Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa mwaka 2022/2023. Vilevile nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianzie ukurasa wa 18 Ibara ya 26 ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu anazungumzia habari ya kufanya mapitio ya sera ya uwekezaji. Tanzania tuna Wizara ya Uwekezaji na Ukuzaji wa Mitaji kwa Umma. Ukiitazama bajeti ya Wizara hiyo na kama Wizara hiyo itaamua sasa kuihamishia bajeti hiyo kwenye kukuza mitaji ya wananchi wenzetu tutasogea mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini nataka kusema hapa. Badala ya kila siku kusema Wizara inashughulika na sera, hapana! Wizara sasa iende ikuze mitaji ya watu na ituletee orodha ya wananchi ambao mitaji yao imekuzwa. Hivyo ndivyo tutakavyotengeneza mabilionea wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusiwe na Wizara za kisera tu, sasa una Wizara ya Uwekezaji na Ukuzaji wa Mitaji ya Umma halafu huna mtu hata mmoja wa kutolea mfano kwamba mtaji wake umekuzwa, hiyo inasaidia nini? Haisaidia chochote!

Mheshimiwa Mweyekiti, kwa hiyo ninataka niishauri Serikali kama kweli tuna Wizara ya Uwekezaji na Ukuzaji wa Mitaji ya Umma basi mwakani watuletee hapa orodha ya wafanyabiashara waliokuwa na mitaji midogo, mitaji yao imekuzwa nakufikia hatua ya juu. Vinginevyo tutakuwa na Wizara inatamkwa vizuri lakini kazi inayofanyika haionekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia habari ya mfumuko wa bei. Juzi hapa tulipata maoni mengi sana kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge. Tulimsikia Mheshimiwa Shabiby akisema, tukamsikia Profesa Kitila Mkumbo akisema, tukamsikia Mheshimiwa Tabasam akisema. Nini nataka kusema hapa, ili tuwe na uelewa wa pamoja tunaomba Wizara pamoja na taasisi zake ikiwemo EWURA waje hapa Bungeni watupe semina ya pamoja tenda zinatolewaje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa na uelewa wa pamoja Wabunge ni rahisi sana kuishauri Serikali vizuri kuliko kila Mbunge akiwa na uelewa wake. Huyu anasema tenda zinatolewa kimagumashi, huyu anasema watu wanne ndiyo wanaopanga, haya mambo yanaumiza sana watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie nchi yetu tusisahau kwamba ni nchi maskini na Wabunge hata nikiwemo ninayezungumza natokana na familia maskini. Kuna watu leo wanashindwa kula, wanakula mlo mmoja, hali ni mbaya sana mtaani hatuwezi kufanya kama hatuoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali wakati wa njaa kubwa ikitokea hapa, tunaona Serikali inafungua maghala ya Serikali inashusha bei ili kupunguza makali. Vipi Serikali haifungui maghala ya mafuta ya Serikali? Kama haina kwa nini? Kwa nini tusianze mchakato wa kutengeneza maghala tuwe na mafuta ya Serikali ikitokea bei kubwa kama hii Serikali inafungua maghala yake inashusha bei ina-regulate, mambo yanakaa sawa. (Makofi)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti taarifa!

MWENYEKITI: Taarifa kutoka wapi?

T A A R I F A

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimweleze mchangiaji kwamba Serikali inayo maghala, inayo maghala TIPER, Oryx ana 49 na Serikali ina 51, Serikali ina maghala mengine tena kama BP, kule BP ambapo sasa hivi ni PUMA tuna zaidi ya Milioni 80 ya kuhifadhi mafuta. Endelea mchangiaji.

