze kuwa na rekodi ambazo zitakuwa kumbukizi ya muda mrefu ili na watoto wetu, wajukuu zetu waweze kuja kujionea hasa nini nchi imepitia, athari zilizojitokeza zilisababishwa na nini ili kuweza ku-overcome hizo situation zisiweze kujirudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)