MWENYEKITI: Unaipokea taarifa Mheshimiwa. Haya endelea.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naipokea taarifa yako Mheshimiwa Tabasam. Ninaiomba Serikali ifungue maghala kama yapo. Ndugu zangu mnakumbuka Waheshimiwa Wabunge wote wakati wa shida ya chakula Serikali hufungua maghala yake na kushusha bei ya mahindi. Ikishusha bei ya mahindi tunaona wafanyabiashara nao wanashusha. Kama Serikali ina maghala na ina mafuta iyafungue sasa ili bei ya mafuta ishuke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani tuwe tunazungumza tu yatapanda tena. Lakini vilevile Mheshimiwa Mwenyekiti hebu ninaomba nisaidie muda wangu huo. (Makofi)

MWENYEKITI: Unazungumza na kiti, endelea.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali…

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa!

MWENYEKITI: Taarifa kutoka wapi? Mheshimiwa Shangazi aah! umesimama hapo. Mheshimiwa Shangazi taarifa. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza pamoja na mchango mzuri wa mzungumzaji lakini ninataka tu nitoe taarifa kwamba Serikali ina zile facility lakini stock iliyoko kwenye maghala yale siyo ya Serikali. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Lusinde unapokea taarifa?

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama taarifa ya Mheshimiwa Shangazi ni ya kweli basi tuna mtihani mkubwa sana. (Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Endelea Mheshimiwa Lusinde.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mtihani mkubwa kwa sababu jambo kubwa kama hili ndugu zangu hivi hata kweli ndio imetokea shida purukushani hayo mafuta tunayatoa wapi? Hili ni jambo kubwa sana ni suala la usalama wa nchi. Kweli kabisa Taifa hili likose maghala ya Serikali ya kutunza mafuta? Hii ni hatari. Hatari kubwa sana hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ninakuomba Serikali kama kweli hakuna, hili tatizo ni kubwa wala siyo jambo la kufumbia macho, tuende tupange bajeti tuanze kutengeneza maghala ya kutunza mafuta ili tuwe na hifadhi ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine mimi nakushuru sana.

MHE. CHARLES J. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa!

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwijage taarifa.

T A A R I F A

MHE. CHARLES J. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpe taarifa mzungumzaji kwamba pamoja na Serikali haina mafuta kwenye maghala yale ya kwake lakini kutokana na location advantage na mfumo wa kudhibiti mafuta Tanzania nchi yetu iko salama na ina mafuta ya kutosha. (Makofi)

MWENYEKITI: Unapokea taarifa Mheshimiwa Lusinde?

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani sasa tena Mwijage unataka kunipiga siasa hata mimi Mbunge mwenzako bwana? Hili jambo ni zito. Jamani eeh! hili jambo ni kubwa. Hili jambo tusiliongelee kwa lugha hiyo. Tusipige siasa kwenye mambo ya hatari. (Makofi)

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wajumbe muacheni Mbunge achangie; endelea Mheshimiwa Lusinde.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi kufika mahala inakosa akiba ya mafuta ya Serikali halafu tunasema nchi iko salama! tunasema hali ni nzuri! Hii jamani tutakuwa tunajifungia humu ndani tunajidanga. Hapana, hapana, hapana! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tuwe na utaratibu mzuri na nataka nikwambie, nisikilize. Sisi hali hii siyo ya kwanza, alizungumza hapa Profesa. Sisi vita imeshapigana kwenye eneo ambako ndiko tunanunua mafuta. Ishapigana na Uajemi vita lakini hali yetu haikufikia kama hii ambayo vita inapigana Urusi ambako ni mbali. Sasa hebu niambie kama hali hii vita wanapigana Urusi na Ukraine. Je ingepigana hapa OPEC ambako ndiko tunanunua mafuta tungeishi hapa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kuna watu wanashindwa kufikisha wagonjwa hospitalini wanakufa. Ndugu zangu kukodi pikipiki gharama imeongezeka mara kumi. Vijijini huko lita moja ya petrol inauzwa Shilingi Elfu Nne, nani atakubali kumsafirisha mgonjwa wako kumkimbiza? Ambulance za Watanzania ni pikipiki za vijijini!

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo lazima tuyazungumze katika ukubwa wake tusiweke mambo ya siasa kwenye jambo hili, hapana tumsaidie mama kwenye jambo hii. (Makofi) Kwa hiyo, mimi ninasema hapa hii itasaidia kushusha mfumuko wa bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna miaka 60 ya kuongoza hili Taifa, tunashindwaje kuwa na hifadhi ya mafuta ya kwetu, tunashindwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya naona alikuwa amesimama Waziri wa Fedha.

MWENYEKITI: Nimemuona Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango.

T A A R I F A

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitambue mchango wa mchangiaji na jambo analochangia ni jambo la msingi na ni jambo kubwa, kitu ambacho ninataka kukisema ni kwamba sambamba na mchango wake na dira hiyo anayoisema, Serikali inalifuatilia kwa umakini mkubwa sana jambo hili na siyo tu kwa maana ya hivi vita vinavyoendelea pamoja na majanga mengine yanayojitokeza lakini Wizara imeendelea na dira hiyo hiyo ya kufufua Tanzania iwe na akiba ya kutosha na siyo tu yakutosha kwa maana na majanga lakini iwe focal point kwa sababu ni entry ya nchi nyingi za ukanda huu hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo tunaenda kuwa na akiba ya kutosha siyo tu kwa ajili ya majira haya ya sasa ya vita, lakini tutakuwa na utaratibu tu wa kuwa na mafuta ya kutosha na actualy tuta-supply na kwenye nchi majirani kwa sababu lango la mafuta haya katika ukanda huu linapitia kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuhusu hiki kinachoendelea ambacho ni cha sasa hivi, tumesema hata jana tumetoa kauli ambayo tumewaambia wananchi kwamba tunaenda kuangalia baadhi ya maeneo ambayo hayagusi Development Budget yanayogusa Other Charges matumizi ambayo yanaenda kwa njia ya makato kwenye TBS, EWURA na maeneo mengine TPA, customs tunaenda kuyaangalia yale ili tuweze kuchomoa ili kuweka unafuu kwa wananchi na wakati ule ule Hazina iweze kuzisaidia zile taasisi zilizokuwa zinachukua kwenye mafuta. Maana yake tutoe unafuu kwa wananchi lakini Hazina na taasisi zingine ambazo zilikuwa zinachukua kwenye eneo lile tuweze kuangalia namna ya uendeshaji ndani ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili ni jambo ambalo linafanyiwa kazi na liko kwenye vipaumbele vya Mheshimiwa Rais na viko kwenye dira ya Wizara na Serikali inaipa umuhimu mkuwa kwa sababu mafuta ni injini ya uchumi wa nchi yoyote ile.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Lusinde.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, bado narudia kwanza tukubaliane kwamba ni lazima tuwe na hifadhi ya mafuta ya kwetu kama nchi, kama Taifa. Mafuta ya Serikali kuacha hivi visheli vya Serikali magari yanapita Mawaziri kuweka mafuta. Tuwe na hifadhi ya mafuta ya nchi, sisi kama Taifa ili hata ikitokea huko duniani kuna shida, sisi tunakuwa nayo. Jamani tunashindwaje kutunza? Watu wa kawaida tu wanatunza chakula wakati wa njaa anaenda anafumua watoto wanaishi, hayo ndiyo ninayoyataka maono yetu yawe hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni lazima inapotokea crisis kubwa kama hii tuiangalie jamii. Tuangalie maisha ya watu mtaani tunayafanyaje? Haiwezekani tuwe tunaendelea kupanga. Tunapanga maendeleo, tunapanga matumizi makubwa kana kwamba hakuna tatizo. Hiyo haiwezekani! Tukijifungia humu tuelewe kwamba Watanzania wana wakati mgumu sana kutokana na hii hali iliyopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nihame hapo niende kwenye kilimo. Hebu niwaombe Serikali Maprofesa wale wa SUA pale watutengenezee mtaala wa kilimo ufundishwe kuanzia shule ya msingi mpaka sekondari. Kwa kufanya hivyo tutakuwa na wataalam wa kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anayeishia Darasa la Saba atakuwa anajua kilimo kwa kiwango fulani. Anayeishia Sekondari atakuwa anajua kilimo kwa kiwango fulani. Kwa utaratibu huo watu watalima kilimo siyo cha chakula tu. Tutakuwa na kilimo cha biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani Taifa kama hili tunazungumzia habari ya kumpa leo mtu pikipiki, kumpa Afisa Ugani kipimo. Yale yote tukiyafundisha shuleni tutakuwa na Maafisa Ugani wa kiwango hicho nchi nzima. Lazima watu wetu wafundishwe namna ya kutunza chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Kilimo Bashe, anafanya kazi vizuri sana lakini tumuongezee nguvu kwa kutengeneza mtaala wa elimu ya kilimo ufundishwe mashuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nataka kuzungumza ni kuhusu ahadi za viongozi. Hivi ndugu zangu akiahidi Rais kwa Watanzania nitafanya jambo Fulani, halafu nyinyi watu wa Wizara hiyo hamtekelezi, ndiyo maana mwaka jana nilisema na leo narudia, tuweke kwenye kitabu kimoja ahadi za Marais, ziandikwe kwenye kitabu cha peke yake ili mwakani anaposimama hapa Waziri Mkuu anatueleza katika ahadi za Marais walizoahidi sehemu fulani imetekelezwa hii, imetekelezwa hii, imetekelezwa hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa utaratibu huu wa kwenda pamoja hivi tutakuwa tunatoka kwenye reli. Wananchi wanashangaa Rais anaahidije jambo lisitekelezwe? Sasa wasubiri nani aahidi? Rais alishaahidi kutengeneza barabara ya Mvumi kwa lami. Alishaahidi kujenga pale barabara ya Mvumi kwenda kuunganisha na barabara ya Iringa, leo ni hii mwaka wa 10 huu ni Mbunge nazungumzia ahadi ya Rais. Sasa watu wanauliza hivi akisema Rais kuna nani mwingine tena mkubwa wa kuzuia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivyo Marais wameahidi kwa Wabunge karibu wote. Tutengenezeeni kitabu hata Ilani, tutengenezeeni kitabu cha ahadi za Marais waliopita na zilivyotekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la MSD Rais alishalitolea maamuzi suala hili. Rais ameagiza kwamba MSD ifanyiwe overhauling, sasa Wabunge kuanza kueleza nani alikuwa anafanya kazi vizuri. Nani aaah! siyo kazi ya Bunge, tusubiri hiyo overhauling inafanyikaje, tumuache Rais atengeneze pale ili utaratibu uweze kwenda. Rais amesema haraka kwa hiyo nina hakika kabisa soon mambo yatakaa sawa pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie jambo kidogo hapa, kuna maneno yanazungumzwa mitaani kuhusu Mheshimiwa Waziri Nape kuzunguka kwenda kuhamasisha anuani za makazi. Hapa ndipo panatuonesha wapi lipo tatizo. Tatizo lilipo siyo kwa Nape. Mheshimiwa Nape ameona kazi iliyofanyika mpaka sasa hivi ni asilimia 68 bado asilimia 32 na muda umeisha. Nategemea kwamba baada ya kumaliza ziara Mheshimiwa Nape hili jambo tutakuwa tumelikamilisha kwa asilimia 100. Kuna viungo vyetu havifanyi kazi sawa sawa. Tuna Wakurugenzi, tuna Wenyeviti, tuna Watendaji, tuna Ma-DC kwa hiyo, tuna uhakika akirudi hapa atatuambia wapi panavuja ili tuweze kusukuma nchi iweze kwenda. Kwa hiyo tusilaumu tu. (Makofi)